NURU TUKUFU YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W.)

NURU TUKUFU YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W.)
1.    Sheikh Shahabuddin Qastalani katika kitabu chake Mawahib al- Ladunniyyah ameandika hivi:- Alipokusudia Mwenyezi Mungu  kuwaumba viumbe vyake, aliichomoza Nuru ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.); Nuru ambayo ni tukufu ndipo akaumba dunia.
2.    Amehadithia Bwana Jabir bin Abdullah Ansari: “Nilipomwuliza Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ‘Ya RASUL-ALLAHI wazee wangu nakufidia, ni  julishe kiumbe yupi aliumbwa mwanzo?’. Akanijibu ‘Ewe Jabir, Mwenyezi Mungu aliumba nuru ya Mtume wake kutokana na nuru yake kabla ya  kuumba chochote’”.

3.    Na vile vile Sayyidna Ali (a.s.) ameeleza kwamba mpenzi wa Mwenyezi Mungu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) amesema: “Mwenyezi Mungu ameumba nuru yangu miaka kumi na nne elfu kabla ya kumuumba Nabi Adam (a.s.)”.

4.    Mwanahistoria maarufu wa Ki-Islamu Bwana Abul-Hasan Ali bin Husain al-Mas’udi katika kitabu chake maarufu cha historia kiitwacho  Muruj adh-dhahab wa Ma’adin al-Jawahir, amepokea hadithi hii  kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba Mwenyezi Mungu alipotaka  kuumba dunia na watu na kila kilichomo ndani ya dunia, basi  kwanza kabla hakuiumba hii ardhi, kwa upekee kwa Nuru yake Jalali  akaidhihirisha nuru yenye kung’aa kutokana na nuru yake na ikawa ile nuru inatoa cheche za nuru na mshabaha wa sura; tena  akakusanya zile sura akaifanya sura moja na ikatokeza sura ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), basi hapo Mwenyezi Mungu akaikhutubia ile sura na kusema “Wewe ndiye niliyekuchagua, na wewe ndiye nuru yangu, kwako wewe nimewacha hazina ya uwongofu na kwa ajili yako (kwa mapenzi juu yako) mbingu nitainyanyua; na ardhi (dunia)  nitaitandaza na maji nitawacha yamiminike na yaende; na kujaalia thawabu na adhabu, Pepo na Jahannam (Moto) kwa watii na wasiotii; na nitawafanya Aali yako (AHLUL-BAYT) kuwa viongozi wa Haqi, na nitawajaza kwa elimu hata wasishindwe kueleza au kuwafahamisha Umma mushkili wowote wala jambo lolote lililofichika wasishindwe kulieleza, na nitawafanya wao (AHLUL-BAYT) wenye Hoja na Mfano juu ya viumbe wangu na kuwa nabihisha (kuwafahimisha upekee/ Wahdaaniyah) wangu na Qudra yangu juu ya viumbe vyote”. Baadaye Mwenyezi Mungu akachukuwa Ahadi kwa kuyakubali yote, na kabla hakuchukua hiyo Ahadi akawajulisha viumbe vyote kwa kumchagua Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Aali zake kuwa ni viongozi wa  Haqi na wamechaguliwa naye ili iwe ndio njia ya uadilifu na viumbe wasiwe na udhuru wowote wa kwamba hawakujua.

5.    Bwana Abul Qasim al-Tabarani (360 A.H.) katika kitabu chake  Muj’am al-Kabeer anahadithia kutokana na Bwana Ibn Abbas kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Mimi nilikuwa Mtume wakati Adam (a.s.) alipokuwa kati ya roho na kiwiliwili (maana yake bado umbo la Nabi Adam lilikuwa halikukamilika)”.


Huu ndio ukweli kuwa Mtume Muhammad (saww) ndio Mtu wa kwanza kuumbwa na Mungu aliwachagua Ahlulbayt kuwa makhalifa wa Mtume kabla hata ya dunia kuumbwa. Hapa hakuna Abubakar wala Umar. Makhalifa ni Ahlulbayt tu. Na jumla ya makhalifa ni 12. Wa kwanza wao akiwa ni imam Ally na wa kumi na mbili wao ni imam Muhammad Mahdi (a.s).

Comments