BAHLUL AMSIHI FADHIL IBN RABI'I

BAHLUL AMSIHI FADHIL IBN RABI'I

Siku moja Waziri wa khalifa (wa bandia) Harun Rashid, Fadhil ibn Rabii alikuwa akipita njia moja hapo alimkuta Bahlul ameketi akiwa ameinamisha kichwa chini akiwa anawaza. Fadhil alisema kwa sauti, "Ewe Bahlul! Je, unafanya nini?"

Bahlul alikiinua kichwa na alipomwona Fadhil, alisema: "Nimekuwa nikiwazia yatakayokupata kwani yaliyompata Jaafar Barki ndiyo hayo hayo yatakayokupata wewe."

Kwa hayo, moyo wake Fadhil ulitingisika, na akasema: "Ewe Bahlul! Mimi nimeweza kusikia hali hiyo kutoka watu tofauti tofauti, lakini sijawahi kukusikia wewe, hivyo nitapenda kukusikia, juu ya kuuawa kwa Jaafer."

Bahlul akaanza kuelezea:"Katika zama za Ukhalifa wa Mahdi, Yahya aliteuliwa kuwa Katibu na mshauri wa Harun Rashid. Katika kipindi kifupi, Harun, Yahya na Jaafer (rafiki wa Yahaya) walishikamana mno. Harun na Jaafer walipendana mno hadi Harun dada yake Abbasa, kuolewa na Jaafer. Lakini pamoja na ndoa hiyo, alimpa sharti la kutomwingilia dada yake. Lakini Jaafer alimwingilia kimwili, na hapo Harun alipopata habari hizo aligeuza urafiki wake katika uadui na upingamizi. Kila wakati alikuwa akibuni mbinu za kumwua na kuuteketeza ukoo wao mzima. Usiku mmoja alimwambia mtumwa wake Mansur: "Mimi nataka usiku wa leo uniletee kichwa cha Jaafer."Kwa hayo, Mansur alishtushwa na kukiinamisha kichwa chake chini. Hapo Harun alimwambia: "Je kwa nini umenyamaza na wawaza nini?"

Mansur alimjibu: "Loh! Kazi hii ni kubwa mno, lau ingeliniijia mauti kabla ya kuamriwa kazi kama hii."

Harun alimjibu: "Iwapo hutaitekeleza amri yangu hii, basi utanaswa na ghadhabu na adhabu zangu na utambue wazi wazi kuwa nitakuua vile hadi wanyama pia watakuhurumia."

Mansur kwa khofu ya mdhalimu huyo aliingia nyumbani mwa Jaafer na kumwelezea vile hukumu ilivyokuwa.

Jaafer alimwambia: "Labda hukumu hii ameitoa akiwa katika hali ya ulevi na kutakapokucha atajuta, hivyo nakuomba uende kwa Khalifa na umjulishe kuuawa kwangu. Iwapo utakuta hakuna athari zozote za kujuta na kusikitika hadi asubuhi basi, utambue kuwa nitakuwekea kichwa changu tayari kwa upanga wako."

Mansur hakuweza kusadiki maneno ya Jaafer, na alimwambia: "Nataka wewe ufuatane nami hadi kwake Harun Rashid, labda inawezekana akakusamehe kwa upendo wako alionao."

Jaafer aliyakubalia maneno ya Mansur na alijitolea kwa maangamizi yake. Basi Mansur alitokezea mbele ya Harun akiwa anatetemeka.

Harun aliuliza: "Mansur, je umetekeleza?" Mansur alimjibu:"Nimemleta Jaafer, yupo nyuma ya pazia amesimama."

Khalifa akawa amekasirika, alisema: "Iwapo utachelewa hata punde kutekeleza amri yangu, basi nitahakikisha kuwa wewe uuawe kwanza."

Baada ya mazungumzo hayo, hapakuwapo na fursa ya kupoteza. Mansur alimkimbilia Jaafer, kijana mtanashati, na mwema, na kumkata kichwa na kukileta mbele ya Harun.

Khalifa huyu aliyekosa huruma, hakukomea hapo tu, bali aliamrisha kuuangamiza ukoo mzima na mali na vitu vyao vyote kuchukuliwa. Mwili wa Jaafer usio na kichwa ulininginizwa katika jumba la Khalifa na baada ya siku chache ukachomwa moto.

Sasa ewe Fadhil! Mimi nahofia matokeo yako. Nahofia matokeo yako pia yasiwe kama yale yaliyompata Jaafer."

Fadhil alishtushwa mno kwa mazungumzo ya Bahlul, na alimwambia Bahlul kuwa "Niombee usalama wangu!"

Comments