1. Sheikh Shahabuddin
Qastalani katika kitabu chake Mawahib al-Ladunniyyah ameandika
hivi:- Alipokusudia Mwenyezi Mungu kuwaumba viumbe wake, aliichomoza
Nuru ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.); Nuru ambayo
ni tukufu ndipo akaumba dunia.
Amehadithia Bwana Jabir
bin Abdullah Ansari: “Nilipomwuliza Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ‘Ya RASUL-ALLAHI
wazee wangu nakufidia, nijulishe kiumbe yupi aliumbwa mwanzo?’. Akanijibu ‘Ewe
Jabir, Mwenyezi Mungu aliumba nuru ya Mtume wake kutokana na nuru yake kabla ya
kuumba chochote’”.
Na vile vile Sayyidna
Ali (a.s.) ameeleza kwamba mpenzi wa Mwenyezi Mungu Mtume Muhammad (s.a.w.w.)
amesema: “Mwenyezi Mungu ameumba nuru yangu miaka kumi na nne elfu kabla ya
kumuumba Nabi Adam (a.s.)”.
2. Mwanahistoria maarufu
wa Ki-Islamu Bwana Abul-Hasan Ali bin Husain al-Mas’udi katika kitabu chake
maarufu cha historia kiitwacho Muruj adh-dhahab wa Ma’adin al-Jawahir,
amepokea hadithi hii kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba Mwenyezi Mungu alipotaka
kuumba dunia na watu na kila kilichomo ndani ya dunia, basi kwanza kabla ya kuiumba
hii ardhi, kwa upekee kwa Nuru yake Jalali akaidhihirisha nuru yenye kung’aa
kutokana na nuru yake na ikawa ile nuru inatoa cheche za nuru na mshabaha wa
sura; tena akakusanya zile sura akaifanya sura moja na ikatokeza sura ya Mtume Muhammad
(s.a.w.w.), basi hapo Mwenyezi Mungu akaikhutubia ile sura na kusema “Wewe
ndiye niliyekuchagua, na wewe ndiye nuru yangu, kwako wewe nimewacha hazina ya
uwongofu na kwa ajili yako (kwa mapenzi juu yako) mbingu nitainyanyua; na ardhi
nitaitandaza na maji nitawacha yamiminike na yaende; na kujaalia thawabu na
adhabu, Pepo na Jahannam (Moto) kwa watii na wasiotii; na nitawafanya Aali yako
(AHLUL-BAYT) kuwa waongozi wa Haqi, na nitawajaza kwa elimu hata wasishindwe
kueleza au kuwafahamisha Umma mushkili wowote wala jambo lolote lililofichika
wasishindwe kulieleza, na nitawafanya wao (AHLUL-BAYT) wenye Hoja na Mfano juu
ya viumbe wangu na kuwa nabihisha (kuwafahimisha upekee/
Wahdaaniyah) wangu na
Qudra yangu juu ya viumbe vyote”. Baadaye Mwenyezi Mungu akachukuwa Ahadi kwa
kuyakubali yote, na kabla hakuchukua hiyo Ahadi akawajulisha viumbe vyote kwa
kumchagua Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Aali zake kuwa ni waongozi wa Haqi na
wamechaguliwa naye ili iwe ndio njia ya uadilifu na viumbe wasiwe na udhuru
wowote wa kwamba hawakujua.
3. Bwana Abul Qasim
al-Tabarani (360 A.H.) katika kitabu chake Muj’am al-Kabeer anahadithia
kutokana na Bwana Ibn Abbas kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Mimi nilikuwa
Mtume wakati Adam (a.s.) alipokuwa kati ya roho na kiwiliwili (maana yake bado
umbo la Nabi Adam lilikuwa halijakamilika)”.
Comments
Post a Comment