Kuamini yasiyonekana ni sehemu muhimu katika Imani ya
kiislamu. Mfano wa haya ni kumwamini Allah, kiama, Jahanam na pepo, malaika,
majini, mitume, vitabu. Mambo yote haya kwa dhahiri tumeyaamini bila kuyaona.
Safari ya Usiku (Isra) ni sehemu hii ya kutakiwa
kuamini tusiyoyaona kwa macho yetu na hiki kilikuwa kipimo cha kuipima imani ya
waislamu wa awali. Wapo waliolikubali tukio hili na wapo waliolikataa katakata
na kuacha kabisa Uislamu.
Tukio
hili limeandikwa katika Qur’an na hadith na lina sehemu mbili. Sehemu ya kwanza
ni kusafiri kutoka Maka hadi Yelusalem (Israa) na sehemu ya pili ni kutoka Yerusalem
hadi mbinguni (miraj).
Mtume Mohammad (s.a.w.w)
alianza safari akiwa na malaika Jibrail kutokea nyumba ya Umm Al-Hani dada wa
Imam Ally (a.s) katika mji wa Maka kwa kumtumia mnyama aitwaye Buraq hadi
msikiti wa baitil Aqsa ulioko Palestina ya sasa. Alipitia maeneo kadhaa kama
vile Bayt al Laham (Bethlehemu), mahala alipozaliwa Nabii Issa (Yesu). Akiwa angani
aliona umbile zima la ulimwengu na sayari na nyote zilizosheheni angani. Pia aliongea
na malaika na roho za mitume waliomtangulia. Tena akiziona kwa karibu zaidi
Pepo na moto wa Jahanam.
Safari hii iliishia sehemu iitwayo Sidratul
Muntaha, mahala patakatifu palipojaa nuru kila aina ya miujiza. Alirejea nyumbani
kwa kupitia njia ile ile aliyoendea.
Wakati akirejea aliupita
msafara wa kibiashara wa Makuraish ambao katika safari yao walimpoteza ngamia
mmoja na wakiwa wanamtafuta. Mtume alikunywa maji waliyokuwa wamebeba watu
hawa. Jua lilipochomoza alikuwa amekwisha fika pale pale nyumbani kwa Umm Hani.
Aliwakusanya Makuraish na
kuwahadithia kuhusu safari yake hii. Habari hizo zilienea kwa kasi na kumfikia
kila mtu katika eneo hilo. Makraish hawakuamini kabisa masimulizi haya ya Mtume
Makraish wakaanza kuulizana
kuhusu ni nani anayejua vyema namna ulivyomsikiti wa Baitil Aqsa ili aulize
Mtume (s.a.w.w) aeleze ukoje ili kuthibitisha kama alifika huko.
Alipoulizwa Mtume kufafanua
msikiti ule ukoje, akaeleza vizuri sana na tena akaongeza kwa kuwaeleza tukio
la msafara wao wa biashara na namna walivyokuwa wakimtafuta ngamia aliyepotea.
Comments
Post a Comment