UADILIFU WA MWENYEZI MUNGU KWA MUJIBU WA SHIA

Kumtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu kutokana na dhulma na upuuzi na uongo wa Mawahhabi, kumefundishwa na Maimamu waongofu ambao ni taa ziondoazo kiza, na wao ndio mwangaza wa Ummah. (maimamu 12 wa Shia ndio wanaofafanua vizuri zaidi uadilifu wa Allah)

Hebu basi na tumsikilize mlango wa mji wa elimu Amiri wa waumini Ali ibn Abi Talib (a.s.), anawafafanulia watu itikadi hii ambayo imeendelea kutokutambulika kwa baadhi ya Waislamu ambao wameuacha mlango huo yeye anasema alipoulizwa na mmoja wa wafuasi wake, "Je, kwenda kwetu Shamu kulikuwa kunatokana na Qadhaa (maamuzi) ya Mwenyezi Mungu na Qadar yake?"
Anajibu Imam Ali (a.s.): "Ole wako, huenda wewe umedhania kuwa Qadhaa ya kulazimisha na Qadar yenye kuwajibishwa, na lau ingekuwa hivyo thawabu na adhabu vingebatilika, ahadi na maonyo vingetenguka, hakika Mwenyezi Mungu amewaamuru waja wake kwa kuwahiyarisha na akawakataza kwa kuwatahadharisha. Akawalazimisha (kufanya mambo) mepesi na wala hakuwalazimisha (mambo) mazito. Akatoa (malipo) mengi kwa (matendo) kidogo na wala hawakumuasi hali ya kuwa ni mwenye kushindwa na hawakumtii hali ya kuwa ni mwenye kulazimisha. Wala hakuwatuma Mitume kwa ajili ya mchezo tu na hakuteremsha vitabu kwa waja ili iwe ni upuuzi, wala hakuumba mbingu na ardhi na vilivyomo bure bure tu. "Hizo ni fikra za wale waliokufuru basi ole wao waliokufuru kutokana na adhabu ya moto.  Amesema kweli Imam (a.s.) basi, ole wao kutokana na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu wale wanaomnasibishia Mwenyezi Mungu kufanya upuuzi na dhulma.
Ni vizuri kusema na haki husemwa, ya kwamba Ahlus-Sunna Wal-Jamaa wanamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumuepusha na upuuzi na dhulma, basi iwapo utamuuliza mmoja wao huenda kamwe asimnasibishe Mwenyezi Mungu na dhulma kwa utukufu wake, lakini huenda yeye mwenyewe akajikuta anaona vibaya kuzikataa hadithi zilizotolewa na Bukhari na Muslim na wakati huo huo akaziamini kwamba ni sahihi, kwa ajili hiyo utamuona wakati unamjadili kwa mantiki inayoingia akilini atadai kwamba hiyo kwa Mwenyezi Mungu siyo dhulma kwani yeye ni Muumba, na Muumba anawafanyia viumbe wake vile atakavyo, kwani yeye haulizwi kuhusu ayatendayo nao viumbe wataulizwa.
Wakati utakapomuuliza kwa kusema. Ni vipi Mwenyezi Mungu anamhukumu kiumbe kuingia motoni kabla ya kumuumba, eti kwa kuwa amemuandikia uovu na mwingine amemhukumia pepo kabla ya kumuumba kwa kuwa kamuandikia wema? Basi je, hiyo siyo dhulma kwa wawili hao kwa sababu yule atakayeingia peponi haingii humo kwa ajili ya matendo yake bali Mwenyezi Mungu kamchagulia, na vile vile atakayeingia motoni haingii humo kwa makosa aliyoyatenda bali Mwenyezi Mungu amemkadiria. Je, katika hali hiyo siyo dhulma na ni jambo linalopingana na Qur'ani?
Jawabu lake atakuambia; "Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anafanya atakavyo."
Huwezi kufahamu msimamo wake unaopingana; na hii bila shaka ni kwa sababu anampa Bukhari na Muslim daraja ya usahihi kama Qur'an, na anasema kuwa vitabu sahihi baada ya kitabu cha Mwenyezi Mungu ni Bukhari na Muslim.
    Ndani ya Bukhari na Muslim kuna maajabu na misiba ambayo Waislamu wamekumbwa na mtihani huo. Hakika Banu Umayyah na baada yao Banu Abbas wamefaulu sana kueneza uzushi wao na itikadi zao ambazo zinaafikiana na siasa zao mbaya, na athari zao zimebakia mpaka leo hii, kwani Waislamu wanazizingatia kuwa ni urithi bora kwa kuwa (wanaona) ni mkusanyiko wa hadithi sahihi za Mtume kama wanavyodai.Lau Waislamu wangefahamu kiwango ambacho (Banu Ummayah na Banu Abbas) walivyomzulia Mtume (s.a.w.w.) kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kisiasa, basi wasingezisadiki kabisa hadithi hizo na hasa zile zinazopingana na kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu amechukua jukumu la kuihifadhi Qur'an Tukufu, na Masahaba walikuwa wameihifadhi na wakawa wanaiaridhi kwa Mtume (s.a.w.w.) ndiyo maana (Banu Umayyah na Banu Abbas) hawakuweza kuigeuza wala kuibadilisha, na kwa hali hiyo basi wakaigeukia Sunna takatifu wakaweka waliyoyataka kwa ajili ya yule wamtakaye, khususan kutokana na uadui wao dhidi ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w.) ambao ndiyo walinzi wa Qur'an na Sunna. Walizua hadithi kwa kila tukio wakainasibisha kwa Mtume (s.a.w.w.) na wakairemba kwa Waislamu (na kuwambia) hadithi hizi ni sahihi kuliko nyinginezo, na watu wakazikubali kwa nia njema hali wakipokezana hadithi hizo kwa kurithiana kizazi baada ya kizazi tena kwa uadilifu kabisa. Mimi nasema kwamba Mashia nao ni mateka wa uharibifu na uzushi (uliofanywa) katika hadithi nyingi ambazo zinanasibishwa kwa Mtume (s.a.w.) au kwa mmoja wa Maimamu watukufu (a.s.). Lakini Shia hukataa kuziamini hadithi hizi za Uongo.

Comments