Hamna shaka kuwa historia ya mwanadamu ndio chemchemu
na chanzo cha maarifa, chanzo ambacho mataifa yanakihitaji katika safari yake
yenye kuendelea. Na ndio chanzo pekee chenye uwezo wa kuhuisha na kulisukuma
taifa mbele na kulipa sifa na hadhi maalum huku kikilifunganisha taifa hilo na
mizizi yake ya ustaarabu ambayo hulizuwia taifa dhidi ya mmong'onyoko.
Qur'ani imemhimiza kila mwanadamu, ikamtaka azame
ndani ya Historia ya mwanadamu na
azingatie yaliyomo ili awaidhike na kuongoka, hivyo Mwenyezi Mungu akasema:
"Je, hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo za kufahamia au masikio ya
kusikilizia?"1.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutoa historia ya
Adi, Thamudi, Firauni, watu wa miji iliyopinduliwa na watu wa Nuh akasema:
"Ili tuifanye ukumbusho kwenu na sikio lisikialo lisikie."2
Historia ya ujumbe mbalimbali wa Mwenyezi Mungu imejaa
masomo na mazingatio, masomo ambayo yameonyesha jinsi manabii watukufu walivyojali
mataifa yao ili kuyaokoa toka kwenye matatizo mbalimbali.
Pia ujumbe huo umeonyesha lengo na mwelekeo wake wenye
kujaa nuru na manufaa. Kwa ajili hiyo sira ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na
kizazi chake huwa ni tafsiri ya kivitendo ya misingi na sheria za kiislamu.
Hivyo kusoma sira yao na historia ya maisha yao ni
chanzo muhimu cha kuifahamu Qur'ani na Sunna, na ni chemchemu ya maarifa ya wanadamu
wote, kwa sababu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu alioutuma kwa wanadamu kupitia kwa
Nabii wa mwisho na mawasii wake wateule wakiwa ni viongozi wa wanadamu wote
bila kubagua.
Kwa kuwa umma wote umekubaliana juu ya wema na utakaso
wa viongozi wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu basi inafaa kuwafundisha watu historia
ya maisha yao ndani, kwani Qur’ani imetamka wazi kuhusu umaasumu na utakaso wao
ili wawe ni kiigizo chema kwa yule anayetarajia fadhila za Mwenyezi Mungu na malipo
mema ya Siku ya Kiyama.
Rejea
1. Al-Hajj: 46.
2. Al-Haaqah: 12.
Comments
Post a Comment