YANAYOHUSIANA NA HASARA NA MAJUTO KWA WAISLAMU

Kwa nini nisijute; bali ni kwa nini kila Muislamu asijute wakati usemwapo ukweli huu unaoelezea hasara waliyoipata Waislamu kutokana na kutengwa kwa Imam Ali kwenye Ukhalifa ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu alimtawalisha, na hivyo kuunyima umma (wa Kiislamu) uongozi wake na hekima, na elimu yake nyingi.
Na pindi Muislamu atakapochunguza bila ya chuki wala upendeleo, atamkuta Imam Ali ndiyo mwenye elimu na mjuzi mno kuliko watu wote baada ya Mtume (s.a.w), kwani tunashuhudia historia inayotuonesha kwamba wanachuoni wa Kisahaba walikuwa wakimuuliza Ali kwa kila lililowatatiza, na kauli ya Umar bin Al-Khatab aliyoisema zaidi ya mara sabini ya kwamba "Lau kama si Ali basi Umar angeliangamia' لولا علي لهلك عمر wakati ambapo Imam Ali (a.s.) hakupata kamwe kumuuliza Sahaba yeyote miongoni mwao.
Kama ambavyo historia inakiri kuwa Ali bin Abi Talib ni shujaa mno na mwenye nguvu kuliko Masahaba wote, na kuna mashujaa wengi miongoni mwa Masahaba waliokimbia vita katika sehemu nyingi tu, wakati ambapo Imam Ali (a.s.) alisimama imara mahala pote palipopiganwa vita, na inatosha kuwa ni dalili ile nishani aliyopewa na Mwenyezi Mungu pale Mtume (s.a.w.w) aliposema:
"Kesho nitampa bendera yangu mtu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye anapendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, mkali katika mapambano si mwenye kukimbia, Mwenyezi Mungu amekwisha unawirisha moyo wake kwa imani".
Masahaba wakaitamania (kuipata) bendera hiyo, Mtume akampa Ali bin Abi Talib.
Kwa kifupi, bila ya shaka maudhui ya elimu , nguvu na ushujaa, ni sifa ambazo Imam Ali alikuwa nazo, ni maudhui yanayofahamika kwa wote (Sunni na Shia) na ukiachilia mbali maandiko yanayojulisha kwa uwazi wa kuashiria juu ya Uimamu wa Ali, hapana shaka kwamba Qur'an haikubali uongozi na Uimamu isipokuwa kwa mtu mwenye elimu, shujaa tena mwenye nguvu.
Mwenyezi Mungu anasema kuhusu wajibu wa kuwafuata wanachuoni (wenye elimu). pale Allah (s.w) aliposema:-

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَآئِكُم مَّن يَهْدِى إِلَي الْحَقِّ قُلِ اللّهُ يَهْدِى لِلْحَقِّ اَفَمَن يَهْدِى إِلَي الْحَقِّ اَحَقُّ اَن يُتَّبَعَ اَمَّن لاَّ يَهِدِّى إِلاَّ اَن يُهْدَي فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ
[1]
Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina anaye ongoa kwendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je, anaye stahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?).
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu wajibu wa kumfuata mwenye elimu, shujaa tena mwenye nguvu:
وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ اللّهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكاً قَالُوَاْ اَنَّي يَكُونُ لَهُ الْمُلْكُ عَلَيْنَا وَنَحْنُ اَحَقُّ بِالْمُلْكِ مِنْهُ وَلَمْ يُؤْتَ سَعَةً مِّنَ الْمَالِ قَالَ إِنَّ اللّهَ اصْطَفَاهُ عَلَيْكُمْ وَزَادَهُ بَسْطَةً فِى الْعِلْمِ وَالْجِسْمِ وَاللّهُ يُؤْتِى مُلْكَهُ مَن يَشَاءُ وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ[2]
Na Nabii wao akawaambia: “Mwenyezi Mungu amekuteulieni Taluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi”.
"Wakasema, ni vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema, Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na kiwiliwili na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye, naye Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mwenye kujua".
Hapana shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu amemzidishia Imam Ali wasaa wa elimu kuliko Masahaba wote, akastahiki kuwa ni "Mlango wa elimu," pale Mtume Muhammad (s.a.w.w) aliposema aliposema:-
 انا مدينة العلم وعلي بابها"
akawa ndiye rejea pekee kwa Masahaba baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) nao Masahaba walikuwa kila wanaposhindwa kutatua mambo husema "Mas-ala haya magumu hakuna ayawezaye isipokuwa Imamu Aliy (a.s) ."
Na alimzidishia wasaa wa kiwiliwili, kwa kweli alistahiki kuwa simba wa Mwenyezi Mungu aliye mshindi, na nguvu zake na ushujaa wake ni wenye kupigiwa mfano katika kila zama kiasi kwamba wanahistoria wamesimulia visa vingi kuhusu ushujaa na nguvu zake visa ambavyo vinakurubia kuwa ni miujiza, kama vile kuung'oa mlango wa Khaybar, wakati ambapo Masahaba ishirini walishindwa hata kuutikisa. Na pia kuling'oa Sanamu kubwa la Hubal. kutoka juu ya paa la Al-Kaabah na kulisogeza jiwe kubwa ambalo jeshi lote lilishindwa hata kulitikisa, na mengineyo miongoni mwa riwaya mashuhuri.

Na Mtume (s.a.w.w) alimsifu na kumtaja kwa ubora mwana wa ammi yake Ali, na akazibainisha fadhila zake mahala mbali mbali na aliyatambulisha mambo yake maalum yanayomuhusu na daraja yake.
Kuna wakati Mtume akisema:
"Hakika huyu ni ndugu yangu na ni wasii wangu na ni Khalifa wangu baada yangu, basi msikilizeni na mumtii"
Na kuna wakati Mtume humwambia Ali (a.s.):
"Wewe kwangu mimi unayo daraja ya Harun kwa Musa isipokuwa hapana Nabii baada yangu".
Na kuna wakati mwingine Mtume akisema:
"Yeyote mwenye kutaka kuishi nilivyoishi mimi na kufa mauti (kama) yangu na akae katika bustani ya milele aliyoniahidi Mola wangu, basi na amtawalishe Ali bin Abi Talib, kwani yeye hatakutoeni kwenye uongofu na kamwe hatakuingizeni katika upotofu".
Na yeyote atakayefuatilia sera ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) atamkuta Mtume hakutosheka kwa kusema maneno tu na hadithi zinazomuhusu Ali, bali maneno yake yakionekana kwa matendo yake, kwani katika uhai wake Mtume katika uhai wake hakupata kumuwekea Ali amiri yeyote juu yake miongoni mwa Masahaba pamoja na kwamba alikuwa akiwawekea maamiri Masahaba wengine wao kwa wao. Hapana shaka kwamba Mtume aliwawekea Abubakar na Umar amiri (wa kuwaongoza) katika vita ya "Dhatus-Salasil" amiri huyo alikuwa Amr bin Al-As .
Kama ambavyo Mtume (s.a.w.w) aliwawekea Masahaba amiri ambaye alikuwa kijana mdogo Usamah bin Zaid na hilo alilifanya katika jeshi la Usamah kabla ya kufariki kwake yeye Mtume (s.a.w.w.).
Amma Ali bin Abi Talib hakuwa katika ujumbe wowote ila yeye ndiye amiri, hata kuna wakati fulani Mtume (s.a.w.w.) alituma ujumbe wa namna mbili, akampa uamiri Ali kwenye moja ya ujumbe huo na Khalid bin Walid akampa uamiri kwenye ule wa pili kisha akawaambia:
"Mutakapoachana kila mmoja awe amiri wa jeshi lake na mkikutana basi Ali ndiye amiri wa jeshi lote.”
Kutokana na maelezo yote yaliyotangulia tunakuta kwamba Ali ndiye mtawalia mambo ya waumini baada ya Mtume (s.a.w.w.) na haifai kwa yeyote yule kumtangulia.
Lakini kwa masikitiko makubwa, Waislamu wamepata hasara kubwa, na ndiyo maana wanapata taabu hadi leo na wanachuma matunda ya kile walichokipanda, na bila shaka waliokuja baadaye wamekwisha yatambua yale yaliyoasisiwa na hao waliotangulia.
Hivi kweli inawezekana kwa mtu yeyote kufikiria kuna Ukhalifa ulioongoka zaidi ya ule Ukhalifa wa Ali bin Abi Talib? Lau umma huu ungelifuata kile alichokichagua Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa kuwa Ali alikuwa ndiye mwenye uwezo wa kuuongoza umma (huu) kwa muda wote wa miaka thelathini juu ya mfumo mmoja kama vile alivyouongoza Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) bila ya mabadiliko yoyote. Tunasema hayo kwa kuwa Abu Bakar na Umar walibadilisha na wakafanya ijtihadi zao dhidi ya maagizo na matendo yao yakawa ndiyo sunna inayofuatwa. Othman naye alipokuja kwenye Ukhalifa akabadilisha mengi mno mpaka ikasemwa kuwa alikikhalifu kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake pia Sunna ya Abubakar na Umar, hapo ndipo Masahaba walipompinga na yakafanyika dhidi yake mapinduzi makubwa yaliyoangamiza Maisha yake na kusababisha fitna kubwa katika umma (fitna ambayo) jeraha lake halijapona hadi leo.
Ama Ali bin Abi Talib, yeye alikuwa akifungamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, hakwenda kinyume na yale anayoyaridhia Mwenyeezi Mungu, na ushahidi mkubwa wa hilo ni kwamba yeye Imam Ali alikataa kuchukua Ukhalifa pale walipomuwekea sharti ya kuhukumu kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake na sunna ya Makhalifa wawili waliomtangulia.
Huenda akauliza muulizaji: Basi ni kwa nini Ali anashikamana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna ya Mtume wake wakati ambapo Abubakar na Umar na Uthman walilazimika kufanya ijtihadi na mabadiliko?
Jawabu ni kuwa, yeye Ali anayo elimu ambayo wao hao hawakuwa nayo, isitoshe Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alimuhusisha kwa milango elfu moja ya elimu na katika kila mlango anaweza kufungua milango elfu moja.
Pia alimwambia: "Wewe Ewe Ali utaubainishia umma wangu yale watakayotofautiana ndani yake baada yangu. "
Amma hao Makhalifa walikuwa hawajuwi mambo mengi katika hukmu za Qur'an za dhahiri licha ya taawili ya Qur'an, hali hii wamethibitisha Bukhar na Muslim ndani ya sahih zao katika mlango wa kutayamamu ya kwamba, kuna mtu fulani alimuuliza Ummar bin Al-Khatab katika zama za Ukhalifa wake akasema yule mtu: "Ewe Amirul-Muuminina hakika mimi nimepatwa na janaba na sikupata maji, basi nifanyeje"? Umar akasema: "Usiswali"!! Kadhalika Umar hakuifahamu hukmu ya watoto wa ndugu wa kiume wa baba (ibnu Ammi) mpaka amekufa na hali ya kuwa anasema, "Natamani lau ningemuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu juu ya watoto wa Ammi".Wakati ambapo hukmu yake imetajwa ndani ya Qur'ani Tukufu, kwa hiyo Umar ambaye Masunni wanasema kuwa alikuwa miongoni mwa wenye kupewa Il-hamu (na Mwenyezi Mungu) hali ya elimu yake ilikuwa katika kiwango hiki, (basi kama Umar ni hivi) hao wengine wala usijisumbue kuuliza, hao ndiyo ambao waliingiza Bid'a (uzushi) ndani ya dini ya Mwenyezi Mungu bila ya kuwa na elimu wala uongofu wala kitabu cha kuwaongoza isipokuwa jitihada zao binafsi.
Na huenda msemaji akasema: "Ikiwa mambo ndiyo yako namna hii, basi ni kwa nini Imam Ali (a.s.) hakuubainishia umma yale ambayo walitofautiana ndani yake baada ya Mtume (s.a.w.w)"
Jawabu ni kuwa: Imam Ali (a.s.) hakuacha kufanya juhudi katika kubainisha yale yaliyoutatiza umma, na yeye alikuwa ndiye marejeo ya Masahaba kwa kila lililowatatiza alikuwa akija na kufafanua na kutoa nasaha. Hivyo basi walikuwa wakiyachukua yale wayapendayo na yasiyopingana na siasa zao na kuyaacha yasiyokuwa hayo, na historia ndiye shahidi mkubwa kwa haya tuyasemayo.
Kwa kweli lau siyo Ali bin Abi Talib na Maimamu miongoni mwa wanawe, basi watu wasingeyafahamu mafunzo ya dini yao, lakini watu (walivyo) ni kama ilivyotufunza Qur'an yakuwa hawaipendi haki, basi walifuata matamanio yao na kuzusha madhehebu dhidi ya Maimamu wa nyumba ya Mtume ambao serikali zilizokuwa katika wakati wao zilikuwa zikifuatilia kila wasemalo, wala hazikuwapa uhuru wa kushughulika na kufanya mahusiano ya moja kwa moja na watu.
Basi Imam Ali (a.s.) alikuwa akipanda juu ya mimbari na kuwaambia watu, "Niulizeni kabla hamjanikosa" Na yatosha kuwa Imam Ali ameacha Nahjul-Balagha, nao Maimam kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.w) wameacha elimu ambayo imeenea ulimwenguni na hilo wamelishuhudia viongozi wa Kiislamu Masunni na Mashia.
Sasa tunarudia kwenye maudhui na kusema: "Kwa msingi huu, lau Ali angewezeshwa kuuongoza umma kwa miaka thelathini kwa mujibu wa sera ya Mtume (s.a.w.) basi Uislamu ungeenea na kuimarisha itikadi katika nyoyo za watu zaidi na kwa undani wala pasingekuwa na fitna ndogo au kubwa wala (mauaji ya) Karbala yasingekuwepo wala msiba wa Ashuraa. Lau tutaukadiria uongozi wa Maimamu kumi na moja baada ya Ali, Maimamu ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwataja, na uhai wao uliendelea kwa kipindi cha karne tatu, basi pasingebaki hapa duniani miji isiyokuwa ya Kiislamu, na ulimwengu usingekuwa katika hali tunayoishuhudia leo hii na maisha yetu yangekuwa ya kibinaadamu kwa maana yake ya hakika lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
 "[3]الم, اَحَسِبَ النَّاسُ اَن يُتْرَكُوا اَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لاَ يُفْتَنُونَ"
"Alif Lam Mim, Je, watu wanadhani kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema: "Tumeamini" wasijaribiwe (wakapata Mitihani)? Umma wa Kiislamu umefeli katika mtihani huu kama vile zilivyofeli umma zilizotangulia, kama ambavyo Mtume wa Mwenyezi Mungu, alivyotamka katika minasaba mbali mbali na kamaambavyo Qur'an ilivyosisitiza mara nyingi ndani ya aya nyingi.



[1] Surat Yunus Aya ya 35
[2] Suratul-Baqarah Aya ya 247
[3] Surat Ankabuut Aya ya 2


Comments