Faqihi mashuhuri kutoka Khurasan alifika
Baghdad, alialikwa na khalifa wa kiwahhabi, Harun Rashid katika Baraza lake na
akimkalisha ubavuni mwake. Wakati alipokuwa akizungumza na Harun, alitokezea
Bahlul ambaye naye alikaribishwa aketi karibu nao. Huyo mtu alimwona Bahlul yu
kama mwehu na hivyo alimwambia Harun:
"Nimestaajabishwa na heshima na
mapenzi yako Khalifa, kwa kuwa unawastahi hata wehu hadi kuwakaribisha karibu
nawe?"
Alipoyasikia hayo Bahlul, alielewa kuwa
alikuwa akisemwa yeye tu na hapo akajikaza akamwambia: "Kwa nini waringia
ilimu yako hiyo kidogo, usinidharau kwa udhahiri wangu bali jitayarishe kwa majadiliano
ili nami nimdhihirishie Khalifa kuwa wewe haujui lolote!"
"Mimi nimesikia kuwa wewe u - mwehu
na hivyo siwezi kubishana na wehu!" Aliyasema huyo Faqihi.
Hapo Bahlul alimjibu akiwa ameghadhabika,
"Mimi ninaukubalia uwehu wangu lakini wewe unakataa kuukubalia ujahili
wako na kutokuwa na ilimu kamili."
Harun alipoyasikia hayo, alijaribu
kumtuliza Bahlul, lakini ilishindikana huku akidai kuingia katika mjadala na
huyo Faqihi, iwapo anajiamini kwa ilimu kamili."
Basi Harun alimgeukia huyo Faqihi na
kumwambia: "Je kuna kipingamizi gani katika kumwuuliza maswali?"
Hapo huyo Faqihi alijibu: "Mimi nipo
tayari kujadiliana naye iwapo atakubaliana na shuruti langu moja nalo ni, iwapo
ataweza kunijibu basi nitampa Dinar elfu moja za dhahabu na akishindwa itambidi
anilipe hivyo."
Bahlul alimjibu: "Kwa kweli mimi huwa
sina mali za kidunia na wala sina Dinar wala dhahabu, lakini nipo tayari kuwa
mtumwa wake iwapo nitashindwa kumjibu, na iwapo nitamjibu basi nipatiwe hizo
Dinar elfu moja za dhahabu ambazo nitazigawa miongoni mwa mafukara."
Kwa hayo, huyo mtu alianza kumuuliza swali
hivi: "Katika nyumba moja yupo mwanamke aliyeketi na mume wake halali kisheria
na humo humo wapo watu wawili ambao mmoja wao anasali na mwingine yupo katika
hali ya saumu. Ghafla anatokezea mtu kutokea nje na kuingia ndani ya nyumba
hiyo. Kutokezea huku kwa mtu huyo, wale bibi na bwana wanakuwa haramu baina yao
na sala na saumu za wale wawili zinakuwa batili. Je unaweza kuniambia huyo mtu
aliyotokezea ni nani?"
Bahlul bila ya kusita anamjibu: "Huyo
mtu aliyeingia nyumbani kwa ghafla alikuwa ndiye bwana wa kwanza wa yule bibi
kwani alikwenda safari na baada ya muda mrefu kupita, ilijulikana kuwa
amefariki na hivyo huyo mwanamke akaolewa na bwana wa pili (aliyekuwa nyumbani)
baada ya kupokea idhini ya kadhi. Wale watu wawili walikuwa wamelipwa kwa ajili
ya kusali na kufunga saumu zilizo za qadhaa za bwana wake aliyesadikiwa amekufa
safarini.
Na kurejea kwake kutoka safari ndefu
aliyosadikiwa amekufa, imebatilisha ndoa ya mke wake na yule bwana kwani yu hai
bado, vile vile saumu na sala pia zinabatilika kwani kumsalia mtu aliye hai pia
ni batili."
Kwa hayo, Harun na wanabaraza wake wote
walivutiwa na majibu ya Bahlul na walimsifu sana.
Baada ya hapo, ilikuwa ni zamu ya Bahlul
kuuliza swali: "Je niulize?" " Uliza tu!" alijibiwa.
Bahlul aliuliza: "Iwapo ninayo kasiki
moja ya siki na nyingine ya urojo wa sukari, na kwa ajili ya kutengeneza
Sikanjabin (kinywaji cha Siki) nimeweka ili kuchanganya katika kasiki ya tatu
na hapo tunakuja kumkuta panya amefia humo. Je unaweza kutuambia kuwa huyo
panya alitokea kasiki ya Siki au Urojo wa Sukari?
Hapo huyo sheikh wa kiwahhabi alijaribu
kwa uwezo wake wote kumjibu Bahlul, lakini alishindwa. Kwa kuona hali hiyo,
Harun alimwambia Bahlul "sasa wewe mwenyewe tujibu hayo."
Bahlul alimwambia Harun: "Nitafanya
hivyo iwapo huyu mtu atakiri kutoelewa majibu yake." Kwa masikitiko na
aibu kubwa huyo Faqihi alikubali kushindwa kwake kuling'amua hilo
fumbo.
Alianza Bahlul kulijibu: "itabidi
sisi kumtoa huyo panya na kumwosha vizuri kwa maji safi halafu tupasue tumbo
lake na humo iwapo tutakuta siki au urojo wa sukari, basi itatubidi tumwage
kile kitakachothibitika kuwamo tumboni mwake."
Wote waliokuwa wamehudhuria,
walifurahishwa mno na majibu ya Bahlul na Faqihi alilazimika kutoa Dinar elfu
moja za dhahabu ambazo Bahlul alizigawa miongoni mwa mafuqara wa Baghdad.
Comments
Post a Comment