DINI SAHIHI INARUHUSU KUJADILIWA

DINI SAHIHI INARUHUSU KUJADILIWA
Neno dini lina maana nyingi. Linaweza likatafsiriwa kuwa sheria, utaratibu au kanuni zilizoletwa na Mwenyezi Mungu ili kuwaongoza wanadamu. Lakini kwa bahati mbaya kanuni hizi zimezuka nyingi kwa kiasi cha kuwachanganya wanadamu kujua dini sahihi ni ipi.

Kwa kuwa, maana halisi ya dini ni kuwa dini inatokana na Mwenyezi Mungu, na ninaamini kuwa na wewe unaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuumba sote, haiwezekani Mungu mmoja ashushe dini mia. Kwa vyovyote vile dini sahihi ni moja kama ambavyo Mungu ni mmoja. Sasa dini nyingi zimetokea wapi? Bila shaka kuna uchakachuzi unaosababishwa na vibaraka wa shetani miongoni mwa wanadamu.

Kwa mfano, Nabii Mussa alitumia maisha yake yote akiwahubiria watu wamwabudu Mungu mmoja tu, lakini alipokwenda kupokea amri kumi za Mungu, aliwakuta watu wake wamepindua uongozi aliouacha chini ya Harun, badala yake Samiriyu akachukua madaraka na kuwatengenezea sanamu ya shaba, wakaanza kuiabudu hiyo sanamu. Huu ni ushahidi kuwa Mitume wanapoondoka wafuasi wao hubadili maudhui ya dini zao na hii ndio sababu ya dini kuwa nyingi.
Kitu kama hiki kimetokea kwa wafuasi wa Yesu. Yeye alikuwa akiwaambia kuwa yeye ni mwana wa Adamu aliyeona kweli toka kwa Mungu, kwa hiyo ameletwa na Mungu kuwaongoza waache maovu na watende mema. Lakini alipoondoka wakabadili na kuanza kusema kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, tena hawakuishia hapo, wakaamua kumwongeza cheo na kumwita Mungu mkuu. Huu ni uchakachuzi uliobobea.

Kwa msingi huu tutajuaje dini sahihi? Kwa kweli kama tuna nia safi, ni lazima tuzichunguze dini zetu kwa undani na tuhoji kila kipengele cha dini zetu, ili kujiridhishe mantiki ndani yake. Mungu wetu ni mwenye hekima, mwenye ujuzi. Mafunzo yake yamejaa hekima na ujuzi. Hakuna sababu viongozi wa dini watukataze kuhoji. Ukiona viongozi wako wanakataa kuhoji kuhusu imani mnayoifuata, elewa kuwa imani hiyo ni ya magumashi na kwamba hawana majibu kwa sababu sio imani sahihi.

Uislamu uko huru mtu ahoji chochote atakacho. Na unapomhitaji mtu kuamini kanuni Fulani, humshauri kuimakinisha imani yake katika hali ya kuwa na ushahidi. Na humweka huru kuuliza swali lolote na haimlaumu iwapo ataona mashaka, na mashaka hayo yatatoka tu baada ya juhudi kubwa za kuutafuta ukweli.
Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an kuwa wala usifuate usiyo na elimu nayo, hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa (17.36).
Kisha anasema, “Na kama ukiwatii wengi katika (watu) waliomo Ulimwenguni watakupoteza kutoka kwenye njia ya Mwenyezi Mungu. Hawafuati ila dhana tu ...”(6:116).

Anasema tena, “Na tumemuusia mwanadamu kwa ajili ya wazazi ...., unishukuru mimi na wazazi wako, marudio (ya mwisho) ni kwangu. Na kama watakulazimisha kunishirikisha na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema katika dunia hii...”(31:14-15).

Comments