FAIDA ZA KUFUNGA SWAUMU KWA KIWILIWILI

kiwiliwili cha binadamu ni kama mashine ambayo huhitajia mapumziko kidogo. Na mapumziko hayo hayawezi kupatikana hadi mtu ajizuie kula na kunywa kwa muda ambao ala ya kuyeyusha chakula (tumbo) itulie. Vile vile upatie moyo na vifaa vyote vya ndani mapumziko na kujisafisha vyenyewe. Basi kwa kufunga saumu hupungua, na pengine hutoka kabisa maradhi.
Elimu ya afya siku hizi imethibitisha kwamba mtu kuweka siha yake vizuri, inampasa kwa uchache afunge saumu, siku moja katika kila wiki, au wiki moja kila mwezi na bora mwezi mmoja kila mwaka.
Vile vile imethibitisha elimu za sasa kwamba bidii za akili na nguvu ya mwili huzidi kwa kuuweka mwili katika hali ya njaa. Bila shaka faida na maendeleo yanaweza kupatikana kwa kufunga saumu, kuliko mtu anapokuwa amejaa tumbo na uvivu pia umemshika. Madaktari na matabibu katika maradhi mara nyingi huwaongoza wagonjwa wao kufunga. Yapo baadhi ya maradhi kama mtu akifunga saumu tu badala ya kutumia dawa atapona kabisa.
Baada ya kujua na kufahamu hayo yote, basi tutapata hakika kuwa Mwenyezi Mungu kwa njia na taratibu bora kabisa ametuamrisha kuacha kula; na kitendo hicho kakifanya kuwa ni Ibada. Hii ni uthibitisho dhahiri wa huruma juu ya viumbe wake, isitoshe kakifanya hicho kitendo (kufunga) si faida ya duniani tu, bali kwa akhera pia. Juu ya hayo yote ikiwa tutahalifu, tutakuwa watu wajinga mno, tusio na mfano kwa kuzisahau hisani zake.

Si vibaya hapa tukisema kwamba baada ya kujua faida ya saumu kwa kiwiliwili, basi mtu haifai kwake ukifika usiku ale chakula kwa wingi kulipia njaa ya mchana, au kula vitu ambavyo ni vizito kwa tumbo na vyaweza kumletea taabu na maradhi. Kwa hiyo ni bora sana kutumia chakula chepesi anapofuturu ili apate faida kwa kiwiliwili na roho                            

Comments