Qur'ani imemhimiza kila mwanadamu ikamtaka azame ndani ya historia ya
mwanadamu na azingatie yaliyomo ili awaidhike na kuongoka, hivyo Mwenyezi Mungu
akasema: "Je, hawatembei katika ardhi ili wapate nyoyo za kufahamia au
masikio ya kusikilizia?"1
Baada ya Mwenyezi Mungu kutoa historia ya Adi, Thamudi, Firauni, watu wa
miji iliyopinduliwa na watu wa Nuh akasema: "Ili tuifanye ukumbusho kwenu
na sikio lisikialo lisikie."2. Historia ya ujumbe mbalimbali wa
Mwenyezi Mungu imejaa masomo na mazingatio, masomo ambayo yameonyesha jinsi
manabii watukufu walivyojali mataifa yao ili kuyaokoa toka kwenye matatizo
mbalimbali.
Pia ujumbe huo umeonyesha lengo na mwelekeo wake wenye kujaa nuru na
manufaa. Kwa ajili hiyo sira ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kizazi chake huwa
ni tafsiri ya kivitendo ya misingi na sheria za kiislamu.
Hivyo kusoma sera yao na historia ya maisha yao ni chanzo muhimu cha
kuifahamu Qur'an na Sunna, na ni chemchemu ya maarifa ya wanadamu wote, kwa
sababu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu alioutuma kwa wanadamu huku Nabii wa mwisho
na mawasii wake wateule wakiwa ni viongozi wa wanadamu wote bila kubagua.
Kwa misingi hii nitaendelea kuleta mada hatua kwa hatua kuhusu sira ya
viongozi hawa watukufu ili tuitumie kama mwongozo wa kuitafsiria Qur’an na
hivyo kupata mwongozo kamilifu katika maisha yetu ya kiuchamungu.
Comments
Post a Comment