HOTUBA YA MTUME (S.A.W.W) KUHUSU RAMADHANI

Amenakili Sheikh As-Sadduq r.a. kutoka kwa Al Imam 'Ali ar-Ridha (a.s.) kutokea kwa Al Imam Musa al-Kadhim a.s. kutokea kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kutokea kwa Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kutokea Al Imam Zaynul 'Aabediin a.s. kutokea kwa Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kutokea Imam Amir Al-Muuminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kutokea kwa Mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w.):
Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Kwa hakika Mwezi wa Allah (sw) umewafikieni pamoja na baraka, rehema na misamaha yake, kwani ni mwezi ulio bora kwa Allah (sw), usiku na mchana wake ni bora kuliko usiku na mchana wowote mwingine, saa zake ndizo bora kabisa kuliko saa zote na ni mwezi ambamo Allah (sw) anakualikeni na kuwafanyeni katika watu waliokirimiwa, pumzi zenu katika Mwezi huu ni Tasbihi, na usingizi wenu humo ni ‘
ibada, na ‘amali zenu humo zinakubaliwa na Dua’a zenu humo zinajibiwa na hivyo mumwombe Allah (sw) kwa nia safi na iliyo kweli na moyo msafi ili awajaalieni tawfiqi ya kufunga saumu na usomaji wa Qur’ani Tukufu katika mwezi huu mtukufu. Kwa hakika yeyote atakayekosa msamehe wa Allah (sw) katika mwezi huu ulio Adhimu basi atakuwa ni mtu asiyebahatika.

Mkumbukeni njaa na kiu cha Siku ya Qiyamah mkiwa katika hali ya njaa na kiu katika mwezi huu mtukufu, na vile vile, mutoe sadaqa zenu kwa ajili ya mafukara na masikini miongoni mwenu, muwaheshimu walio wakubwa wenu, na kuwahurumia walio wadogo miongoni mwenu na muwajaze kwa huruma zenu.
Mzihifadhi ndimi zenu na muyaweke macho yenu chini kwa yale yote yasiyoruhusiwa kutazamwa na wala msiyasikie yale yote yasiyoruhusiwa kusikilizwa, muwawie vyema mayatima ili wanapokuwa watoto wenu mayatima, nao pia watendewe mema na mumwombe Allah (sw) msamaha wa madhambi yenu, na mnyoosheeni Allah (sw) mikono yenu kwake kwa ajili ya Dua’a katika nyakati za Sala kwani ndiyo iliyo saa bora kabisa
ambamo Allah (sw) huwatazama wanaomwabudu kwa Rehema na hujibu anapoombwa na huitikia anapoitwa.

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Kwa hakika nafsi zenu zinategemea amali zenu na muzikomboe kwa istighfar zenu, migongo yenu imelemewa kwa uzito wa madhambi yenu na hivyo mpunguze uzito wenu kwa kurefusha sijida zenu na mjue kuwa Allah (sw) ametamka kwa kula kiapo cha Ukuu Wake kwa kutowaadhibu wanaosali na wanaosujudu na kutowatishia moto Siku ya Qiyamah, ambamo watu watakuwa wamesimama mbele ya Mola wao.

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Miongoni mwenu atakayemfuturisha aliyefunga saumu katika funga za Mwezi
huu Mtukufu basi ni sawa na kupata thawabu za kumpatia uhuru mtumwa mmoja na kupatiwa msamaha wa madhambi yaliyopita.”

Masahaba walisema: “Ewe Mtume Mtukufu (s.a.w.w.)! Si wote tulio na uwezo huo.” Mtume Muhammad Mustafa
(s.a.w.w.) alijibu: “Jiepusheni na moto wa Jahannam hata kwa kulisha kipande cha tende au hata kwa kunywisha maji. Kwa hakika Allah (sw) hupendezewa na hulipa mema kwa atendaye hivyo hata kama hatakuwa na zaidi. ”

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Yeyote atakayezirekebisha tabia zake basi Allah (sw) atamfanyia wepesi upitishio wake siku ya Qiyamah juu ya Siraat ambapo miguu ya wengineo ikitetemeka, na yeyote yule atakayewafanyisha kazi kidogo wamfanyakazi wake siku hizi za funga, basi Allah (sw) pia atamfanyia wepesi
hesabu yake Siku ya Qiyamah, na yeyote yule atakayeziepusha shari zake kwa watu, basi Allah (sw) atamwepusha na ghadhabu Zake, na yeyote atakayewakirimu mayatima basi Allah (sw) atamkirimu Siku ya Qiyamah na yeyote atakayewatendea mema ndugu na jamaa zake basi Allah (sw) atamjaalia Rehema Zake Siku ya Qiyamah.

Na yeyote atakayevunja uhusiano wake pamoja na jamaa na ndugu zake, basi Allah (sw) pia atauvunja uhusiano wake pamoja mtu huyo. Na atakayesali Sala za Sunnah katika mwezi huu Mtukufu, basi Allah (sw) atamwepusha na adhabu za Kaburi. 

Comments