IMAM ALLY NA SABABU ZA KUSHUHUDIWA KWENYE ADHANA KUWA NI WALII WA ALLAH.

Kwa hakika Amirul-Muumina Ally (a.s) ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu ambao
Allah amewachagua na kuwatukuza ili waendeleze jukumu zito la ujumbe baada ya Mitume, na watu wa namna hii ni mawasii wa mitume kwani kila nabii anawasii wake na Imam Ali ibn Abutwalib ni wasii wa Mohammad. Mashia tunamboresha Imam Ally juu ya Masahaba wengine kwa sababu Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamemboresha.
Kuna ushahidi wa kiakili, Qur'an na Sunnah. Lakini utawala wa Banu Umayyah ulihakikisha unafuta kila aina ya dalili juu ya Imam Ally kuwa walii wa Mwenyezi Mungu na kumpiga vita Ally na wanawe na kuwaua, na mambo yakafikia kumtukana na kumlaani juu ya mimbari, na kuwalazimisha watu wamlaani amirul-muunini, ndipo Mashia wake na wafuasi wake wanashuhudia kwamba Ally ni walii wa Mwenyezi Mungu na haifai kwa waislamu kumtukana walii wa Mwenyezi Mungu, na Shia walifanya hivyo ili kuonesha upinzani wao kwa tawala dhalimu zilizochukua madaraka muda mfupi baada ya Mtume kufariki.
Kumtangaza huku Imam Ally ni kwa ajili ya kuwafundisha watu wa vizazi vyote ili waelewe Historia iliyopotoshwa na watawala waovu. Shia tumeliweka hili katika adhana kwa minajili hii tu na wala si sehemu ya adhana. Na mtu yeyote akiweka uwalii wa Imam Ally katika adhana na huku akiamini kuwa ni sehemu ya adhana au iqama basi adhana na iqama zake zitabatilika.

Comments