Kilugha; neno “Swaum”
lina maana ya kujizuilia kufanya jambo lolote la kawaida. Katika Qur-an
tunafahamishwa kuwa Bibi Maryam baada ya kumzaa nabii Isa (a.s) alijizuilia
(alikuwa katika Swaum ya kutosema na mtu yoyote juu ya mtoto wake).
“... Na kama ukimuona mtu yeyote
(akauliza habari za mtoto huyu) sema: `Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi
wa Rehema ya Swaum (kufunga), kwa hiyo leo sitasema na mtu’” (19:26).
Katika Sharia ya Kiislamu kufunga
(Swaum) ni kujizuilia kula, kunywa, kujamiiana, kuingiza kitu chochote katika
matundu ya mwili na kujizuilia kumuasi Allah (s.w) kuanzia alfajiri ya kweli
mpaka usiku.
Lengo la Swaum katika Uislamu ni
kumuwezesha mja awe mcha Mungu kwa kufuata maamrisho yote ya Allah (s.w) na
kuacha makatazo yake yote. Hivyo, ili lengo hili litimie mfungaji pamoja na
kujizuilia kula, kunywa, kujamiiana, hana budi pia kujizuilia na kitendo
chochote kitakachompelekea kuvunja amri ya Allah (s.w) na Mtume wake (s.a.w.w).
Kwa maana nyingine, ili Swaum ya mfungaji iwe na maana na yenye kufikia lengo,
mfungaji hana budi kukizuilia (kukifungisha) kila kiungo chake cha mwili -
macho, ulimi, masikio, mikono na miguu pamoja na fikra na hisia zake -na
matendo aliyoyakataza Allah (s.w.). Funga ya macho ni kujizuilia kutazama yale
yote aliyoyakataza Allah (s.w), funga ya ulimi ni kujizuilia na mazungumzo yote
aliyoyakataza Allah (s.w), kama vile kusengenya, kusema uwongo, kugombana n.k.,
funga ya masikio ni kujizuilia kusikiliza yale yote aliyoyaharamisha Allah
(s.w); funga ya miguu ni kujizuilia kuendea yale yote aliyotukataza Allah
(s.w); funga ya fikra na hisia, ni kujizuilia na fikra na dhana mbaya ambazo
zinampelekea mja kuvunja amri na makatazo ya Allah (s.w). Ni katika maana hii
Mtume (s.a.w) anasema katika Hadith zifuatazo:
“Mtume wa Allah amesema: Yule
ambaye haachi kusema uwongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allah hana haja na
kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake - (Allah (s.w) hana haja na
funga yake).
kisha Mtume wa Allah akasema; Ni wangapi wamefunga
lakini hawana funga ila kukaa na kiu tu, ni wangapi wanaoswali usiku ambao
hawana swala ila huambulia kupoteza usingizi tu.
Hadith hizi zinatuthibitishia kuwa
ufungaji usioambatana na kujizuilia na maovu na machafu, haumpatii mfungaji
faida yoyote.
Comments
Post a Comment