MTUME (S.A.W.W) KABLA TU YA TANGAZO LA UJUMBE WAKE

Licha ya ukweli kwamba Arabia ilikuwa ni shimo la uovu na ngome ya ibada ya masamu na ushirikina, Muhammad mwenyewe hakuwa kamwe amechafuliwa na inda au dhambi yoyote, na kamwe hakuinama mbele ya sanamu lolote. Hata kabla hajatangaza kwamba amekuja kusimamisha ufalme wa Mbinguni hapa duniani, tabia yake na mwenendo wake mwenyewe vilikuwa ni kiakisi (picha) cha Qur'an Tukufu. Hata wakosoaji wake hawakuweza kuonyesha tofauti kati ya tabia yake na maagizo ya Qur'an wakati wowote, kabla na baada ya Tangazo.
Baada ya Tangazo la ujumbe wake kama Mtume wa Mungu, aliziweka mila na desturi za kipagani chini ya amri ya kupigwa marufuku, lakini hakuna ushahidi kwamba kabla ya kufanya hivyo, yeye mwenyewe aliwahi kutenda jambo la kipagani, au hasa tendo lolote lenye kukinzana na Qur'an.
Inaonekana kwamba, Qur'an, kitabu cha Mungu kilikuwa kimegandamizwa kwenye moyo wa Muhammad tokea mwanzo, na pia inaonyesha kwamba "alihubiri" Uislamu hata kabla ya kubaathiwa, bali tu kupitia matendo yake na sio kwa maneno. Matendo yake yalikuwa fasaha sawa kama ilivyokuwa hotuba zake, na yaliutangazia ulimwengu ni vipi alivyokuwa mtu wa adabu. Hata hivyo walikuwa ni wale mapagani waliomwita Amin (mwaminifu) na Sadiq (mkweli), na walikuwa ni watu haohao ambao, katika miaka ya baadae, walimsumbua, wakamuwinda, wakamfukuza, na kuweka na kutangaza malipo juu ya kupatikana kichwa chake.
Pamoja na kupotoka na ukorofi, kama mapagani wa Kiarabu walivyokuwa, bado walivutiwa na ukweli; hata ukiwa kwa adui. Bado kupendezewa kwao na ukweli wa Muhammad (s.a..w.w) hakukuwazuia kutafuta kumuangamiza aliposhutumu ibada yao ya masanamu na ushirikina wao. Walishikwa na kiu juu ya damu yake tangu pale alipowaita kwenye Uislamu lakini hawakujiuliza kuhusu kuwa kwake mkweli. Juu ya hoja hii hapawezi kuwepo na ushahidi wa kuaminika kabisa hasa zaidi ya wao.

Waislamu tunatakiwa tuwe na tabia njema kama alivyokuwa Mtume wetu kiasi kwamba adui ashindwe kupata kisingizio cha kutushambulia na kama akitushambulia kwa ujeuri dunia nzima itashuhudia kuwa waislamu wanaonewa. Haikubaliki kwa muislamu kuwa mbabe na mwonezi ambayo kazi zake ni kuwapiga na kuwadhalilisha wanadamu wengine.

Comments