MUDA SAHIHI KWA KUFUTURU

MUDA SAHIHI KWA KUFUTURU
Allah (s.w) anasema katika Qur’an tukufu, “... na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe katika uzi mweusi wa alfajiri, kisha timizeni swaumu mpaka usiku. ... (2.187).
Kwa aya aya hii inabainika muda wa mwisho wa kula daku na muda wa kufuturu. Kwa maana kwamba mwisho wa kula daku ni muda mfupi kabla ya swalatil Sub-hi na mwanzo wa kufuturu ni usiku unapoingia. Tukiambiwa usiku, sio msamiati usioeleweka, ninaamini kuwa kila mtu anajua hivi sasa ni usiku au la.
Lakini kwa bahati mbaya baadhi ya ndugu zetu katika imani wamekuwa wakifuturu mchana kweupe badala ya usiku. Wao huhimizana kuwa “cheleweni kula daku na harakisheni kufuturu” na kuyanasibisha maneno haya na kauli ya Mtume (s.a.w.w). Maneno haya hayawezi kukubaliwa kiurahisi bila kuyafanyia uchambuzi ili tujue utekelezaji wake ukoje.
Je, kama aya inatuagiza tufunge mpaka usiku, Mtume (s.a.w.w) anaweza kuagiza kinyume chake? La hasha Mtume hakuwahi kwenda kinyume cha Qur’an hata siku moja. Hivyo aidha hiyo hadith itakuwa ni ya uongo au watumiaji wa hadith hiyo wameipotosha maana.
Hivi kama hadith inasema wahini kufuturu, imetuwekea muda? Hapana, hadith hiyo haina muda wa kufuturu. Kwa maana hii bila shaka imepotoshwa maana na masheikh kwa maslahi yao binafsi. Kuwahi kufuturu ina maanisha kuwa pindi usiku unapoingia tuwahi kufuturu na sio kuwafuturisha watu bado mchana peupe kwa madai ya kuwahi kufuturu.

Utasikitishwa na baadhi ya misikiti ambapo huwahi kuadhini, bado peupe kiasi kwamba ukiwaambia watu muda huu ni usiku watapinga na wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kukubali huwa muda huu ni usiku. Wakati huo baadhi ya watu hugawa tende na kuwahimiza watu wazile haraka haraka kabla ya hata ya swala ili wao wapate thawabu za kuwafuturisha. Lakini kwa bahati mbaya watu hawa watapata dhambi ya kuwafunguza swaumu watu waliowapa tende badala la kupata thawabu kwa sababu muda wa kufuturu unakuwa bado. 

Comments