NJIA ZA KUTUMIA ZAKA
Kurani Tukufu imetaja njia
nane za kutumia Zaka:
(1) Kuwapa mafukara, watu
ambao umaskini wao umeonekana waziwazi:
(2) Maskini, ambao wameishiwa
mali au njia za kuchumia mali lakini wanajaribu kuuficha umaskini wao
wasiudhihirishe kwa wengine kwa sababu ya ari ya moyo wao;
(3) Wafanyao kazi ya kukusanya
Zaka,
(4) Waungiwao mioyo yao, yaani
watu ambao nyoyo zao zimeelekea kwenye dini, lakini kwa kuwa wametengana na
jamaa zao, wanakuwa na haja ya msaada. Hiyo siyo maana yake kwamba watu wapewe
fedha na kuvutwa kuingia dini ya Islamu, bali watu wapya katika dini ambao
pengine wanaachishwa kazi au wanataabishwa kwa njia nyinginezo kwa sababu ya
wao kuacha dini yao ya zamani na kukubali dini ya Islamu wamewekewa sehemu
katika mali ya Waislamu.
(5) Kuwakomboa wafungwa na
watumwa. Wale watu ambao wanafungwa kwa kutoweza kulipa deni pia wanaweza
kusaidiwa na pesa hizo. Hata wafungwa na watumwa wasiokuwa Waislamu wanaweza
kukombolewa na kuachwa huru kwa fedha ya Zaka
(6) Wasio na uwezo wa kulipa madeni
yao au walipata hasara; nzito katika biashara zao au waliotakiwa kulipa dia (fidia
kwa mtu aliyefariki) ya jamaa zao;
(7) Katika njia ya Mwenyezi
Mungu: katika fungu hili yanaingia matumizi yote yanayofanywa kwa ajili ya dini
ya Mwenyezi Mungu au kwa ajili ya watu wote kwa jumla; kama kueneza na
kupigisha chapa vitabu na magazeti ya dini, kufungua shule za elimu za dini na
za kidunia, kuendesha hospitali na viwanda vya sanaa na mambo mengine yote
yenye kustawisha Waislamu na dini yao; (8) Wasafiri wanaopata taabu katika
safari kwa kupungukiwa pesa au wanaosafiri kutafuta elimu. Msafiri ye yote awe
tajiri au maskini anaingia katika fungu hili. Nyumba za wageni zaweza kujengwa
kwa fedha ya Zaka. Wasio Waislamu pia wanaweza kualikwa waje watembelee nchi za
Waislamu na kuonana nao wakalipwa kwa fedha ile.
Matumizi ya Zaka yana wasaa
mwingi na watu wote wanapata faida. Siku za Khalifa wa Kiislamu, yaani Imam
Ally (a.s) Mayahudi na maskini wengine wa dini zingine walikuwa wakipata msaada
mwezi hata mwezi katika beit-il-mal ya Waislamu. Watu walioshindwa kujipatia
riziki kwa sababu ya uzee au ugonjwa au kwa kukosa njia za kuchumia mali
walisaidiwa na Maimamu wa Mtume s.a.w. kwa njia ya Zaka na Khumsi.
Lakini watawala waliovamia
utawala baada tu ya Mtume kufariki, waliwanyima familia ya Mtume (s.a.w.w) haki
yao ya khumsi ambayo walikuwa wamepewa na Allah (s.w). Waliwanyima Mali hizo
ili kuwadhoofisha na kiuchumi, waweze kuzitii tawala zao za kidhalimu.
Comments
Post a Comment