SAUMU (KUFUNGA)

Saumu (kufunga) ni kitu gani na vipi inatubidi kufunga?
Maana ya saumu inavyoelezwa katika kitabu cha lugha (Kamusi) ni kujizuia kufanya jambo fulani. Na maana yake kwa kisharia ni hii:- Mtu kujizuia kutwa na mambo yafuatayo yanayovunja saumu; kuanzia alfajiri ya pili iitwayo Subh-Saadiq hadi magharibi ya kisharia .[1]
Ukikaribia kuja mwezi mtukufu wa Ramadhani, utawaona watu wengi wameshughulika kuandalia huo mwezi mtukufu kwa furaha, vile vile (utawagundua) utawaona baadhi ya watu wanatafuta masingizio ya kutokufunga. Laiti wangefikiria faida ya kufunga na makusudio yake, ijapokuwa udhuru wenyewe wenye maana, na akajaribu kufunga. Ikiwa anafahamu fadhila na faida ya roho ambayo hupatikana kwa kufunga tu bila shaka hatoacha saumu hata siku moja.
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wenye baraka nyingi, na bwana wa miezi yote, na huitwa mwezi wa Mwenyezi Mungu. Katika mwezi huu Mwenyezi Mungu anawafungulia viumbe wake milango ya rehema, na rehema hizo kuwafikia na huwazingia viumbe wake. Basi ndugu zangu tufanye bidii kama tuwezavyo tuziteke hizo baraka na rehema za mwezi huu. Neema bora na kubwa ya mwezi huu ni hiyo kufunga saumu.
Hakika mwezi wa Ramadhani huwazindua na kuwaamsha katika usingizi waovu na wahalifu na kuwanabahisha kuyafahamu na kuyafuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu (mwenye hekima) ili kuepukana na yaliyo katazwa na dini ya Kiislam, wapate kujitenga nafsi zao kwa kutenda maovu, na kukimbilia kwa Mola wao, kwa kusali, kusoma dua, kulisha na kufanya utiifu mwingi.
Walevi wengi huwacha kulewa mwezi wa Ramadhani na wafasiki na waovu wengi hawatubii ila katika mwezi wa Ramadhani na Wasio amini wengi hawaoni huruma nyoyoni, lakini ukiingia mwezi huu mtukufu huruma inawajia na hulainisha nyoyo, na wenye mali (tajiri) wengi wasiowaonea huruma masikini ila ukiingia mwezi mtukufu ndipo huonyesha huruma.
Unapoingia mwezi wa Ramadhani tu basi huingia baraka, heri, na utiifu. Usiku na mchana wake hunawirika na kung'aa kwa ibada na utiifu wa watu. Misikiti na mahala pa ibada hujaa wachamungu wanaosujudu na kurukuu na huku wakiomba wasamehewe. Wengine hushughulika kuisoma Qur'ani usiku na mchana, na kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mwenye huruma kwa nyoyo ya unyonge iliyo sali, huku macho yakilia na wakimwomba kwa sauti ya huzuni.
Huu ndio mwezi mtukufu wenye uzuri na jamala na kuwa bora kuliko miezi yote. Katika mwezi huu wanatubia wenye kutaka kutubia, na wanaomba kughufuriwa wenye kutaka kughufuriwa, na huo ndio msimu wa wenyekufanya ibada. Basi ewe mwenye kufanya ibada hima kimbilia kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu. Usije mwezi mtukufu huu ukapita, ila nawe uwe na tamaa ya kuwa umekwisha samehewa.
Ewe tajiri, masikini, mwenye miliki, mkulima, na waungwana wakubwa na wadogo, msiwadhulumu walio chini yenu na msishindane na wakubwa wenu.
Ewe, mwislamu mahala popote ulipo, kimbilia kufanya mema ya kumridhisha Mola na Mtume (s.a.w.w), na pia waridhishe Maimamu "Masumin" (A.S.) kwani mwezi huu ni mwezi ule ambao Mwenyezi Mungu huyafuta madhambi na huongeza juu ya hayo thawabu kwa viumbe, na huinua daraja zao; basi tukimbilie kumridhisha Mola, tukimbilie kufanya ibada, na tukimbilie kutubia kwa Mwenyezi Mungu.
[1] Subh-Saadiq ni weupe wa mchana unaonekana kwenye mstari wa upeo wa macho upande wa mashariki wenye kutanuka 'kwa upana, na kuzidi kua mweupe mpaka linapotoka jua, na ndio wakati ambapo huwa haramu kula na kila kinachovunja Saumu kwa mwenye kutaka kufunga.
Magharibi: Kwa kawaida magharibi ni wakati jua linapozama na kufichika upeo wa macho, na kwa sharia ni wakati ule wekundu unaonekana upande wa mashariki baada ya kuzama juu ufike sawa na utosi mbinguni

Comments