TAWBA (UTANGULIZI)

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, mwenye kurehemu.
Sifa zote ni za Allah swt Mola wa dunia zote na salaam zimfikie Mtume wake Muhammad (s.a.w.w.) pamoja na ahali wake wataharifu (a.s.) na Sahaba Muttaqiina.
Vijana wetu katika zama hizi wapo wanasikitikia na kujutia juu ya yale waliyoyatenda, lakini kwa kuwa hawana mategemeo, basi wapo wanaendelea na matendo yao maovu.Wanafikiri kuwa sasa wameshatenda madhambi na hawajui kama watasamehewa au la, na hivyo utawaona wakiupoteza ujana wao katika maasi mbele ya Allah swt.
Imenilazimu kuanza kuandika makala za tawba ili kuziathiri roho za watu au nafsi zao, waweze kuacha maovu na kuwa watu wema na watamkuta Allah ni msamehevu tena mrehemevu.
Iwapo mwanadamu amekwisha tenda madhambi katika maisha yake huku duniani, basi asikate tamaa bali inambidi ajitokeze mbele ya Allah swt kwa taadhima na heshima kwa kuomba TAWBA na MSAMAHA, na kwa hakika Allah swt lazima atatusamehe. Allah swt yupo kila wakati akisema: 'Ewe Mja wangu! na kamwe hujatuita; Ewe mwovu, muasi au jina lingine lolote lililo ovu, Ilhali unazijua aibu zetu, lakini kazificha. Sisi tunapojua aibu za mtu miongoni mwetu, basi huwa tunamwona kwa mtazamo wa dharau, lakini Allah swt amezificha aibu zote.
Mtu anapokuwa akilaumiwa na dhamira yake, akili yake na nafsi yake kumfanya au kumshurutisha afanyeTAWBA, basi asiwe na wasiwasi, ila ajielekeze katika kufanya TAWBA YA ALLAH swt na hivyo atoe ahadi yake thabiti ya kutotenda madhambi tena. Hapo ndipo Allah swt anaposema kuwa kilio cha mwenye madhambi ni afadhali kuliko tasbihi za Malaika.
Kwa mujibu wa Ahadith na riwaya mbalimbali, madhambi ya mfanya TAWBA hudondoka kama vile yanavyodondoka majani katika mti au mfano wa mtoto mchanga anapozaliwa huwa hana madhambi. Hivyo inambidi mtu asiendelee kufanya madhambi baada ya kufanya TAWBA wala tusisite kuomba TAWBA kwa ajili ya madhambi tuliyokwisha tenda hapo kabla.
Ni matumaini yangu kuwa kazi hii ndogo itatusaidia sote na tuombe kwa Allah swt aikubalie na kutujaalia tawfiqi ya kutenda matendo mema na tukifariki tuwe miongoni mwa wale waliokwisha fanya TAWBA

Comments