Allah swt katika sura Tahrim Aya ya 8
anatuambia:
"Enyi mlioamini! tubuni kwa Mwenyezi Mungu TAWBA iliyo
ya kweli.........."( 66:8 )
Kwa watu wenye kuona na kufikiri, haikufichika kwao
kuwa TAWBA ni fungu mojawapo la ukarimu na rehema za Allah (swt) na kwamba
TAWBA ni mlango mmojawapo mzuri kabisa ambao Allah swt ametufungulia ukawa wazi
daima kwa ajili ya sisi waja wake. Iwapo mlango huu wa TAWBA ungalikuwa
umefungwa, basi hakuna mtu ambaye angeweza kuokoka na kufanikiwa mbele ya Allah
(swt), kwani maisha na matendo yake mwanadamu yamejaa makosa, madhambi na
maasi.
Kwa kifupi ni kwamba mwanadamu anaweza kujizuia
asitende madhambi, lakini hakuna mtu anayeweza kudai kuwa yeye hakutenda
madhambi tangu alipopata akili, isipokuwa Mitume (a.s.) na ma-Imamu (a.s.)
ambao hatuna shaka na utoharifu wao.
Ni kwa sababu hiyo Allah ametuwekea dawa ya kutuponyeshea
magonjwa yetu na maradhi ya kiroho na ni njia ya kuyasafisha matendo yetu
maovu, ili kwa baraka za TAWBA, madhambi ya mwanadamu yaishe na aweze kujipatia
uokovu wa milele.
Amebahatika mtu ambaye ameweza kuuthamini huu mlango
wa rehema na kuweza kufaidika nao akawa mpenzi wa Allah (swt) na ameweza kuwa
mja mwenye kushukuru neema zake. Lakini hakubahatika yule ambaye hakuweza
kufaidika kwa mlango huo ambapo milango na njia zote za TAWBA zimekuwapo wazi
mbele yake!
Siku ya Kiyama wakati wa kutoa hisabu, mtu atakapokuwa
akijitafutia visingizio na sababu katika kujibu maswali atasema: Ewe Mwenyezi
Mungu! Mimi nilikuwa mjinga na wala sikuwa na habari, matamanio na ghadhabu
zangu zilinifunga kwa minyororo na wala sikuweza kamwe kumudu msimamo wangu
dhidi ya wasiwasi na upotofu wa Sheitani." Hapo atajibiwa pamoja na
masingizio na sababu zake "Je, sikukuwekea wazi njia zote za TAWBA?
Ulielezwa kazi zote zilizo ngumu, na je alitokea yeyote mwenye kuzidi uwezo
wako? Je, masharti ya TAWBA yalikuwa hayakushughulishi wewe?"
Mti atakaye ng’ang’ania madhambi na kugoma kutubu
hatokuwa na sababu ya Kumwambia Mwenyezi Mungu. Hivyo tuitumia nafasi hii
kutubu. Allah sasa ametuletea mwezi wa Ramadhani ambao ni wa rehema na mlango
mmoja wapo wa toba. Tuutumie vizuri mwezi huu kiasi kwamba utakapokwisha tuwe
tumekwisha samehewa.
Comments
Post a Comment