Kuna watu
wanasema kuwa masahaba wote wa Mtume (s.a.w.w) walikuwa ni wachamungu. Sielewi labda
ni kutokujua Historia yao au kutokufahamu maana ya sahaba.
Sahaba ni
Mtu yeyote aliyezaliwa au kusilimu wakati Mtume (s.a.w.w) akiwa hai awe
alimuona kwa macho au hakumuona kwa sababu ya upofu au umbali wa kutoka eneo
analoishi huyo na eneo alilokuwa akiishi Mtume (s.a.w.w) na hivyo kusababisha
wasionane kwa macho, lakini bado ni sahaba. Hii itakuwa na maana kuwa malaki ya
watu waliokuwa wakiishi Uarabuni kipindi hicho walikuwa Masahaba. Wale waliozaliwa
au kusilimu baada ya Mtume kufariki wanaitwa Tabiin, na kizazi kilichopatikana
baada ya tabiin huitwa tabitabiin. Sasa hakuna uwezekano wa kuwasema wote kuwa
wachamungu bila kuwatofautisha kulingana na matendo yao.
Jee wake
wa Mtume Muhammad (s.a.w.w); hawakuwa Waislamu? Hawakuwa ma mama wa waumini?
Mbona Mwenyezi Mungu amewawekea sharti ya ucha-Mungu (Sura 33:32) ndipo wapate
daraja yao, kwa kuwaambia: 'Enyi wake wa Mtume! Nyinyi si kama yeyote kati ya
wanawake, kama mtamcha Mwenyezi Mungu...' Hili ni kutuonyesha kwamba kama
hawatakuwa na mwendo mwema (hawatamcha Mola wao), basi ile kuwa ni wake wa
Mtume tu hakutawafaa kitu. Bali ikizidi, kama watafanya machafu yoyote, inatakikana
adhabu yao iwe maradafu kama inavyoelezwa kwenye Sura 33:30. Na hivyo ndivyo
inavyotakikana tuwe kwa masahaba.
Ili tupate
mafunzo toka kwa Masahaba tunatakiwa tuchunguze mienendo yao, tutakao ona kuwa
wana mienendo mizuri tuwafuate na tutakao ona kuwa wana mienendo mibaya
tuambizani kukwepa kuwafuata.
Maana kama
wao-waliokaa na Bwana Mtume (s.a.w.w.) na kupokea kwake maadili yote hawatatuwekea
ruwaza njema, nani mwingine atatufanyia hilo? Na jee, kama hatutawatuhumu kwa
yale maovu waliyoyatenda, watu wengine si watayachukulia kuwa ni mema kwa
sababu tu yamefanywa na sahaba wa Mtume (s.a.w.w.), hasa kwa hivi ambavyo,
Kisunni, mwendo wa baadhi ya sahaba [1] wa
Bwana Mtume (s.a.w.w.) huhesabiwa kuwa ni sunna?!
Kutokana
na aya mbili tatu tulizozitaja hapo juu, nataraji nimeweza kuthibitisha kwamba
ule mtazamo wa kuwa sahaba wote ni waadilifu, baada ya kuambiwa kwamba sahaba
ni yule aliyemwona Mtume (s.a.w.w) japo kwa mbali-na akafa ni Mwislamu, ni
mtazamo unaopingana na Qur'ani Tukufu na mafunzo ya Bwana Mtume (s.a.w.w.).
Nitaendelea
kutoa mada hii kuonesha kuwa imani ya kuwa Masahaba hawakosei na kwamba wote ni
wachamungu unavyopingana na ukweli wa maisha yao wenyewe Masahaba. Kwa mfano
masahaba walipingana vita na kuuana, hivi ni kweli kwamba aliyeua na aliyeuawa
wote walikuwa wachamungu? Haitoshi baadhi ya ndugu wa Mtume ndio waliokuwa
makafiri wakubwa na wakimpiga vita Mtume (s.a.ww.).
Marejeo:
[1] - Taz. uk. 74 wa
Juzuu ya Nne ya al-Muwafaqat ya Shatibi.
Comments
Post a Comment