Juu ya sadaka hii Mtume (s.a.w.) alisema kuwa “Zaka
inachukuliwa kwa matajiri wa Waislamu na hurudishiwa mafukara wao”.
Neno la "kurudishiwa" linastahili kufikiriwa
kidogo. Mtume (s.a.w.w) hakusema "hupewa" bali alisema
"hurudishiwa". Mradi wake ni kwamba watu wanaopewa sehemu katika Zaka
hawafanyiwi hisani na wenye kuitoa, bali kwa hakika
wanapokea haki yao.
Kurani Tukufu imesema. "Na Amekutiishieni
vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote vimetoka Kwake" (45:14).
Tena amesema, "Na ambao katika mali zao iko
sehemu maalumu kwa ajili ya aombaye na
anayezuilika kuomba" (70:25,26): Basi mtu
anayechuma mali, hiyo yote si yake peke yake;
bali iko ndani yake haki ya watu wengine. Kwa maana
ardhi na mvua na wanyama na madini na vyombo vingine vya kuchumia mali, kwa
hakika, viliumbwa kwa ajili ya wanadamu wote.
Basi tajiri anayechuma mali kwa kutumia vile vitu
vilivyoumbwa si kwa ajili yake tu awe na
hakika ya kuwa haki ya watu wengine haikosi kuwamo
katika mali yake. Na asipotoa haki ya watu hao mali yale hayatakuwa halali
kwake. Ndiyo sababu neno lililotumiwa kwa sadaka hiyo ni "zaka",
yaani kitu cha kutakasa mali. Kwa maneno mengine, mali aliyopata mtu haiwi
halali kwake mpaka awe ametoa sehemu maalumu kwa ajili ya watu wengine ambayo
ni haki yao.
Comments
Post a Comment