ADHANA: JE NI NDOTO AU WAHYI
Kila sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu
mlezi wa ulimwengu.
Rehma na Amani zimfikie mbora wa viumbe na
hitimisho la mitume wake, pia kizazi chake kitakatifu ambacho ndicho kasha la
elimu yake na hazina ya mafunzo yake. Hakika Uislamu
ni imani na sheria. Imani ni kuamini
Mwenyezi Mungu, mitume wake na siku ya mwisho.
Na sheria ni hukumu za Mwenyezi Mungu
ambazo zinajukumu la kumpa mwanadamu maisha bora na kumhakikishia wema wa dunia
na Akhera. Sheria ya Kiislamu ni ya kipekee kwa kuwa inahusika na kila jambo
huku ikiweka utatuzi wa matatizo yote yanayompata mwanadamu katika sekta zote
za maisha yake, hivyo Mwenyezi Mungu akasema: “Leo nimewakamilishieni dini yenu na kuwatimizieni
neema yangu na nimewapendeleeni Uislamu uwe dini yenu.. ( 5:3 ).
Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu
nyote wala msifarakiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu,
mlipokuwa maadui na akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema zake mkawa
ndugu.” (3:103).
Imam Ja’far Sadiq (a.s.) aliambiwa:
”Wanadai kuwa kuna mtu kati ya Answari aliona adhana usingizini.” Imam akajibu:
Wamesema uongo, hakika dini ya Mwenyezi Mungu ni takatifu zaidi ya
kuonekana usingizini.”
Muhammad Al-Hanafiya amesema: ”Mmelizushia
uongo jambo ambalo lina asili ndani ya sheria ya Uislamu na mafunzo ya dini
yenu, hivyo mkadai eti lilitokana na ndoto aliyoiona mtu kati ya Answari
usingizini mwake. Ndoto ambayo huenda ikawa ni uongo au kweli, na huenda ikawa
si chochote.”
Adhana Kilugha Na Kisheria
Na nafasi ya muadhuni mbele ya Allah
Adhana kilugha: Ni tangazo. Mwenyezi Mungu
amesema:
وَأَذَانٌ مِنَ اللَّهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ
الْحَجِّ الْلأَكْبَرِ
“Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu
na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa.”(9:3).
Maana yake ni tangazo kwa watu kutoka kwa
wao wawili.
Kisheria: Ni tangazo la kuingia wakati wa Sala ya
faradhi kwa kutumia maneno maalumu yaliyopokewa kwa sifa mahususi. Nayo ni kati
ya amali bora ambazo humkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu, na ni yenye fadhila
nyingi na ujira mkubwa.
Amepokea Sheikh Tusi katika (Tahdhib) kutoka kwa Muawiya bin
Wahabi, toka kwa Abu Abdillah (a.s.) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:
“Atakayeadhini muda wa mwaka mmoja ndani ya mji kati ya miji ya Waisilamu basi
atawajibika kupata pepo.”1
Pia amepokea toka kwa Saadil-askafu kuwa:
“Nimemsikia Aba Abdillah akisema: Atakayeadhini muda wa miaka saba kwa ajili ya
kupata radhi za Allah basi atakuja siku ya Kiyama akiwa hana dhambi yoyote.”2
Amepokea Swaduq toka kwa Al-Urzumiy toka
kwa Aba Abdillah kuwa: “Watakaokuwa na shingo ndefu sana siku ya Kiyama zaidi
ya watu wote niwaadhini.”3
Ameandika Ahmadi Muhammad Al-Barqiy katika
kitabu Al-Mahasini toka kwa Jafar Al-Jaafy toka kwa Muhammad
bin Ali Al-Baaqir kuwa: “Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Muadhini mwenye
kutaka radhi za Allah ni sawa na mpiganaji katika njia ya Allah, mwenye kupigana
kati ya makundi mawili.”4
Na nyingine nyingi riwaya kama hizi zenye
kuhimiza kutoa adhana huku zikiwataka watu wa tabaka zote kuitangaza, na
kukerwa na kitendo cha madhaifu kuificha adhana kwa udhaifu wao.
Tumeleta uchambuzi huu kwa ajili ya
kubainisha mambo mawili:
Kwanza: Hakika sheria ya adhana ni sheria
ya Mwenyezi Mungu haina uingiliano wowote na mwanadamu. Ndio maana zipo hadith
zinazoahidi pepo kwa watu wenye kutoa adhana kwa ikhlasi.
Pili: Kusoma historia ya tamko la
“Sala ni bora kuliko usingizi” (Tathwib)
katika Sala ya asubuhi. Huku tukithibitisha kuwa tamko hili si sehemu ya adhana
bali liliongezwa kwa kuungwa mkono na baadhi ya watu.
Tutaendelea kufafanua mada hii insha-Allah
katika mada zijazo.
REJEA
1. At-Tahdhibu: 2 /283 ?1126
2. At-Tahdhibu: 2 /283 ?1128
3. Thawabul-Amali: 52
4. Al-Mahasin: 48 Namba: 68
Comments
Post a Comment