HESHIMA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

 HESHIMA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI  
“..... Mwezi wa Ramadhani ni ambao imeteremshwa humo Qur’an kuwa mwongozo kwa watu...” (Qur’ani: 2:185) Waislamu kote ulimwenguni hufunga mwezi wa Ramadhani, mwezi ambao ni mwema kuliko miezi yote, ulio na masiku bora kuliko masiku yote, wenye masaa ya baraka kuliko masaa yote na amali zifanyikazo katika mwezi huo ni makbuli kuliko baki ya maombi. Nao ni mwezi wa Ramadhani.

Mwezi huu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa tisa wa miezi wa Kiislamu, ni mwezi wa pekee wa aina yake kwa utukufu. Ni mwezi wa kusameheana, kuombeana heri na hata kufanya ibada kwa wingi na kwa usahali kabisa. Mwezi huu una matukio mbali mbali ya kihistoria ambayo hayatasahaulika, na ambayo vile vile hupambanua wazi utukufu wake.
Imam Ja’far as-Sadiq alisema kutoka kwa Babuye, (Mtume s.a.w.) “Taurati ilishuka na kumfikia Nabii Musa (a.s.) tarehe 6 Ramadhani, nayo Injili iIiteremshiwa Nabii Isa (a.s.) tarehe 12 za Ramadhani, kadhalika Zaburi ya Nabii Daud (a.s.) iliteremshwa mnamo tarehe 18 za Ramadhani, vile vile Qur’ani Takatifu iliteremka katika usiku wa Lailatul Qadri ambao kwa kawaida huwa katika mwezi huu wa Ramadhani.” Bila shaka hiyo ni heshima kuu kabisa.

Na umejionea mwenyewe, hakuna kitabu kati ya vitabu vitukufu vinne kutoka kwa Mungu kilichoshuka ila kilishuka mwezi huu wa Ramadhani, na hayo yote ni kuonyesha utukufu wa mwezi huu. Kwa hivyo lazima vitendo vyetu katika mwezi huu viwe vitukufu kama mwezi wenyewe ulivyo.
SAUMU NI AMRI YA MUNGU Sisi kama Waislamu, hatufuati amri yeyote ile ila sharti iwe imenasiwa katika Qur’ani ama katika Hadithi tukufu za Mtume wetu (s.a.w.) Saumu katika Qur’ani imetajwa kutoka Aya ya 183 ya Sura ya pili ‘AL-BAQARAH’ hadi Aya ya 187 ya Sura hiyo hiyo.
Na Mwenyezi Mungu Ametufunza kama ifwatavyo: “Enyi mlioamini, mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu. “Siku chache tu (kufunga huko). Na atakayekuwa mgonjwa katika nyinyi au katika safari (akafungua baadhi ya siku), basi (atimize) hesabu katika siku nyingine. Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini.
Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake. Na (huku) kufunga ni bora kwenu. Ikiwa mnajua (haya sasa basi fuateni) “(Mwezi huo mlioambiwa mfunge) ni Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’ani kuwa mwongozo kwa watu na hoja zilizo wazi wa uwongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili). Atakayekuwa katika mji katika huu mwezi (wa Ramadhani) afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi (atimize) hisabu (ya siku alizowacha kufunga) katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na pia (anakutakieni) mtimize hesabu hiyo, na (anakutakieni) kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongezeni, ili mpate kushukuru. “Na waja wangu watakapokuuliza hakika yangu, (waambie kuwa) Mimi Niko karibu nao. Naitika maombi ya mwombaji anaponiomba Basi na waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka.
                                      

Maneno hayo yenye ufasaha usioweza kukataliwa na mfasaha yeyote, ndiyo asili na misingi ya Saumu. Yeyote abishanaye au kukaidi Amri tunamjibu na kumlainisha kwa Nassi hiyo. Maana Ya ‘Saumu ’ Neno ‘Saumu’ ki lugha ya Kiarabu lina maana ya kujizuia. 

Comments