JE BINADAMU ANAO UHURU KATIKA MATENDO YAKE AU LA?

JE BINADAMU ANAO UHURU KATIKA MATENDO YAKE AU LA?
Moja ya maswali yanayovutia watu wengi wakiwemo wanafalsafa ni juu ya asili ya mwanadamu na maisha yake kwa ujumla, tatizo lenyewe linaanzia katika kutaka kufahamu kama binadamu ana uhuru kamili katika matendo yake au anadhibitiwa? Je, matamanio yake na mwelekeo wa maisha na uhuru alionao katika maamuzi ndio vitu pekee vinavyomfanya awe katika hali fulani? Au matendo na tabia zake vyote hivyo vimedhibitiwa? Je, kuna vitu fulani katika mazingira anamoishi vinamlazimisha yeye kuwa katika hali fulani?
Ili kufahamu umuhimu wa swali hili ni vyema ikumbukwe kwamba jibu lake linategemea faida tunayoweza kuyapata ya kiuchumi, sheria, dini, saikolojia na matawi mengine mengi ya taaluma ambayo binadamu ndio mlengwa mkuu.
Suala la kuwa binadamu anao uhuru katika mambo yake au sio halihusu nyanja ya kielimu au falsafa tu, bali yapaswa lihusishe kila nyanja.
Lakini juu ya jambo kwamba huyu binadamu anao uhuru pia sio la kulipinga moja kwa moja kwa sababu kama hana uhuru wowote vipi juu ya hukumu ya siku ya Mwisho? Kwa waliofanya mema watalipwa pepo na wale watakaofanya maovu kuwa watapewa adhabu ya Moto. Kama binadamu anatenda kama alivyopangiwa na Mwenyezi Mungu, anapewa malipo ya nini au adhabu ya nini na je haitokuwa dhulma kumwadhibu mtu ambaye hakuwa na maamuzi na yote aliyofanya kwa mujibu wa mipango ya Muumba?
Baada ya kuenea kwa Uislamu, Waislamu nao walikuwa wakijihusisha kwa kiasi kikubwa kupata majibu ya swali hilo kwamba binadamu yu ana uhuru au la?
Watu wa vipindi vyote viwili, wakati uliopo au wakati uliopita wanaweza kugawanywa katika makundi mawili kuhusiana na suala hilo la kuwa binadmu anao uhuru au la?
Kundi la kwanza lenyewe linapinga binadamu kuwa na uhuru katika vitendo vyake na kama matendo yake yataonyesha aina fulani ya uhuru basi hiyo ni kwa sababu ya ufinyu wa ufahamu wa binadamu (yaani kwamba ni kutokana na makosa tu).
Kundi la pili ni lile linalo amini kwamba binadamu anao uhuru kamili katika mambo yake, uwezo wake wa kufikiri na kuamua una athari kubwa katika matendo yake na wala hautegemei mazingira.
Kwa kweli binadamu anakabiliwa na mambo fulani ambayo hana amri juu yake. Mfano kuzaliwa, kufa na mambo mengine mengi tu yanayomzunguka. Kwa sababu hiyo ndio maana watu wengine wakalazimika kuamini kwamba binadamu hana uhuru kabisa katika matendo yake.
Wakati huohuo binadamu anatambua kwamba yeye yuko huru kabisa. Mfano anao uwezo wa kupambana na vikwazo vingi katika maisha yake pia katika harakati za kuyakabili mazingira yanayomzunguka kwa kutumia elimu aliyo nayo, lakini kuna ukweli ambao kamwe hawezi kukanusha nao ni juu ya jinsi anavyoweza kuitumia mikono yake na miguu, lakini wakati huo huo akashindwa kufanya hivyo kwa viungo kama vile moyo, ini na
mapafu.
Kwa kuwa na matakwa, uwezo wa kufahamu na uwezo wa kuchagua vitu ambavyo vinavyompa sifa ya ubinadamu na ndio chanzo cha majukumu na wajibu alionao, binadamu
anatambua wazi kabisa kwamba kuna mambo ambayo yanauwezo wakufanyika pasipo ridhaa ya mwanadamu huyo na mambo hayo yanachukua sehemu kubwa sana ya maisha
yake.
Tutaendelea na mada insha-Allah.

Comments