JE MTUME (S.A.W.W) ALIACHA AMEMTEUA KHALIFA

JE MTUME (S.A.W.W) ALIACHA AMEMTEUA KHALIFA
Kumbukumbu za tarikh ya Mitume inaonyesha waziwazi kuwa: Kila alipoondoka Mtume aliweka mtu wa kushika mahala pake, na hapa tutaonyesha kwa ufupi: Wakati iliposhuka Aya 214 katika Sura ya Ash'Shuaraa, Mtukufu Mtume (s.a.w.) alisema:
"Enyi Bani Abdil Muttalib! Hakika mimi wallahi simjui kijana yeyote katika Waarabu, aliyewaletea watu jambo bora kabisa kuliko nililokuleteeni mimi. Hakika mimi nimekuleteeni kheri ya dunia na ya akhera, Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikuiteni kwake, basi nani kati yenu atakayenisaidia jambo hili ili awe ndugu yangu na wasii wangu na Khalifa wangu kwenu? Watu wote wakanyamaza, nikasema (Ali) na mimi ni mdogo wao kwa umri, mng'avu wao wa macho, mkubwa wao wa tumbo, mnene wa miundi, mimi ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu nitakuwa waziri wako. Pale pale akanishika shingo yangu, kisha akasema: Hakika huyu ni ndugu yangu, na wasii wangu, na Khalifa wangu kwenu, basi msikilizeni na mtiini".
Akili, na maandiko, pamoja na matukio ya tarikh, vyote vinaonyesha kwa pamoja kuwa: Msingi wa asili katika hukumu ni maamuzi ya Mwenyezi Mungu tu peke yake, na yeye ndiye anayemtawalisha amtakae katika waja wake.
Tukio la Ghadir Khum ni tangazo muhimu Ia uongozi mkuu, lililokamilisha dini na neema na radhi ya Mola. Tarehe kumi na nane mfungo tatu Mtukufu Mtume (s.a.w.) alipokuwa akirejea Madina kutoka Makka katika mwaka wa kumi baada ya kumaliza ibada ya Hija alifika mahali katika bonde la Khum akiwa na Waislam zaidi ya laki moja. Mwenyezi Mungu akateremsha Aya: "Ewe Mjumbe fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu, hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu wanaokufuru" (5:67).
Baada ya kushuka Aya hii, Mtume (s.a.w.) alimshika mkono Imam Ali (a.s.) akasema:- "kwa kila ambaye mimi natawalia mambo yake, basi huyu Ali ni mtawala wake. Ee Mola! Muunge mkono atakaye muunga, na mfanyie uadui atakaye mfanyia uadui".
Ilipokamilika hutuba ya Mtume (s.a.w.) Masahaba walianza kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s.) kama tunavyomnukuu hapa Umar bin Khattab:- "Hongera ewe mwana wa Abu Twalib sasa umekuwa kiongozi wangu na kiongozi wa Waislamu wote".
Tazama; Tarikhu Dhahbi J.2 Uk. 197. Tariku Baghdad J.8 Uk. 290. Tarikhu Ibn Asakir J.2 Uk. 45. Al Isaba J.1 Uk. 305. Tafsirul Kabir J.12 Uk. 49. Addurrul Manthur J.5 Uk. 182. Ansabul Ashraf J.2 Uk. 315. Albidayatu Wannihaya J.7 Uk. 359
Hata hivyo, wako baadhi ya Masahaba waliopinga kitendo hiki cha kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s.). Baada ya Masahaba kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s.) Harithi bin Nuuman Al'fahri, alimkabili Mtume (s.a.w.) akamwambia: Ewe Muhammad! umetuamrisha kushuhudia kuwa hapana apasae kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu na wewe ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, tumekubali. Umetuamrisha kusali mara tano kila siku, tumekubali. Umetuamrisha kutoa zaka katika mali yetu, tumekubali. Umetuamrisha kufunga mwezi wa Ramadhani kila mwaka, tumekubali. Umetuamrisha Kuhiji AI'kaaba, tumekubali. Kisha hukutosheka yote haya mpaka umempandisha mtoto wa ammi yako juu ya shingo zetu! Hili ni wazo lako au ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu?"
Mtume (s.a.w.) akajibu:- "Wallahi, hapana apasaye kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu, hili si langu isipokuwa ni Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu".
Harithi akaondoka zake na huku akisema: "Ee Mola! ikiwa haya anayosema Muhammad ni kweli, basi tuteremshie mvua ya mawe au tuletee adhabu nyingine kali". Naam, pale pale alipokuwa, Mwenyezi Mungu akamdondoshea kijiwe kikagonga utosini kikatokezea kwenye tundu ya nyuma akafa papo hapo. Mwenyezi Mungu akateremsha Aya ya kwanza na ya pili katika Suratul Ma'ariji: "Muombaji aliomba juu ya adhabu itakayotokea, kwa makafiri hapana awezae kuzuia" Taz: Tafsirul Qurtubi J.18 Uk. 278.
Tukio la Ghadir Khum ni ujumbe muhimu sana kwa Waislamu, na kila anayeshuhudia: "LAA ILAHA ILLA LLAHU MUHAMMADUN RASULULLAH" Lazima vile vile atoe kiapo cha utiifu kwa uongozi wa Ahlul Bait (a.s.). Kwa sababu tarikh inaonyesha kuwa Masahaba waliokataa kutoa kiapo chao kwa Imam Ali, Mwenyezi Mungu aliwaadhibu. Katika hao walioadhibiwa ni huyu Harithi bin Nuumani Al'fahri, kama ulivyoona kisa chake hapo juu.
Pia tarikh inaonyesha kuwa Sahaba Zaid bin Ar'qam alipotengua kiapo chake cha utiifu kwa Ahlul Bait, alipofuka macho yake mara moja. Taz: Manaqibul Imam Ali Uk. 23

Comments