MAANA YA UTUME

MAANA YA UTUME
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma mwenye kurehemu.
 Sifa njema zote (Himidi)  ni za Mwenyezi Mungu pekee, mola wa walimwengu. Na rehema na amani ziwe juu ya mtume wake Muhammad (s.a.w), na kizazi chake chema na kilicho twahirika.

Hukumu ya mbinguni na ardhini inapokuwa ni ya Mwenyezi Mungu mtukufu -pekee- bila ya kuwa na mshirika au mwenye kugombea cheo hicho, kwa kuzingatia kuwa yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipo kuwa yeye tu, Mfalme mtakasifu mwenye usalama, mtoaji wa amani, mwenye utawala wa kuyaendesha mambo yote, mtukufu, mwenye nguvu na ushindi na mwenye utukufu wote na “Yeye ni Mwenyezi Mungu muumba na mwenye kuvipa vitu maumbile, majina yote mazuri ni yake” na “Yeye ni Mwenyezi Mungu ambaye hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye, Mjuzi wa mambo ya ghaibu (yasiyo onekana) na yaonekanayo, Yeye ndiye mwingi wa rehma mwenye kurehemu”, basi hukumu inapokuwa ni ya Mwenyezi Mungu kwa undani huu na upana huu na kwa ushahidi wa dalili na maumbile, hakika jukumu la kwanza la hakimu huyu -kwa upole wake na ukarimu na kwa fadhila yake- ni lazima awawekee viumbe mambo ambayo yataufanya usalama na utulivu wao ubakie na mambo yenye kuzilinda haki zao na utukufu wao, na kuzitengeza (kuzitakasa) kabisa tabia zao na mwenendo wao. Kama ambavyo miongoni mwa majukumu yake ya mwanzo ili kukamilisha fadhila zake na neema zake na upole wake ni kuwafikishia viumbe wote kwa vizazi vyao vyote upambanuzi wa sheria zile na hukumu zile, ili manufaa  yake yaweze kuwafikia wote na hoja nayo iweze kutimia kwa viumbe wote.

Na -kwa ufupi- hii ndio mana ya “Utume” kwa maana yake ya ujumla. Na kutokana na akili ya mwanadamu, kuwa ni yenye kupanuka na kuendelea, kila zama na karne zinavyo pita, na ikiwa kwenye maendeleo yenye kupanuka na mwendo wake wa haraka kuelekea kwenye kukomaa na kuzama na ufahamu ulioenea pande zote, sheria za mbinguni (takatifu) zilikuwa zikishuka taratibu kulingana na maendeleo ya akili na kupanuka kwake, kiasi kwamba katika kila zama na kwa kila kaumu sheria zile ziko katika kiwango kinachowiana na maslahi ya zama zile na watu wale na zenye kulingana na kiwango cha ukuaji wa fikra wa zama zile na watu wake, zikafikia kileleni (zile sheria) katika ujumbe wa kiislamu (Kupitia Mtume Mohammad (s.a.w.w)) ambazo alizichagua Mwenyezi Mungu mtukufu ili ziwe ni sheria bora za mwanadamu katika zama za kukua kwake kiakili na kufikia kilele cha mwisho na katika zama za  maendeleo yake ya utamaduni wenye kushangaza na ulio mkubwa.
Inshallah tutaendelea kuujadili utume kwa upana zaidi.

Na ninataraji msaada na msukumo wa Mwenyezi Mungu.
“Ewe Mola wetu! Hakika sisi tumemsikia muitaji akiita (watu) kwenye Imani ya kwamba “Muaminini Mola wenu” tuka amini. (Ewe) Mola wetu! Tusamehe madhambi yetu na utufishe pamoja na watu wema. (Ewe) Mola wetu! Tupe ulichotuahidi kwa Mitume wako na usituache siku ya kiama (ya mwisho). Hakika wewe huendi kinyume na ahadi”.


Comments