MATUKIO MUHIMU YALIYOTOKEA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI
Katika Historia, tunasimuliwa baadhi ya matukio ya
mwezi huu huu wa Ramadhani, kwa mfano:
1.
Imam Hassan bin Ali bin Abi Talib ni mwanawe Sayyidna Ali
(Imam wa kwanza) na ni Mjukuwe Mtume (s.a.w.); alizaliwa mwezi huu wa Ramadhani
tarehe 15 mwaka wa 3 wa tangu Mtume Kuhama toka Makkah kwenda Madina. Mtume
mwenyewe ndiyo aliyemfanyia Akika kwa kumchinjia mbuzi alipotimiza siku 7. Sayyidna
Hassan, kama ilivyokuja katika Historia, alimfanana sana Babuye, Mtume (s.a.w.)
sehemu ya juu. Naye Mtume (s.a.w.) alimbashiria kuwa “Bwana wa vijana wa
peponi.”
2.
Vita vya Badr vinavyojulikana zaidi kama vita vikuu vya Badr,
au Ghazwatul Badr, vilitukia siku ya Ijumaa mwezi wa Ramadhani tarehe 17 mwaka
wa 2 hijria (624 A.D.). Vita hivi ndivyo vilivyopambanua baina ya wakweli na
waongo. Mushirikina (waabudu masanamu) waliharibikiwa sana na Waislamu ndio
walioibuka na ushindi.
3.
Katika mwezi huu huu, Mtume (s.a.w.) aliirudisha Makkah chini
ya himaya ya Kiislamu tarehe 10 mwaka wa 8 hijria (630 A.D.). Baada ya kuiteka
Makkah, dini ya Islamu ilizidi mno nguvu na makafiri kuharibikiwa.
4.
Imam, Sayyidna Ali bin Abi Talib, bin Ami yake Mtume (s.a.w.)
aliyezaliwa katika Kaaba, alipigwa upanga na adui wa Uislamu, Abdur Rahman bin
Muljim tarehe 19 ya mwezi huu wa Ramadhani mwaka wa 40 Hijria. Alipigwa upanga
msikitini huko Kufa, Iraq alipokuwa amekwenda kusali sala ya Alfajiri, na
alifariki siku ya tatu yake, yaani tarehe 21 Ramadhani. Sayyidna Ali, Simba wa
Mungu alishirikiana sana na Mtume (s.a.w.) na kuhudhuria vita vyote pasi na
kukimbia na ndiye aliyebaki katika kitanda cha Mtume alipokuwa akihamia Madina.
Comments
Post a Comment