KIFO CHA IMAM
ALLY BIN ABITALIB (A.S)
Siku kama ya leo ndio siku ambayo khalifa wa kwanza wa waislamu wote, Imam
Ali (a.s.) alipata pigo la bapa lenye sumu la upanga uliolaaniwa wa Abdul
Rahman lbn Muljim. Ilikuwa mnamo tarehe 19 ya Mwezi wa Ramadhani wa mwaka wa 40
Hijiriya, kuwa Hadhrat Ali (a.s.) alipata
pigo hili kali sana alipokuwa akisali sala ya Alfajiri katika Msikiti wa
mji wa Kufa (nchini Iraq).
Muuaji huyo alipoletwa mbele yake, huruma za sahaba huyu wa Mtume
(s.a.w.) zilimjia na akawaambia wanawe, “Huyu ni mateka wenu. Wala
msimtaabishe. Mpeni chakula kile kile mnachokula ninyi wenyewe. Nikipona
nitaweza kumuadhibu au kumsamehe lakini kama nikifa, na
ikiwa mnataka kumwadhibu basi mpigeni dharuba moja tu kwa sababu yeye
alinipa dharuba moja tu. Msimkatekate viungo vyake kwani kufanya hivyo ni kinyume
na mafundisho ya Uislamu”.
Sumu kali ilifanya kazi yake na mnamo tarehe 21 mwezi wa Ramadhani,
Hadhrat Ali (a.s.) alifariki dunia. Wanawe Hasan na Husain (Amani ya Mwenyezi
Mungu na iwe juu yao wote) walimfanyia ibada za maziko na
lile ua la utu lililazwa kwenye mapumziko yake ya milele katika ardhi ya
Najaf, nchini Iraq.
Ole wao wale wabaya wa ulimwengu ambao hawakuweza kuyavumilia maisha ya
Mchamungu huyu, aliyekuwa bingwa wa amani, usawa, udugu na ubinadamu. Watu hawa
wanaendeleza ugaidi wao wa kuwaua watu bila huruma na katika kila kona ya
dunia.
Tunamwomba Allah awadhoofishe wauaji wote na kuupa nguvu Uislamu sahihi
na wa amani.
Comments
Post a Comment