THAMANI YA SWALA NDANI YA UISLAMU:
Swala huchukuliwa kuwa miongoni mwa mambo ya muhimu zaidi ya
Uislamu na nguzo zake. Imepokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (s.a.w.w) kuwa alisema: “Swala ni nguzo ya dini, ikikubaliwa matendo
mengine hukubaliwa, na ikikataliwa na matendo mengine hukataliwa”3
Daraja hii kubwa ya sala ndiyo tunayoiona katika Aya za Qur’an na Hadithi
Tukufu, ikiwemo:
i. Kudumisha Swala ni miongoni mwa sifa muhimu za waumini:
“Hakika wamefuzu wenye kuamini. Ambao ni wanyenyekevu katika
Swala zao”.4
“Na ambao Swala zao wanazihifadhi.”5
ii. Kutekeleza Swala ni miongoni mwa sababu za udugu wa
kiislamu:
“Na kama wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu
zenu katika dini …”.6
iii. Kusimamisha Swala ni miongoni mwa sifa za jamii bora:
“Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Swala na hutoa Zaka
na huamrisha yaliyo mema na hukataza yaliyo mabaya, na kwa Mwenyezi Mungu ndiko
mwisho wa mambo”.7
iv. Swala ni nyenzo ya mafanikio:
“Hakika amekwishafaulu aliyejitakasa. Na akakumbuka jina la Mola wake na
akaswali.”8
v. Kuwaelimisha watoto Swala ni katika majukumu ya wazazi:
“Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee kwa hayo, hatukuombi riziki
bali Sisi tunakuruzuku, na mwisho mwema ni kwa mcha Mungu.”9
vi. Swala ni katika nguzo za dini:
“Wala hawakuamrishwa ila kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia yeye
dini, hali wameshikamana na haki, na wanasimamisha Swala na kutoa Zaka, na hiyo
ndiyo dini madhubuti.”10
vii. Swala ni shukrani kwa Mneemeshaji:
“Hakika Sisi tumekupa kheri nyingi.* Basi sali kwa ajili ya Mola wako,
na uchinje.* Hakika adui yako ndiye aliyekatikiwa kizazi”.11
Hivyo kila mwislamu ajitahidi kuswali swala zote za faradhi na ajitahidi
kuswali swala za Sunnah.
Rejea
3. Biharul-An'war, Juz. 47 Uk. 2.
4. Sura Al-Muuminun: 1 - 2.
5. Sura Al-Muuminun: 9.
6. Sura At-Tawba: 11.
7. Sura Al-Haji: 41.
8. Sura Al-Aaala: 14 - 15.
9. Sura Twaha: 132.
10.Sura Al-Bayyinah: 5.
Comments
Post a Comment