ZAKA YA FITRI
Allah
anasema, “Hakika
amekwisha faulu aliyejitakasa (na mabaya kwa kutoa zaka) na akakumbuka jina la
Mola wake na akasali.” (Al-A’la : 14-15). Zaka ya Fitri ambayo kwa jina jengine
huitwa ‘Zaka ya kiwiliwili’ ni faradhi ambayo ilifaradhiwa ili kuwatakasia
waliofunga Saumu zao. Zaka hii ya Fitri, humlazimu mtu aliyebaleghe, aliye na
akili, huru, na mwenye kuweza.
Mbali na kuwa utakaso kwa viwiliwili,
Fitri hii huwa ndicho kifurahisho kwa asiye na uwezo ili naye apate kufurahia
siku ya kufuturu (siku ya Iddi) kama wenzake. Aliyeyatimiza masharti ya kuitoa
zaka hii, hulazimika kujitolea yeye mwenyewe na kumtolea kila anayehesabika
kuwa wa familia yake na anayemlazimu kumlisha hata kama ni mgeni akiwa alimjia
kabla ya kuingia usiku wa kuamkia Iddi. Ama mgeni aliyefika baada ya kuingia
usiku, na mtoto aliyezaliwa baada ya kuingia usiku, yaani Magharibi, hawalazimu
kuwatolea zaka hii ya Fitri.
Wakati wa kuitoa, ni baada ya kuingia
usiku wa kuamkia Iddi, na ni vizuri zaidi kuitoa kabla ya Kusali sala ya Iddi.
Kitolewacho ni tende, ngano, shayiri (barley) na zabibu au kiwango (senti) cha
chakula kitumikacho zaidi nchini.
Kila mtu hutolewa pishi (kilo tatu -
3kg). Wapewao zaka hii ya Fitiri, ni Waislamu wenye imani wasiojiweza. Ni Sunna
kuwatanguliza katika ugawanyaji, watu wako, yaani wa ukoo wako, kisha majirani
walio fukara (masikini). Na miongoni mwa wanaostahili kupewa, ni vyema
kuwatanguliza wenye elimu kisha wenye dini zaidi. Ama (Mwisilamu) mlevi, na
asiyesali watu hao hawapewi.
Comments
Post a Comment