EIDIL AL-GHADIIR NI UKAMILIFU WA UISLAMU
Ijumaa tarehe 18 dhulhajj sawa na tarehe 2/10/2015 ni siku
muhimu sana kwetu waislamu kutokana na kwamba siku hii ndio siku ambayo Mtume
Muhammad (s.a.w.w) alimtangaza Imam Ally kuwa khalifa wake wa kwanza, katika
eneo liitwalo Ghadiir, lililopo baina ya Makkah na Madina, pindi ambapo Mtume
alikuwa ametoka hijja yake ya mwisho.
Nakuombeni tuisherehekee siku hii kwa kufanya ibada mbali
mbali ikiwemo kuwasaidia wenye shida na kuhimiza amani ya nchi yetu.
Allah (s.w) anasema, “Ewe Mtume, fikisha uliyoteremshiwa
kutoka kwa Mola wako; na kama hutafanya, basi hujafikisha ujumbe wake, na
Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. (Qur'an: 5, 67)
Agizo lililotajwa na Aya hiyo ya Qur’an lilitekelezwa na
Mtume (s.a.w.w.) alipomteua Imam ‘Ali bin Abi Talib (a.s.) kuwa wasii wake
kwenye siku ya Ghadir Khumm.
Ghadir Khumm ni sehemu iliyoko maili kadhaa kutoka Makka
kwenye barabara ielekeayo Madina. Mnamo tarehe 18 Dhul hijja (Mfungo tatu),
Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akipita sehemu hii akirejea kutoka kwenye Hijja yake
ya kuaga (ya mwisho), Aya hii ilishuka: “Ewe Mtume fikisha uliyoteremshiwa…”
Hivyo alisimama kuwatangazia mahujaji aliokuwa amefuatana nao kutoka Makka na
ambao walikuwa watawanyike kutoka kwenye njia panda hiyo na kuelekea sehemu
mbalimbali waendazo. Mtume akaamrisha mimbari maalum ya matawi ya miti
itayarishwe kwa ajili yake. Baada ya Swala ya adhuhuri, Mtume (s.a.w.w.)
aliketi juu ya mimbari hiyo na kutoa hotuba yake ya mwisho, akiihutubia
kadamnasi kubwa kabla ya kifo chake miezi mitatu baadaye.
Jambo kubwa lililojitokeza katika hadhara hii ni pale
alipomshika mkono Imam ‘Ali (a.s.) na kuwauliza wafuasi wake iwapo yeye (Mtume)
alikuwa ni bora zaidi (awla) katika mamlaka kuliko wao wenyewe. Hapo mkusanyiko
wa watu ulijibu kwa sauti moja kuu: "Ni hivyo ee Mtume wa Mwenyezi
Mungu."
Kisha Mtume (s.a.w.w.) akatangaza: "Ambaye mimi ni
Bwana (Mawla) wake, basi 'Ali pia ni Bwana wake. Ewe Mwenyezi Mungu, mpende ampendaye, na uwe
ni adui wa amfanyiaye uadui."
Mara tu Mtume (s.a.w.w.) alipomaliza hotuba yake, ilishuka
Aya hii:
“Leo nimewakamilishieni dini yenu, na kuwatimizieni neema
yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu”. (Qur'an 5:3).
Baada ya kumaliza hotuba yake, Mtume (s.a.w.w.) alimtaka
kila mtu kutoa kiapo cha utii kwa 'Ali (a.s.) na kisha akampongeza. Miongoni
mwa waliompongeza ni 'Umar bin al-Khattab, aliyesema: "Hongera Ibn Abi
Talib! Leo umekuwa Bwana wa kila muumini, wanaume na wanawake."
Mwarabu mmoja aliposikia tukio la Ghadir Khumm, alikwenda
kwa Mtume (s.a.w.w.) na kumwambia: "Ulituamrisha kushuhudia ya kwamba
hapana Mungu ila Allah na wewe ni Mtume wake, tukakutii. Ulituamrisha kuswali
Swala tano kila siku, tukakutii. Ulituamuru kufunga katika mwezi wa Ramadhani,
tukakutii. Ukatuamuru kuhiji Makka pia tukakutii. Lakini hukutosheka na hayo
yote, kwa mkono wako ukamwinua binamu yako na kutulazimisha sisi awe bwana wetu
ukisema 'Ali ni bwana wa yule ambaye mimi ni Bwana wake.' Kulazimishwa huku
kunatoka kwa Mwenyezi Mungu au kunatoka kwako?" Mtume (s.a.w.w.) akasema: "Naapa kwa
Mungu wa pekee! Hii ni amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu mkuu, Mtukufu."
Aliposikia majibu haya, yule mtu aligeuka na kumuelekea
ngamia wake huku akisema: "Ee Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ayasemayo
Muhammad ni sahihi, basi tuteremshie jiwe kutoka mbinguni na utuadhibu
vikali." Basi mtu huyo kabla hajamfikia ngamia wake, Mwenyezi Mungu
alimteremshia jiwe lililomwingia mwilini mwake kupitia kichwani kwake na
kumwacha akiwa amekufa. Ilikuwa katika tukio hili ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu
alipoteremsha Aya ifuatayo: Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayotokea. Juu
ya Makafiri - ambayo hapana awezaye kuzuia. Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye
utukufu mkubwa. (Qur'an 70:1-3)
Je Wanavyuoni wa Sunni hulichukulia tukio hili kuwa ni la
kweli? Idadi kubwa ya Wanavyuoni wa
Sunni waliosimulia tukio hili, kwa urefu na kwa muhtasari, ni ya kushangaza!
Tukio hili la kihistoria limesimuliwa na Maswahaba wa Mtume 110, pia Tabiina
(waliokuwako baada ya Maswahaba) wapatao 84, na Wanavyuoni wengi wa ulimwengu
wa Kiislamu, kutoka karne ya 1 AH hadi karne ya 14 AH (Karne ya saba hadi ya
ishirini miladia).
Takwimu hizi ni zile tu za wapokezi waliotajwa katika Hadith
zilizopokewa na Wanavyuoni wa Sunni!
Idadi chache sana mkusanyiko wa misingi ya marejeo imetajwa hapo chini.
Wengi wa Wanavyuoni hawa hawakunukuu hotuba ya Mtume tu bali pia wameiita kuwa
ni sahihi, nayo ni:
al-Hakim al-Naysaburi, al-Mustadrak `ala al-Sahihayn
(Beirut), Juz. 3, Uk. 109- 110, Uk. 133, Uk. 148, Uk. 533. yeye amesisitiza
kuwa Hadith hii ni sahih kulingana na
vipimo vya al-Bukhari na Muslim;
al-Dhahabi pia amethibitisha hili.
al-Tirmidhi, Sunan (Cairo), Juz.. 5, Uk. 633
Ibn Majah, Sunan, (Cairo, 1952), Juz. 1, Uk. 45
Ibn Hajar al-'Asqalani, Fath al-Bari bi Sharh Sahih
al-Bukhari, (Beirut, 1988), Juz. 7, Uk. 61
Al-'Ayni, 'Umdat al-Qari Sharh Sahih al-Bukhari, Juz. 8, Uk.
584
Ibn al-'Athir, Jami` al-'Usul, i, 277, Na. 65;
Al-Suyuti, al-Durr al-Manthur, Juz. 2, Uk. 259 na Uk. 298
Fakhr al-Din al-Razi, Tafsir al-Kabir, (Beirut, 1981), Juz.
11, Uk. 53
Ibn Kathir, Tafsir Qur'an al-'Adhim, (Beirut), Juz. 2, Uk.
14
Al-Wahidi, Asbab an-Nuzul, Uk. 164
Ibn al-'Athir, Usd al-Ghaba fi Ma'rifat al-Sahaba, (Cairo),
Juz.3, Uk. 92
Ibn Hajar al-'Asqalani, Tahdhib al-Tahdhib, (Hyderabad,
1325), Juz. 7, Uk. 339
Ibn Kathir, al-Bidayah wan Nihayah, (Cairo, 1932), Juz. 7,
Uk. 340, Juz. 5, Uk. 213
Al-Tahawi, Mushkil al-Athar, (Hyderabad, 1915), Juz. 2, Uk.
308-9
Nur al-Din al-Halabi al-Shafi'i, al-Sirah al-Halabiyya, Juz.
3, Uk. 337
Al-Zurqani, Sharh al-Mawahib al-Ladunniyya, Juz. 7, Uk. 13
Lakini je, neno mawla halina maana ya rafiki?
Japokuwa idadi kubwa ya Wanavyuoni wa Sunni wa zama zote na
maoni yote wamethibitisha tukio hilo na maneno ya kihistoria ya Mtume
(s.a.w.w.), lakini imekuwa ni vigumu kwao kukubaliana na yaliyotokea baada ya
kufariki Mtume (s.a.w.w.). Lakini nakala
hii fupi haiwezi kutaja kwa ufafanuzi matukio hayo. La muhimu ni kwamba
Wanavyuoni wengi wa Sunni wamedai kwamba Mtume (s.a.w.w.) alimtangaza ‘Ali
(a.s.) kuwa ni rafiki na msaidizi wa Waislamu!
Kuna mitazamo mingi ya tukio hili inaoonyesha jinsi
lilivyokuwa na umuhimu. Miongoni mwayo
ni kufunuliwa kwa Aya nyingi za Qur’an, mkusanyiko mkubwa wa watu, hatua za
mwisho za maisha ya Mtume (s.a.w.w.), watu kuthibitisha kwamba Mtume (s.a.w.w.)
alikuwa na mamlaka makuu, kupongezwa baada ya tukio hilo na ‘Umar, na sababu
sababu nyingine nyingi ambazo haitoshi kuzitaja katika nakala hii fupi; yote
yanaonnyesha juu ya kutawazwa kwa wasii wa Mtume (s.a.w.w.). Ni dhahiri kwamba
neno mawla lilitumika kwa maana ya mamlaka kamili baada ya Mtume na si kwa
mamlaka ya muda tu.
Neno la Mwisho
Ikiwa bado kuna shaka juu ya umuhimu wa kihistoria wa hotuba
hii, na bidii ya baadhi ya watu ya kuificha, hebu basi neno la mwisho liwe ni
hili:
Wakati Imam 'Ali (a.s.), alipokuwa khalifa, na hapo ni
miongo kadhaa baada ya tukio la Ghadir, siku moja alimwambia Anas bin Malik,
swahaba wa Mtume (s.a.w.w.): “Kwa nini hutoi ushahidi kwa uliyoyasikia kwa
Mtume siku ya Ghadir?" Akajibu, "Ee Amir ul-Muminin! Nimezeeka na
siwezi kukumbuka." Hapo 'Ali (a.s.) akasema: "Mungu atakupa doa jeupe
(la ukoma) lisilofichika na kilemba chako! Ikiwa kwa makusudi waficha ukweli!”
Na kabla Anas hajainuka pale alipokuwa amekaa, alipatwa na doa kubwa jeupe
usoni kwake.
Ibn Qutaybah al-Dinawari, Kitab al-Ma'arif, (Cairo, 1353
AH), Uk. 251
Ahmad bin Hanbal, al-Musnad, Juz. 1, Uk. 119
Abu Nu`aym al-’Isfahani, Hilyat
al-Awliya', (Beirut, 1988), Juz. 5, Uk. 27
Nur al-Din al-Halabi al-Shafi'i, al-Sirah al-Halabiyya, Juz.
3, Uk. 336
Al-Muttaqi al-Hindi, Kanz ul-'Ummal, (Halab, 1969-84), Juz.
13, Uk. 131
Comments
Post a Comment