FAIDA ZA
DINI NI ZIPI?
Zipo sababu
nyingi zimfanyazo mwanadamu ahitaji Dini.
1. Sote
twajua kuwa mwanadamu ni mnyama ahitajiye kuishi kijamii pamoja na wenzake.
Kila mtu anategemea mamilioni ya watu wenzake kwa maisha yake na kwa mahitaji muhimu
ya hayo maisha yake. Pia tunajua kuwa kila jamii inahitaji sheria fulani fulani ili kuzuia dhulma na
kuhifadhi haki ya kila mtu katika jamii hiyo. Lakini basi swali lifuatalo ni
hili, ni nani aliye na haki ya kutunga Sheria hizo? Mtu mmoja? (mtu huyo na awe
mfalme au mtawala wa Kiimla)! Jibu ni “Hapana.” Yeye hataweza, maana kwa ajili
ya silika za kibinadamu, atatunga sheria kwa kufuatana na tamaa yake ya
kibinafsi.
Kikundi cha
watu? (Watu hao na wawe wa kikundi cha Utawala wa watu wa koo Bora au wa
kikundi cha kidemokrasi)! Jibu ni kuwa,
“Hawa pia hawataweza kuifanya kazi hiyo ipasikavyo,
maana kila mmoja wao hawezi kujiepusha
na uamuzi usio sawa na wingi wa uamuzi usio sawa, hauwezi kupatana na uamuzi
ulio sawa.
2. Vile vile
ni dhahiri kuwa hakuna kikundi cha watu kiwezacho kujiepusha na kujitia katika
tamaa za kibinafsi. Kwa mfano katika siku za utawala wa kikoloni, mabunge na
halmashauri za Makoloni zilikuwa
zikitunga sheria kufuatana na
mapendekezo ya watawala wa Kizungu. Siku hizi, mabunge na Halmashauri
hizo hizo hutunga sheria kufuatana na
mapendekezo ya wananchi. Kujali ubinafsi kulikuwa na bado kungali jambo
muhimu la kutunga sheria duniani pote.
3. Zaidi ya
hapo hakuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kutunga sheria za mambo mengi
na ambazo zimo katika msingi wa usawa na uadilifu kamili.
Kwa sababu
hiyo, ni lazima sheria hizo zitungwe na yule ambae ni mbora kuliko mwanadamu,
ambae hana chochote cha kupoteza au cha kufaidika nacho kutokana na sheria
hizo, na ambae kila mwanadamu ana uhusiano wa aina iliyo sawa kwake.
NI ALLAH
pekee ndiye asiyependelea na ni mkamilifu. Kwa sababu hiyo tunawajibikiwa kuwa na dini.
4. Zaidi ya
hapo ni kuwa, sheria na desturi zilizotungwa na
mwanadamu zina upungufu mmoja mbaya sana: Sheria na desturi hizo
haziwezi kuzuia matendo ya jinai. Upungufu huu, hukufanya kuwepo kwa sheria za
aina hii kuwa kusiko na faida yoyote.
Kwa mfano,
mwizi anaingia nyumba isio na watu, katika
kijiji cha ughaibuni, usiku wa manane kwa ajili ya kutaka kuiba vitu vyenye thamani. Yeye aelewa wazi
kuwa hakuna mtu aiwakilishaye Serikali, kwa maili nyingi sana kutoka nyumba hiyo. Hivyo ataona kuwa na usalama
kutokana na kukamatwa. Je! Katika hali
hii, iko sheira ya serikali ambayo
itamzuia mwizi huyu kutimiza jinai hii? Jibu ni kuwa “HAKUNA”.
Kusema kweli
hakuna serikali itakayomzuia mtu huyu kuiba, lakini Dini inaweza. Dini iliyo ya
kweli, kama tulivyoieleza hapo juu, huwafundisha watu kuwa yupo Mwenyezi Mungu,
ambaye ajua kila kitu na anayeona kila kitu. Yeye Mwenyewe ni Mwadilifu na
Mwema na anatutaka nasi tuwe waadilifu na wema; kuwa tunahusikana na matendo
yetu mbele yake na tutakuja mpa hesabu ya matendo yetu baada ya kufa kwetu.
Kama mtu anaiamini dini hiyo basi, hivyo (Na kwa hivyo tu) anaweza kujiepusha
na kutenda dhambi, jinai na kuwadhulumu
watu wengine popote awapo.
Sheria za
serikali zaweza kuzuia mtu kutenda matendo
mabaya ya wazi wazi na hata hivyo, ni katika muda na mahali ambapo mikono ya serikali hiyo yaweza
kupafika. Lakini kumwamini Mwenyezi
Mungu na dini, hutawala si matendo ya mwanadamu ya kiwazi wazi tu bali hata
yale yaiiyojificha na yaliyo mawazo ya
moyoni pia.
Utawala huu,
hauna mipaka kwa kutegemea mahali maalum au muda fulani, kwa sababu Mwenyezi
Mungu yupo kila mahali na anaona kila
kitu.
5. Ili
kuzielewa vizuri faida zilizo wazi wazi, ambazo jamii yazipata kutokana na imani ya kuwepo Mwenyezi
Mungu na dini, hebu jaribu kufikiria machafuko na ghasia ambazo wanaadamu wangeliweza kujitia, kama imani ya
kuwepo Mungu ingalitupiliwa mbali. Hakutakuwa na jamii yoyote. Badala yake, kutakuwa na umati wa watu tu.
Katika hali hiyo, kila mmoja anao uhuru wa kufanya chochote kile akipendacho. Mtu atafikia kuwa hakuna Mungu,
na hakuna maisha ya Akhera, na kuwa yeye amekuwepo hapa duniani kwa bahati ya hali ya asili iliyojitokeza tu.
Na pia anajua kuwa muda wa maisha ni
mfupi. Kwa hivyo, kikawaida
atashawishika na kuyafaidi maisha kwa kadri iwezekanavyo bila ya kujali
kitu chochote kile. Kitu atakacho kiwazia ni
kujaribu kuepuka kukamatwa akiwa anatenda jambo lolote baya, au kuonwa
na serikali tu. Na wakati wowote
atakaojiona kuwa yu salama, hataacha kutenda jinai lolote ili kujikidhia
tamaa zake, bila ya kujali dhara la tamaa yake hiyo kwa wenzake.
Comments
Post a Comment