MTU WA KWANZA KUSILIMU
Ameeleza Ibn Hajar al-Asqalani katika kitabu chake al-Isabah,
kwa namna ya maelezo ya wanavyuoni wengi, kuwa mtu wa kwanza aliyeleta imani na kukubali dini ya Kiislamu
ni Bwana Abul Hasan Ali bin Abi Talib. Ali alizaliwa miaka kumi (10) kabla ya
“Bi’that” (kabla Mtume (s.a.w.w.) kutangaza Utume wake). Alilelewa katika
mikono ya Mtume (s.a.w.w.) na hawakuachana (hawakufarakiana) maisha yao yote.
Abdul Malik Ibn Hisham katika kitabu chake alichoandika juu
ya maisha ya Mtume, kinachoitwa Sirat Ibne Hisham, amehadithia hivi kwamba Ali
ni mtu wa kwanza aliyemwamini Mtume (s.a.w.w.) na akaukubali Uislamu na yale
aliyoteremshiwa Mtume: Umri wa Ali
alipoikubali dini ya Kiislamu ulikuwa miaka kumi (10). Katika neema
aliyombariki Mwenyezi Mungu Ali ni kulelewa na Mtume chini ya uongozi wake wa
haqqi kabla ya kudhihirika Uislamu. Baada ya Ali, Zaid Bin Harth akakubali
Uislamu na akasali na baada ya huyu Zaid, Abu Bakr akaingia katika Uislamu.
Katika kitabu cha maisha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.)
kiitwacho Isteeab alichoandika Ibn Abdul
Bir al-Maliki, amesema kwamba Muhammad
ibn Kaab Qarzi aliulizwa na watu, nani aliyeifuata dini ya Kiislamu kwanza, Ali
au Abu Bakr. Akajibu: “Subhaanallah! Ali ndiye wa kwanza kukubali Uislamu”.
Baadaye Ibn Abdul Bir anaeleza: “Sisi hatuna shaka kwamba Ali
ndiye wa kwanza miongoni mwa hawa wawili (Ali na Abu Bakr) kukubali Uislamu.
Zaidi ya haya Salman
al-Farsi, Abu Dhar, Miqdad, Khabbab, Abu Saeed Khudri na Zaid Bin Arqam
wanashuhudia kwamba hakika Ali ni wa kwanza kukubali Uislamu na masahaba hawa
wamemfadhilisha Ali juu ya masahaba wengineo.”
Comments
Post a Comment