MWANZO WA WAHYI (UFUNUO AU REVELATION)

MWANZO WA WAHYI (UFUNUO AU REVELATION)
Amesema Bukhari na Muslim na wengineo kuwa: Imepokewa kutoka kwa Azzuhry naye amepokea kwa U'rwa bin Zubeir naye amepokea kwa Mwana Aisha (mkewe Mtume) kwamba: Malaika Jibril (a.s) alikuja kwa Mtume (s.a.w.) naye akiwa katika pango la Hiraa akamwambia: Soma.
Mtume akajibu: Mimi sijui kusoma. Mtume anasema: Malaika akanikaba kwa nguvu mpaka nikazidiwa kisha akaniambia: Soma, Mtume akajibu: Mimi sijui kusoma. Kisha ndipo Malaika alipomsisitiza kwa nguvu akisema: "Soma kwa jina la Mola wako, ambaye ameumba. Amemuumba mwanadamu kutokana na damu iliyoganda. Soma na Mola wako ni Mtukufu kuliko wote". (Qur'an, 96:1-3).
Baada ya hapo, Mtume (s.a.w.) alirudi kwa mkewe mwana Khadija (a.s.) akiwa amejawa khofu kubwa. Alipoingia ndani alijitupa chini na huku akilalamika: "Nifunikeni, nifunikeni!!" Alipotulia akasema: "Ninaogopa sijui kitanipata nini?!" Khadija akamtuliza: "Sivyo! Wallahi Mwenyeezi Mungu hatakuangamiza abadani, wewe unaunga udugu, unavumilia matatizo, unasaidia wanyonge, unasaidia kuleta haki."
Kisha Khadija akamchukua Mtume akampeleka kwa Ibnu ammi yake Waraqa bin Nawfal (alikuwa mnasara, mwandishi wa Injili kwa lugha ya kiibrania). Walipofika kwa Waraqa, Khadija akamwambia: "Ewe Ibnu ammi! Msikilize Muhammad aliyo nayo." Waraqa akamuuliza, "una nini?" Muhammad akamwelezea yote kama aliyoyaona, Waraqa akamwambia: "Huyu ni Malaika ambaye amepata kumteremkia vilevile Nabii Musa (a.s.) Ee!!!" Natamani kama nitakuwa hai wakati watakapokufukuza watu wako!!! Muhammad (s.a.w) akashituka: "Watanifukuza??" Waraqa akajibu: "Ndiyo, hakuna mtu yeyote anayeleta jambo kama hili uliloleta wewe isipokuwa atapigwa vita na watu wake".
Tazama:
Sahihi Bukhari J.I uk, 5-6
Sahihi Muslim J. I uk, 97
Almuswannaf J. 5 uk, 322
Tarikhut Tabari J. 2 uk, 47

Ebu tujadili kidogo. Je hadith hizi ziko sahihi? La hasha haziko sahihi. Hadith hizi ziliandikwa na maadui wa Mtume yaani Bani Umaya ili kumdhalilisha Mtume wetu, kwa sababu zifuatazo.
1.  Suala la kumtaalifu mtu kuwa ni mtume hufanywa na Mungu mwenyewe kupitia kwa malaika Jibrail na si vinginevyo.
2.  Ukweli hauwezi kutambulika kwa kupitia upotofu, mnaswara ni mtu aliyepotea njia kwa sababu wao wanaamini kuwa Yesu ni Mungu au mwana wa Mungu, haiwezekani alete hoja kuwa Muhammad ni Mtume wa Allah.
3.  Hadith hii imetumika na wakristo kuudhalilisha Uislamu kwa maana kuwa aidha Muhammad alipewa utume na Khadija au kasisi wa kikristo kwa maana kuwa Mtume wetu alikuwa mtumishi wa kanisa. Allah hawezi kuacha mwanya wa namna hii.
4.  Muhammad (s.a.w.w) alijulikana kuwa ni Mtume tokea alipokuwa motto, haiwezekani ajisahau cheo pindi alipokuwa mkubwa hadi akaambie cheo chake ni wakristo.
5.  Suala la kusoma, Mwenyezi Mungu anasema kumwambia Mtume, “Tutakufundisha na wala hautosahau”. Suala la kumfundisha Mtume halikuwa la kupigana tena kama shule zetu, bali Allah alimfundisha kimuujiza. Kwani inajulikana kuwa ufundishaji wa kawaida watu husahau.

6.  Ilikuwa ni desturi ya wayahudi na wakristo kubuni hadith na kuzipachika katika vitabu vyetu, ni lazima tuwe makini katika kukubali hadith kwa sababu zingine zinakwenda kinyume na Uislamu. Waliagizwa na watawala wa zama hizo kufanya hivyo kwa maslahi ya watawala waliojiita kuwa ni makhalifa.


Nitaleta hadith sahihi kuhusu suala hili, kunako majaliwa ya Mola. 

Comments