MWENYEZI MUNGU MTUKUFU NA SIFA ZAKE NJEMA

MWENYEZI MUNGU MTUKUFU NA SIFA ZAKE NJEMA
Mwenyezi Mungu aliye takasika anazo sifa nyingi kama:
1. ELIMU: Yeye ni mwenye kufahamu kila kitu, kikubwa na kidogo na anayafahamu yaliyomo ndani ya nyoyo.
2. UWEZO: Yeye ni mwenye uwezo juu ya kila kitu, ana uwezo wa kuumba, kutoa riziki, kufisha na kuhuisha na mengineyo.
3. UHAI: Yeye yu hai hafariki.
4. UTASHI: Yeye hukitaka kitu ambacho kina maslahi ndani yake na wala hakitaki kitu ambacho ndani yake kuna ufisadi au uharibifu.
5. KUDIRIKI: Yeye hukiona kila kitu na husikia kila sauti hata kama itakuwa ni kwa kunong'onezana masikioni au kufikiria.
6. UTANGU: Yeye Mwenyezi Mungu pekee ndiye wa tangu na tangu na ndie wa milele, yaani yeye aliye takasika alikuwepo kabla ya kila kitu kisha akaviumba vitu vyote na atabakia kuwepo baada ya vitu hivyo hadi milele na ulimwengu wote huu ni miongoni mwa uumbaji wake, au ni viumbe vyake, viumbe hivyo ni vyenye kumuhitajia si katika kupatikana kwake pekee bali katika kubakia kwake na kuendelea kuwepo kwa vitu hivyo pia, na kila kilicho umbwa basi kitu hicho ni chenye kuzuka, kwa hivyo basi hakuna wa tangu na tangu isipokuwa Mwenyezi Mungu mtukufu.
7. KUZUNGUMZA: Yeye Mwenyezi Mungu ni mwenye kuzungumza, humsemesha amtakaye katika waja wake wema walio takasika na kutakaswa, mitume wake na malaika wake.
8. UKWELI: Yeye ni mkweli katika yale ayasemayo na hakhalifu ahadi zake (yaani haendi kinyume na ahadi zake), kama ambavyo yeye aliye tukuka ni Muumba, mtoaji wa riziki, muhuishaji, mtoaji, mzuiaji, mwenye huruma, msamehevu, mtukufu, mbora na mkarimu n.k.

Tumezitaja sifa chache tu kuwakilisha zingine, lakini Allah anasifa nyingi kuliko hizo na kwa kweli hakuna uwezekano wa kuziongelea zote. Hivyo tutosheke na hizo. 

Comments