UISLAMU ULIANZA KWA KUTANGAZWA UKHALIFA WA IMAM ALLY (A.S) KAMA KHALIFA WA KWANZA

UISLAMU ULIANZA KWA KUTANGAZWA UKHALIFA WA IMAM ALLY (A.S) KAMA KHALIFA WA KWANZA
Abu Muhammad Husain al-Baghawi katika Tafsir Maalim at-Tanzeel  (inaojulikana kwa jina Tafsir al-Baghawi), Shaikh Alau’ddin Ali bin Muhammad al-Baghdadi (anayejulikana kwa jina la Khazin al-Baghdadi) katika kitabu chake Lubab al-tawil ambacho ni mashuhuri na kiitwacho Tafsir al-Kazin, Abu Bakr Ahmad ibn Husayn al- Bayhaqi katika kitabu chake Dalail al-Nubuwwah, Jalaluddin Suyuti katika kitabu chake Jami al-Jawami, Alau’ddin Ali al-Muttaqi katika kitabu chake Kanzul Ummal, Abu Ja’far Muhammad ibn Jarir al- Tabari katika Tarikh al-Rusul wal-Muluk (inaojulikana kwa jina Tarikh al-Tabari), Abi Sa’adat Mubaraka Ibn Athir al-Jazari katika Tarikh al-Kamil, na Isma’il Abul Fida katika Kitab al-Mukhtasar fi Akhbar- il-Bashar, wote hawa wamesema hivi:
kwamba Hazrat Ali amesema:- “Iliposhuka aya “Waandhir Ashiratak-Al-Aqrabin” (Sura Ash-Shu’ara, aya 214) Mtukufu Mtume akaniita na akaniamrisha, ‘Ee Ali Mwenyezi Mungu ameniamrisha niwahadharishie watu wangu adhabu yake. Kwa kuona hali na tabia yao nikiwafikishia maamrisho ya Mola watapinga kufanya yasiyofaa, basi ikanihuzunisha sana na kudhoofika, kwa hivyo nikakaa kimya nikichelewesha zaidi kutangaza maneno ya Mwenyezi Mungu basi ataishusha ghadhabu yake. Kwa hivyo Ee Ali, chukua saa (kipimo) moja ya mchele, na tia mguu mzima wa mbuzi (kitoweo) na bakuli kubwa la maziwa na utengeneze karamu; baadaye na uwaalike  watoto wote wa Abdul Muttalib karamu kwangu ili niwafikishie  maneno ya Mwenyezi mungu.’
Basi nikafanya alivyoniamrisha Mtume, na watoto wa Abdul Muttalib ambao walikuwa kiasi arubaini ambao miongoni mwao walihudhuria Ammi zake Mtume: Abu Talib, Hamza, Abbas na Abu Lahab. Hapo Mtume akaniamrisha nikalete hicho chakula,  akachukuwa kipande cha nyama na akainyambua tena  akazitawanya pembezoni mwa sinia na akasema, “Kwa jina la  Mwenyezi Mungu anzeni kula”. Wote hawa waliohudhuria wakala  shibe yao ingawa chakula kile na bakuli la maziwa kilikuwa cha  kumshibisha mtu mmoja tu.
Baadaye Mtume akataka kusema nao  lakini Abu Lahab mara akadaka maneno na kusema, “Kweli rafiki yenu amekurogeni”. Kwa kusikia maneno haya wote wakaondoka  wakendazao, basi Mtume hakupata fursa ya kusema nao.”
Siku ya pili Mtume akanitaka nitengeneze chakula na kuwaita tena, basi nikafanya vivyo hivyo; wakaja wakala, walipokwisha kula hapo Mtume akawahutubia hivi: “Enyi watoto wa Abdul Mutalib, nimekuleteeni ninyi heri ya duniani na ahera, na Mwenyezi Mungu ameniamuru nikwiteni  mwende kwake (Mwabudu) yeye. Kwa hivyo nani mwenye kuitikia  (kukubali) mwito wangu miongoni mwenu ili awe Waziri wangu, khalifa baada yangu na ndugu yangu pia?”. Hapana mtu aliyeitikia. Lakini mimi (Ali) ijapokuwa  nalikuwa mdogo kuliko wote katika kundi hilo nikasema, “Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi niko tayari hapa kushika Wizara yako katika kazi hii”. Aliposikia Mtume maneno yangu, akanipapasa shingoni kwa upole na akasema “Enyi watu wangu! Huyu Ali ni ndugu yangu, waziri wangu  na mwandani wangu miongoni mwenu. Msikilizeni na mtiini huyu”.  Waliposikia maneno ya Mtume, mara wakacheka kwa sauti na  wakaondoka huku wakimwambia Abu Talib, “Sikiliza! Umeamrishwa kumtii na kumfuata mtoto wako”.
Toleo hili vile vile limetanjwa na Thomas Carlyle katika kitabu chake  Heroes and Hero Worship, vile vile Edward Gibbon katika kitabu chake Decline and Fall of the Roman Empire, John Davenport katika Apology for Muhammad and the Koran, na mwishoni Washington Irvin katika  Muhammad and His Successors, na maelezo yake yote.

Hivyo ukhalifa wa Imam Ally ulitangazwa na Mtume kuanzia siku ya kwanza ya kuutangaza Uislamu. Nasi kama tunataka kheri katika dunia hii na akhera hatuna budi kujiunga na ukhalifa huu wa imam Ally (a.s) na Ahlulbayt wake. Na ili tuwe wafuasi wa ukhalifa wa imam Ally ni lazima tuwe Mashia Imamiya. 

Comments