HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA
UISLAMU
Umoja wa mataifa umeanza
kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya ‘Siku ya
Watoto’ katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya
kutangazwa kwa haki za mtoto.
Ukweli ni kuwa mazingatio ya
Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja
na mia nne.
Uislamu kwa mfululizo
unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali
hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake.
Wakati wa utoto katika Uislamu
umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ndoto
njema.
Na aya za Qur’ani zinaonyesha
mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu: “Naapa
kwa mji huu, (wa Makkah). Na wewe
utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzazi na alichokizaa.” (90:1-3).
Watoto wameelezwa katika Qur’ani
kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu:
“Ewe Zakaria tunakupa
habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya….” (19:7).
Pia watoto ni kiburudisho cha
macho yetu. Amesema Mwenyezi Mungu:
“Ewe Mola wetu, tupe
katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu….”(25:74).
Na watoto ni pambo la maisha
katika ulimwengu huu: “Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani….” (18:16).
Mtume (s.a.w.) anatudhihirishia
ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: “Watoto ni vipepeo vya
Peponi.”
Kuwatunza watoto ni jambo la
lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume (s.a.w.)
amesema: “Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali)
na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.”
Inaonyesha wazi kwamba huruma na
uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia
adhabu juu ya watu wake.
1. Mapenzi Ya Mtume Kwa Watoto
Mapenzi ya Mtume (s.a.w.) kwa
watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: “Siku moja
Mtume (s.a.w.) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan
na Husein (a.s.) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka
kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi
mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema: “Enyi watu, hakika mali zenu
na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu wangu wawili wakikimbia na
kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.”
Siku moja Mtume (s.a.w.) alikuwa
anaswali, mara Hasan na Husein (a.s.) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni
kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume (s.a.w.) akaendelea kusujudu tu.
Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposhuka wao wenyewe. Kisha alipotoa
salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba wake sababu zilizomfanya
asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu: “Wajukuu wangu wawili walikuwa
wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.”
Mtume (s.a.w.) alizoea
kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema: “Mimi huchukia
kumchosha mama yake.”
Siku moja alikuwa anapita
nyumbani kwa Fatima (a.s.) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein (a.s.)
akilia, aliingia ndani na baada ya kumkemea Fatima akasema: “Je hujui kwamba
nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka?”
Siku moja Mtume (s.a.w.)
alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume (s.a.w.) akiwabusu
wajukuu zake, Al-Akraa akasema: “Unawabusu watoto wa binti yako? Naapa kwa
Mungu nina watoto kumi, na sijawahi kumbusu hata mmoja.”
Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Je ni
kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.”
Comments
Post a Comment