MADHARA YA KUTOIELEWA DINI

MADHARA YA KUTOIELEWA DINI
Mara kwa mara tunasikia maneno mabaya yakisemwa wazi wazi, ili kuipinga “Dini”. Maneno haya yanatumiwa sana siku hizi, na Makomyunist. Maneno hayo ni:
 i. Dini inapinga sayansi
ii. Dini ni dawa iliyogunduliwa na mabeparili kuwatuliza watu wa tabaka linalodhulumiwa, na kuwafanya watosheke na hali yao hiyo ya kimaskini; kwa usemi mwingine dini ilikuwa  kasumba ya kuwalazia watu.
iii. Dini hupunguza maendeleo ya kimwili na kiakili.
Basi hebu ngoja tuzichunguze hoja hizi. Habari hizi hizi  zimesemwa na Wazungu wengi (toka Karl Marx hadi Bertrand Russel) ambao walikuwa na ujuzi wa dini moja tu, nayo ni Ukristo; hakika wametenda dhambi kubwa ya kiakili, kwa kuona dini fulani, na kudhania kuwa dini zote (hata Uislamu) ni lazima ziwe na fikara hizo hizo.
Hakika kwa vyovyote vile maneno yao hayo kama si fikara  zilizotolewa kwa shabaha maalum, ni udanganyifu mtupu.
Ili kuueleza kinaga naga usemi huo hapo juu, inatulazimu kuieleza kwa muhtasari tu hali ya fikara za kikristo ilivyokuwa kuhusu ujuzi na maendeleo.
“Tangu karne ya kumi na sita ya baada ya Nabii Isa (a.s.),  ulitokea ugomvi kati ya Kanisa na sayansi. Ugomvi huu mbaya sana haukuanzwa na wanasayansi, ila ulianzwa na viongozi wa  kikrsto; ambao walihofu kuwa dini yao ilikuwa katika  hatari kubwa ya kupoteza nguvu zake miongoni mwa wakristo. Ngome ya mafundisho yao ilikuwa katika hatari ya kuanguka.
Madhehebu zote mbili (Wakatoliki na Maprotestanti) ingawa  zilikuwa zikigombana zenyewe kwa zenyewe, zilikuwa na  msimamo mmoja kuhusu mapambano baina ya mafundisho yao na njia za kimapinduzi za kisayansi, za Bwana Cupernicus, na mwenzie bwana Galileo. Walifanya kile kile ambacho kila  mdhalimu anayeogopa unyoge wake wa kiasili angeliweza  kukitenda. Mateso makali sana yalitolewa kwa wanasayansi washupavu waliolipinga Kanisa na ambao walisema kuwa kile wakijuacho kilikuwa ukweli mtupu.
“Kwanza hatuna budi tumchukue Bwana Cupernicus (Nicolaus Koppernigk) aliyeishi kati ya mwaka 1473-1545, maana yeye  alikuwa ndiye aliyeanzisha jambo hilo. Bwana huyu kwa muda mrefu hakuthubutu hata kuchapisha kitabu chake kijulikanacho  kwa jina la On the Revolution of Heavenly Bodies (katika  mzunguko wa sayari za Angani) kwa ajili ya kuliogopa Kanisa. Mwishoni alifaulu kulituliza Kanisa kwa kukiandika kitabu hicho  kwa heshima ya Papa (afisa wa cheo cha juu sana wa Kanisa Katoliki).
Mchapishaji wa kitabu hiki aliandika utangulizi kuthibitisha kuwa maelezo juu ya mzunguko wa dunia ni jambo  linalokubaliwa tu, wala si jambo lililothibitishwa kabisa. Kwa  maneno ya Bwana Bertrand Russel, ‘Kwa muda fulani, mbinu hizi zilitosha, na ni kutokana na wito wa kijasiri wa Bwana Galileo (wa kuwaita wana dini kuja kushindana na Wanasayansi) ambao  ulileta shutma za wakati uliopita wa Bwana Cupernicus’.” (rejea katika kitabu kiitwacho Religion and Science).
“Bwana Luther pia, aliupinga ‘utaratibu’ wa Bwana Cupernicus kwa kutumia njia za Kitheolojia (za kiujuzi wa Sifa na Tabia za Mwenyezi Mungu).
“Mwanasayansi mwingine, Bwana Galileo Galilei aliyeishi kati ya mwaka 1564-1642 Masihiyya, ingawa alikuwa rafiki wa Papa  Urban VIII, alitiwa katika jela ya Mahakama ya kuhukumu kesi za wazushi wa mambo ya kidini, kwa amri ya Papa huyo huyo na kutishiwa atapata mateso makali kama hataacha mafundisho yake hayo. Makosa ya Galileo yalikuwa kuunga mkono mafundisho ya Copernicus kutokana na uchunguzi alioufanya kwa darubini yake. Kwa upande wa Kanisa, uchunguzi huu ulikuwa mgumu  zaidi kupambana nao, kuliko ile elimu ya kimaandishi tu ya  Bwana Copernicus.
“Mwana Sayansi mwingine Bwana Giardino Bruno aliyeishi kati ya mwaka 1549-1600 Masihiyya, alikuwa madhabuha mwingine wa ukatili uliotendewa wanasayansi. Bwana huyu alichomwa hali ya kuwa yu hai.
“Bwana Bertrand Russel, ameandika katika kitabu chake  kiitwacho Religion and Science hivi: ‘Wataalamu wa Elimu  Lahuuti hawakuchelewa kusema kuwa, mafundisho hayo mapya yatafanya yale mafundisho ya kuchukua umbo la kiutu  (incarnation, kwa mfano Yesu kuwa ni Mungu aliyegeuka katika umbo la Binaadamu) kuwa ni vigumu kuaminika’.” (rejea katika kitabu kiitwacho Religion and Science).
“Hivyo mahakama ya hukumu za wazushi wa Kidini, ilitangaza haya yafuatayo kuwa ndiyo ukweli. “Usemi wa kwanza, kuwa jua ndio kitovu (centre) cha Ulimwengu na kuwa jua haliizunguki  dunia ni wa kijinga, kipuuzi, usio kweli hata kidogo katika Elimu lahuuti na ambao ni uzushi mtupu, maana hauafikiani na  maandishi Matakatifu..... Usemi wa pili usemao kuwa dunia si  kitovu cha ulimwengu na kwa hiyo dunia ina lizunguka jua ni  upuuzi, ni uwongo katika elimu ya hekima (filosofia) na kwa upande wa elimu Lahuuti, kwa ujumla haitofautiani na imani  sahihi.” (rejea katika kitabu kiitwacho Religion and Science).
“Na kwa kuongezea zaidi, Kasisi wa shirika la Jesuit aliyeitwa Melchior Inchofer ilimbidi aongezee kusema wazo lihusulo  mzunguko wa dunia ni uzushi mtupu, lichukizalo zaidi, lenye madhara zaidi na lenye kuaibisha zaidi. Kutulia kwa dunia ni  kutakatifu mara tatu; hivyo basi hoja zipingazo maisha ya milele ya roho, kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na wa Mungu kuchukua  umbo la kiutu ni lazima zikubaliwe upesi kuliko hoja  zithibitishazo kuwa dunia inasogea. (rejea katika kitabu kiitwacho Religion and Science).
Kwa sababu ya kukabiliwa na dhuluma kali, Wanasayansi  waliueleza Ukristo, kuwa ni “imani isiyo pendelea mambo ya  kiakili na isiyopendelea mambo ya Kisayansi; ni ushirikina na ni kitu kirudishacho nyuma maendeleo ya binaadamu.”
Jambo la kustaajabisha ni kuwa wameichukulia kila dini kwa ujumla kuwa ni sawa na Ukristo. Kwa hakika Uislamu hauwezi kuwekwa  miongoni mwa dini ‘zisizoafikiana na sayansi, zisizo za kihoja,  au zisizoafikiana na maendeleo ya kibinaadamu.’

Ukweli ni kuwa Uislamu unaafikiana na sayansi katika mambo mengi kuliko ukristo na pia Uislamu unawahimiza waumini wake wafikiri kila hoja ijayo mbele yao na wasikubali kukubali hoja kibubusa.

Comments