AHLUL KISAA NI AKINA NANI?

AHLUL KISAA NI AKINA NANI?
MAANA YA AHLUL KISAA Neno “KISAA” lina maana ya nguo ya kujitanda au kujifunika; Kiswahili ni kishamaia au mharuma. Kutamka “KISAA” kwa fataha ya kafu. Maana yake ni ubora na Utukufu.
Kwa maana zote mbili hizo, neno hili ni sawa kwani hao ni watu wa kishamia, tena wenye mifano bora na yenye utukufu. Lakini makusudio yake mwenye mada hii ni watu wa kishamia.
Hadithi ya Kisaa (Watu wa Kishamia) ni mashuhuri sana, na imepokewa na masahaba wengi na maimamu wa hadithi. Mmoja katika maimamu ni Imamu Muslim, mwenye kitabu chake cha hadithi, kiitwacho SAHIHI MUSLIM, yeye amesema: “Mtume (s.a.w.w.) aliwakaribisha (Imamu) Ali, Fatimah, Hassan na Hussein mwenye Kishamia. kisha akaisoma aya hii: (. . .INNAMA YUURIDULLAHU LIYUDH-HIBA ANKUMU-RRI- JSA-AAHLA-BAYTI WA YUT- WAHHIRAKUM TAT-HEERA.). Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, Enyi watu wa nyumbani, na kukutakaseni kabisa” (Sura Al-Ahzaab 33:33).
Vile vile Imamu Ahmad ameipokea hadithi hii kwa Sahaba Abu Said Al-Khudri kuwa iliteremka aya hii kwa ajili ya Watukufu hawa wanne, na Mwenyewe Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ni wa tano. Kwa hivyo, mshairi amesema:- “Kwanza ni Mtume, Ali na Al-Hasani. Kisha Husseini, mama yao ndiye wa mwishoni, Mkiwa na haja kuu mno, tawasalini kwa watano hao, hujibiwa dua kwa hima”
Kadhalika mwenye hadithi nyingine, Mtume (s.a.w.w.) baada ya kuisoma aya hii tuliyoitaja, aliongeza kusema: “Ewe Mola! Hawa ndio Ahlul Bait wangu khasa, waondolee uchafu na uwatakase kabisa-kabisa, umnusuru mwenye kuwanusuru hawa, na mpige vita mwenye kuwapiga vita hawa”.
Na hadithi nyingine tena mwenye Sahihi Muslim ambayo aliyeipokea ni Ummu Salamah, mke wa Mtume (s.a.w.w.) baada ya kuwakusanya Ali, Fatimah, Hassan na Hussein, akasema: “ewe Mola, hawa ndio ‘Ahlul-Bait’ wangu, waondolee uchafu”. Nikasema: Je na mimi ni pamoja nao ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mtume (s.a.w.w.) akanijibu: “kaa hapo hapo wewe ukatika kheri”.
Kwa hadithi hii ya Imamu Muslim iliyopokewa kutoka kwa mke wa Mtume (s.a.w.w.) na ya pili ni ile tuliyoitaja mwanzo iliyoeleza sababu ya kushuka Aya hii: yatuonyesha wazi kuwa “Ahlul-Kisaa” ndio “Ahlul-Bait”, nao ni hao niliowataja, watu wanne pamoja na Mwenyewe Mtume (s.a.w.w.) ni wa tano, na ingawa aya ya “Ahlul-Bait” imeambatanishwa na aya (WAQARNA FI BUYUTI KUNNA...) kama aya moja kwa maandishi lakini kipande cha mwisho kisemacho (INNA MAA YURIIDU-LLAHU LI YUDH’HIBA.....) Kwa mujibu wa riwaya zinazoeleza sababu ya kuteremka kwake zaeleza kipande cha hii aya: (INNA MAA YURIIDU-LLAHU....) kiliteremka kwa watu waliofunikwa Kishamia tu. Kisha Mtume (s.a.w.w.) aliwakusudia watu hawa na akawaombea Mungu, kama hadithi ya Ummu Salamah, mkewe Mtume (s.a.w.w.) ionyeshavyo, na nyiginezo kadha wa kadha.
Nayatilia nguvu maneno haya kwa kisa cha Wanaswara (Wakristo) wa Najran. Ujumbe wa Wakristo uliokwenda kumhoji Mtume (s.a.w.w.) kwa habari ya Nabii Issa kuwa si mja wa Mungu ni mtoto wa Mungu, hapo Mwenyezi Mungu akamteremshia Mtume (s.a.w.w.) Aya hii: (FAMAN HAAJAKA FIHI MIN BAADI MAJAAKA MINAL- ILMI FAQUL TAALAU NAD-U ABNAANA WA-ABNAAKUM WANI-SAANA WANISAAKUM WA ANFUSANA WA ANFUSA- KUM THUMMA NAB-TAHIL FANAJ- AL-LAANATALLAHI ALAL KA- DHIBIIN)
“Mwenye kujadiliana (kushindana) nawe katika hilo (la Nabii Issa) baada ya kukujia elimu (ujuzi kuwa Issa ni mja wa Mungu. Si mtoto wake), basi sema: Njooni! tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na nafsi zetu na nafsi zenu (watu wetu na wenu); kisha tuombe kwa unyenyekevu na kuiweka “laana” (mateso) ya Mwenyezi Mungu juu ya waongo”. (Sura Aali-Imran 3:61).
Hapo tena Mtume (s.a.w.w.) akatoka yeye na wajukuu zake (“ndio maana ya watoto wetu”) yaani Hassan na Hussein, akatoka na binti yake Bibi Fatimah (ndiyo maana ya “wanawake zetu”), akamchukua pamoja na hao Imamu Ali (ndiyo maana ya “nafsi zetu”); akatoka Mtume (s.a.w.w.) pamoja na watu wanne hao tu, akaenda nao mpaka mbele ya hao Wakristo, akawaambia “Mimi ninaomba Dua na ninyi itikieni (Amin)”; lakini wapi, ukweli ukifika uwongo hujitenga; Nani anathubutu kupambana na watu hawa kwa kuapizana! Wakaogopa, Walikatazwa na mkubwa wao, Aliwaambia: “Hawajaapizana kaumu yoyote na Mtume ila kuangamia (hupotea wakafikiwa na mabalaa).” Hapo tena wakafanya sulhu kwa kutoa jiziya (kodi) kuwapa Waislamu. Hadithi hii imepokewa na Imamu wa hadithi, bwana Abu Nuaim.
Tumeona kuwa Aya ya Qur’an imetaja “wake” na Mtume (s.a.w.w.) hakutoka na mke yeyote miongoni mwa wake zake wala mwanamke yeyote ila alitoka na Bibi Fatimah peke yake; kadhalika Aya imetaja “watoto” na Mtume (s.a.w.w.) hakutoka na kijana wa jamaa yake wala wa yeyote bali alitoka na wajukuu zake Hassan na Hussein.
Basi mabwana wanne hawa, Ali na mkewe na watoto wao, ndio alioamrisha Mtume (s.a.w.w.) wapendwe kwa hadithi nyingi za Mtume (s.a.w.w.), na katika Qur’an ni ile aya niliyoitaja mwanzo. Aya kamili, na maana yake nimekwisha kuieleza.
Na makusudio yake kuteremshwa aya hii ni kwa ajili ya watu wanne hawa, kwa dalili waliyoipokea maimamu hawa: Imamu Ahmad, Tabrani na Hakim: wote wameipokea hadithi hii kutoka kwa bwana Abdullah bin Abass (R.A.), yeye amesema ilipoteremka aya hii, Masahaba walimuuliza Mtume (s.a.w.w.) wakasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani hao walio karibu zake wapasikao juu yetu kuwapenda”. Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Ni Ali, Fatimah na watoto wao (Hassan na Hussein)”.
Na walio karibu na Mtume (s.a.w.w.) yaani jamaa zake ni wengi, ni Banu Hashim wote, hata na Makureish wote. Na wote hao Mtume (s.a.w.w.) aliamrisha wapendwe kwa hadithi nyingi alizozisema juu ya watu hao, lakini walio bora kuliko wote na aliowasisitiza sana Mtume (s.a.w.w.) wapendwe ni hawa watu wanne.

Comments