JE IMAM HUSSEIN NI KIONGOZI WA MAWAHHABI AU MASHIA?
Kwanza tufikirie ni madhahebu ipi yenye kumtukuza yule mtu
Mtukufu ambaye yu Shahidi wa Karbala na inayozifuata nyayo zake, na ni ipi
isiofanya hivyo. Bila ya kusema mengi, ni madhehebu ya Shia yenye kumwamini
Imamu Husayn (a.s.) kuwa yu mtu aliyeteuliwa na aliyewekwa na Allah (s.w.t.) na
yu mrithi wa haki wa nafasi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Shia wanaamini kwamba
kila neno na kitendo cha Imamu (a.s.) ni katika kumtii Allah, vita yake na
amani yake ni kioo cha amali chenye kufaa, na msimamo wake ndio mapenzi ya Allah.
Kwa Shia, Imamu ni sehemu ya Nuru (Nuur) ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.),
Nyama na damu ya Imamu ni nyama na damu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kujitoa
kwa ajili ya Imamu ni jukumu kuu. Kumtii kuna maana ya kuikamilisha imani yake
mtu, na kwanza yeye Imamu katakasika kutokana na kukosea na makosa.
Kumpenda Imamu ni kutimiza malipo ya Utume wa Mtukufu Mtume
(s.a.w.w.). Allah (s.w.t.) anasema: "...Sema (ewe Rasuli Wetu Muhammad):
kwa hayo, siombi ujira wowote kwenu ila mapenzi (yenu) kwa karibu (zangu)..."(Qur'ani,
42:23). Imamu katakasika kutokana na kila aina ya uchafu, uwe wa kimwili au wa
kiroho.
Allah (s.w.t.) anasema: "...Hakika Allah anataka
kukuondoleeni uchafu, enyi Ahlul Bayt (wa Rasuli Wetu Muhammad) na
kukutoharisheni kwa tohara kamili." (Qur'ani 33:33). Imamu yu mwana wa
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).
Allah (s.w.t.) anasema: "...Lakini atakayekuhoji
kuhusiana na hayo baada ya kukufikia elimu, basi sema: "Njooni tuwaite
wana wetu na wana wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu na nafsi zetu na
nafsi zenu..."(Qur'ani 3:61).
Imamu yu ua la Mtukufu Mtume
(s.a.w.w) na anatokana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w), kama alivyosema Mtukufu
Mtume (s.a.w.w) mwenyewe, pale aliposema: "Husayn anatokana na mimi, na
mimi ninatokana na Husayn." Imamat (Uimamu) wake hautegemeani na upatano
wa watu wala kiapo cha utii cha watu. "Yeye yu kiongozi wa vijana wa
Peponi." Yu mtakatifu (kutokana na dhambi na kukosea) tangu kuzaliwa kwake
hadi kufariki dunia kwake. Itikadi hii juu ya Umaasum (Utakatifu wa Maimamu) ni
maalumu kwa Mashia tu, na wasiokuwa Mashia hawashiriki kwenye itikadi hii.
(Ingawa wanavyuoni wakuu wasio Shia wanaweza kuthibitisha Uma'sum wa Maimamu).
Comments
Post a Comment