MAJIBU KWA WANAOPINGA KUOA WAKE WENGI

MAJIBU KWA WANAOPINGA KUOA WAKE WENGI
Upinzani wa wasiokuwa waislamu juu ya jambo hili kwa hakika unachusha.  Wanapenda kulaumu bila kujali ubora wa jambo lenyewe ila tu kwa kuwa wao wenyewe hawanalo  jambo hili kwa ajili ya kuharibiwa na watangulizi wao. 

Padre Dale anasema.  Wakristo hawawezi kuiamini Qur'an kwa kuwa  Vitabu vyao havipatani na Qur'an (uk. 583). Sisi tunauliza, Je, Ukristo unapatana na mafundisho ya Agano la Kale? Mbona wanaamini Agano la Kale pia?  Katika shauri la vyakula, ibada na hukumu nyingine za dini, Ukristo ni mbali na Agano la Kale, lakini juu ya kuhitilafiana hivyo, wanaamini Agano la Kale pia.

Kadhalika Padre Dale anasema. "Mkristo hapewi ruhusa katika Injili kuwa na wake wawili, sembuse wanne" (uk 569).  Lakini Injili inasema, Yesu alisema, "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.  Kwa maana, amin, nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya Torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni (Matt. 5:17-20). 

Tena Yesu akasema "Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa;  basi yo yote watakayowaambia myashike na kuyatenda" (Matt. 23:2).

Je Torati iliharimisha kuoa wake zaidi? Torati inasema,  Akiwa mtu ana wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia vijana . . . na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa; ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, na asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda," (Kumbukumbu 21:15-17). 


Pia soma Kumbukumbu la Torati  (25:5).  Je, maneno hayo hayaonyeshi kuwa kuoa zaidi hakulaumiwi?  Ni wazi Wakristo wanapinga maneno ya Yesu aliyewaambia wafuate amri zote  za Torati na maneno ya Manabii na  ya Mashekhe wa Kiyahudi.

Comments