MUHAMMAD (S.A.W.W) MTUME WA ALLAH: KUZALIWA MPAKA UTU UZIMA

MUHAMMAD (S.A.W.W) MTUME WA ALLAH: KUZALIWA MPAKA UTU UZIMA
Muhammad al-Mustafa, Mtume wa mwisho wa Allah, alizaliwa Makkah, Arabia mnamo mwezi 17 Rabi al-Awaal, mwaka wa kwanza wa tembo (Amul Fiil) 570 A.D.
Mtume Muhammad (s.a.w.) alizaliwa katika ukoo wa Bani Hashim, wa kabila la Quraishi, ambao walikuwa ndio walioheshimiwa sana katika familia za Kiarabu. Bani Hashim walikuwa ni kizazi cha Ismail, mwana wa Nabii Ibrahim.
Babu yake Mtukufu Mtume, Mzee Abdul Muttalib alikuwa ndiye Mkuu wa Bani Hashim na vile vile alikuwa ndio mlezi wa al- Kaaba. Baba yake yeye Mtume, alikuwa anaitwa Abdullah na mama yake aliitwa Amina. Baba yake alifariki miezi michache kabla ya kuzaliwa kwake. Akiwa na umri wa miaka sita, Mtume akampoteza mama yake pia na yeye akawekwa chini ya uangalizi wa babu yake, Abdul Muttalib. Lakini babu yake naye akafariki baada ya miaka minne; na safari hii, ami yake Mtume, Abu Talib alichukua dhima juu yake na akawa mlezi wake, akimchukua kuishi naye nyumbani kwake mwenyewe. Hivyo Mtukufu Mtume (s.a.w.) kwa kiasi kikubwa alikulia nyumbani kwa ami yake na hata kabla ya kufikia umri wa balehe alikuwa akifuatana na ami yake kwenye safari za kibiashara kwa misafara.
Mtukufu Mtume hakuenda shule yoyote, hata hivyo, baada ya kufikia umri wa utu uzima alikuwa maarufu kwa hekima zake, ushauri, uaminifu na ukweli wake. Mara akawa anajulikana kama “As-sadiq al-amin” – Mkweli, Mwaminifu. Ami yake, Abu Talib alikuwa kila mara akisema “Hatujasikia uwongo wowote kutoka kwa Muhammad, wala kuwa na tabia mbaya au kufanya uharibifu. Kamwe hacheki ovyo ovyo wala kuzungumza wakati usiofaa.”
Kwa matokeo ya busara na uaminifu wake, Khadija bint Khuwaylid, bibi wa kikuraishi maarufu kwa utajiri wake, akamteua yeye kama meneja wa biashara zake na akaacha jukumu la kuendesha shughuli zake za kichuuzi mikononi mwake. Mtume, safari moja alikwenda Damascus na bidhaa za Khadija na kutokana na uwezo wake akatengeneza faida kubwa ya kuvutia. Haukupita muda mrefu yeye Khadija akamuomba awe mke wake naye Mtume akalikubali ombi lake hilo. Baada ya ndoa yao, akiwa na umri wa miaka ishirini na tano, Mtukufu Mtume akaanza maisha ya kuwa meneja wa mali za mke wake. Alipofikia umri wa miaka arobaini, alijipatia sifa njema ya kuheshimika iliyoenea sana kwa sababu ya busara na uaminifu wake.
Alikataa kuabudu masanamu, kama ilivyokuwa ndio desturi ya kidini ya Waarabu wa wakati huo. Mara kwa mara alifanya faragha za kiroho kwenye pango la Hira nje kidogo ya Makkah, ambamo alifanya maombi na kuzungumza kwa siri na Allah.

Comments