VITA VYA JAMAL AU VITA VYA BASRA

VITA VYA JAMAL AU VITA VYA BASRA
Hii ni vita ya pili ya waislamu kwa waislamu yaani wenyewe kwa wenyewe. Vita ya kwanza iliendeshwa na Abubakar bin Quhafa pale alipotuma jeshi chini ya uamiri wa Khalid bin Walid kwenda kuwateketeza waislamu waliogoma kutoa zaka ikiwa ni mbinu ya kuugomea uongozi wake batili. Matajili hawa walifahamu wazi kuwa khalifa wa kwanza aliyetangazwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni imam Ally bin Abi Talib (a.s). Khalid bin Walid waliwafyeka wote waliogoma kutoa zaka.

Mama yetu Aisha (R.A) alikuwa akirejea Madina akitoka Hijjah aliposikia taarifa ya kuuawa Uthuman bin Affan na pia taarifa za ukhalifa wa Imam Ally. Kwanza aliamua kurudi Makkah na kufanya mkutano na watu kadhaa ili kuunda jeshi la kumpiga vita imam Ally (a.s). alifanya mkutano na kundi kubwa la maadui wa imam Ally akiwemo Zubeir, Twalha na bani Umayya ambao wamekuwa na uadui wa jadi dhidi ya ukoo wa Mtume yaani Bani Hashim. Ukoo huu ndio ulioongoza mateso na mauaji dhidi ya Ahlulbayt wa Mtume na mti uliolaaniwa katika Qur’an.

Kikao hiki kiliamua kupeleka jeshi kupambana na imam Ally na wafuasi wake kwa madai ya kuwa wanalipiza kisasi dhidi ya mauaji ya Uthuman bin Affan. Walikusanya askari 30,000 na kuelekea Basra na kuuteka mji huo ili kuufanya kuwa ngome yao katika kumshambulia Imam Ally (a.s) na jeshi lake. Walifanikiwa kuuteka mji huu lakini hawakufanikiwa kuwashawishi wenyeji wa mji huu kushirikiana nao katika vita vyao dhidi ya Khalifa Imam Ally (a.s), hivyo wakawaua waislamu 600. Hii ni pamoja na kumteka gavana wa mji huu Uthuman bin Hunaif akiwa msikitini na kuwaua waumini 40 waliokuwa waswali.

Hii ilikuwa ni mbinu ya kuficha ukweli kwani waliamini kuwa imam Ally ni Mtu wa haki na angefanya uchunguzi dhidi ya mauaji yale kwa hiyo wakaona kuwa ili kuwaficha wauaji ambao walikuwa miongoni mwao ni lazima waanzishe vita dhidi ya imam Ally na kumshughulisha vita ili asahabu kumtafuta muuaji halisi wa Uthuman.

Bani Umayya ni kabila la Uthuman, walishirikishwa katika vita hii kwa sababu kwanza aliyeuawa ni ndugu yao lakini wao wanajulikana kwa uadui wao dhidi ya Mtume na Ahlulbayt wake na hivyo walifahamu fika kuwa Bani Umayyah hawatosita kushiriki vita dhidi ya Imam Ally (a.s).

Ukweli ni kuwa kama ukhalifa usingechukuliwa na imam Ally, vita hiyo isingetokea. Walimpiga vita imam Ally na serikali yake kwa sababu ya chuki zao dhidi ya Ahlulbayt. Na lengo hasa la bi Aisha ni kuweka khalifa mpya, Abdullah bin Zubeir, mwipwa wake na mwanae wa kupangwa.

Magavana mafisadi waliotolewa madarakani na imam Ally (a.s) yaani Abdullah bin Amir wa Makkah, Ya’la bin Umayya wa Yemen na Abdullah bin Kuraiz wa Basra, waliungana na jeshi hilo la wanafiki.
Mughira bin Shuba aliwashauri kuwa kule wanakokwenda hakuna wauaji wa Uthuman, wauaji halisi na majenerali wao waliopo katika jeshi hilo na lengo lao ni kupata ukhalifa basi. Jeshi hili haramu lilipinga na kusonga mbele.

Baadaye alifika eneo liitwalo Hauab, mbwa wakamzunguka bi Aisha na kumbwekea sana. Aisha alihamanika sana akauliza ni eneo gani hilo? Wenyeji wa hapo wakamjibu kuwa eneo hilo ni Hauab. Hapo ndipo alipohamanika zaidi na kukumbuka hadith ya Mtume iliyomlaani mke wake atakayebwekewa na mbwa wa Hauab. Akaagiza arudishwe Makkah lakini watu wake wakatafuta mashahidi 50 wa uongo ili wamdanganye kuwa eneo hilo si Hauab. Wakafanikiwa kwa hilo hivyo wakaendelea na safari zao za Shari.

Imam Ally aliposikia habari hii aliandaa jeshi la askari 6000 na kuelekea Basra ili kukabiliana na jeshi hilo la waasi. Kwanza aliwatumia barua ya kuwasihi waache uasi. Watu hawa walipinga na kusonga mbele.

Ndipo imam Ally (a.s) alipoamua kukabiliana na waasi hao na kuwashinda kwa muda mfupi sana. Vita hii iligharimu maisha ya waislamu zaidi ya elfu kumi akiwemo Twalha.
Vita ilimalizika kwa kukamatwa bi Aisha na mateka wengine kutoka upande wa wanafiki. Imam Ally akawasamehe na bi Aisha kukabishiwa kwa kaka yake Muhammad bin Abubakar aliyekuwa Mshia maarufu na alipigana vita ile akiwa upande wa imam Ally na sio dada yake.


Tunajifunza hapa kuwa tuwe makini tunapofanya maamuzi kwani taarifa nyingi tuzipatazo zinaweza kupelekea vita na umwagikaji wa damu za watu wasiokuwa na hatia kama walivyo fanya Aisha na jeshi lake.

Comments