UMUHIMU WA KUJUA
HISTORIA YA UISLAMU
Hamna shaka kuwa
historia ya mwanadamu ndio chemchemu na chanzo cha maarifa, chanzo ambacho
mataifa yanakihitaji katika safari yake yenye kuendelea. Na ndio chanzo pekee
chenye uwezo wa kuhuisha na kulisukuma taifa mbele na kulipa sifa na hadhi
maalum huku kikilifunganisha taifa hilo na mizizi yake ya ustaarabu ambayo
hulizuwia taifa dhidi ya mmong'onyoko. Kwa masharti kuwa watu waisome historia
na kupata mazingatio ndani yake kisha waidadavue na kuitumia kulingana na mahitaji
ya jamii husika kwa zama husika.
Qur'ani imemhimiza kila
mwanadamu ikamtaka azame ndani ya historia ya mwanadamu na azingatie yaliyomo
ili awaidhike na kuongoka, hivyo Mwenyezi Mungu akasema: "Je, hawatembei
katika ardhi ili wapate nyoyo za kufahamia au masikio ya kusikilizia?"1
Baada ya Mwenyezi Mungu
kutoa historia ya Adi, Thamudi, Firauni, watu wa miji iliyopinduliwa na watu wa
Nuh akasema: "Ili tuifanye ukumbusho kwenu na sikio lisikialo
lisikie."
Historia ya ujumbe
mbalimbali wa Mwenyezi Mungu imejaa masomo na mazingatio, masomo ambayo yameonyesha
jinsi manabii watukufu walivyojali mataifa yao ili kuyaokoa toka kwenye
matatizo mbalimbali. Pia ujumbe huo umeonyesha lengo na mwelekeo wake wenye
kujaa nuru na manufaa.
Kwa ajili hiyo sira ya
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kizazi chake huwa ni tafsiri ya kivitendo ya
misingi na sheria za kiislamu.
Hivyo kusoma sira yao
na historia ya maisha yao ni chanzo muhimu cha kuifahamu Qur'ani na Sunna, na
ni chemchemu ya maarifa ya wanadamu wote, kwa sababu ni ujumbe wa Mwenyezi
Mungu alioutuma kwa wanadamu huku Nabii wa mwisho na mawasii wake wateule
wakiwa ni viongozi wa wanadamu wote bila kubagua.
Comments
Post a Comment