ATABITA SIRATI, MTU ATAKAYEIDHINISHWA NA IMAM ALLY TU
Hakuna atakayepita Sirati ila tu yule mwenye kuidhiniwa na imam Ali (a.s) kupita.
Mwanazuoni wa kisunni, Ibn Hajar al-Haitami ash-Shafii katika kitabu chake cha As-Sawaiq al-Muhriqah (uk. 78/97) ameeleza hadithi kutoka kwa Ibn Saman kuwa Abu Bakr amesema, “Nimemsikia Mtume (s.a.w.w.) akisema, ‘Hakuna atakayepita Sirati (njia ya kuendea Peponi) ila tu yule aliyeidhiniwa na Ali kupita’”.
Vile vile katika kitabu cha Sunan Ad-Daraqutni imeelezwa hadithi inayosema hivi: Ali aliwauliza wale watu sita waliowekwa na Umar kushauriana mambo ya Ukhalifa ‘kama kuna anayeweza kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kama kuna yeyote miongoni mwao aliyeambiwa na Mtume (s.a.w.w.) maneno haya, “Ewe Ali, wewe ndiye mgawaji wa Pepo na Moto siku ya Qiyama”. Kama si mimi basi ni nani?’ Wakasema, “Bila shaka ni wewe tu”.
Maneno hayo yanatokana na hadithi iliyoelezwa na Antara ambaye aliipokea kutoka kwa imam Ali al-Ridha (a.s) ambaye amepokea kutoka kwa baba zake kwamba Mtume (s.a.w.w.) amesema, “Ewe Ali hakika wewe ni mgawaji wa Pepo na Moto. Siku ya Qiyama, utauambia moto: ‘Huyu wangu na huyu wako’”.
Na katika kitabu cha Manaqib cha al-Khawarizmi1 imetajwa hadithi ya Antara kuwa Mtume (s.a.w.w.) amesema, “Ewe Ali hakika wewe ni mgawaji wa Pepo na Moto na wewe ndiye utakayengoja mlango wa Pepo na kuingia ndani bila ya hisabu”.
Katika kitabu cha Dhakhair al-Uqba cha Tabari ash-Shafii2 imeelezwa hadithi ya kumsifu Ali (a.s.) kuwa kwa hakika hapiti yeyote katika sirati ila yule aliyeidhiniwa na Ali kupita.
Imepokewa hadithi kutoka kwa Qais bin Hatim ya kwamba walikutana mabwana Abu Bakr na Ali bin Abi Talib (a.s.). Abu Bakr akafurahi kumwona Ali (a.s.) na Ali akamwuliza amefurahia nini? Abu Bakr akamjibu:
“Nimemsikia Mtume (s.a.w.w.) akisema: Hapiti yeyote katika sirati ila yule aliyeidhiniwa na Ali kupita”. Pia amesema kuwa amenakili hadithi Ibn Saman katika kitabu al-Muwafaqah na katika Manaqib cha al-Khawarizmi3 na vile vile katika kitabu chake maarufu kiitwacho Maqtal al-Husain4 hadithi hiyo ilipokewa kutoka kwa Hasan al-Basri ambaye alipokea kutoka kwa Abdallah, kuwa amesema Mtume (s.a.w.w.): “Siku ya Qiyama Ali bin Talib atakaa juu ya Firdausi (mlima ulio juu ya Pepo), na juu yake kuna Arshi ya Mola wa viumbe, na pembezoni mwa jabali ikiteremka mito ya Peponi na yatawanyika katika Pepo mbali mbali na yeye (Ali) amekaa katika kiti cha nuru, na mito yapita mbele yake iitwayo at-Tasneem, basi hapiti yeyote katika sirati ila awe nayo hati ya utii kwake na Ahlul Bayt zake. Ataangalia Ali, atamtia ampendaye Peponi, na amchukiaye Motoni.”
Ibrahim bin Muhammad al-Hamawayni ash-Shafii katika Faraid us-Simtain5 na Muhibuddin at-Tabari katika al-Riyadh al-Nadhirah6 pia wameeleza hadithi hiyo. Kadhalika Hakim katika Al-Arbaeen pia amepokea hadithi hiyo.
Ibn Abi Adsa katika historia amepokea hadithi hii hivi: Abu Bakr alimwambia Ali, “Nimemsikia Mtume (s.a.w.w.) akisema kuwa yeyote hapiti katika sirati ila tu yule aliyeruhusiwa na Ali kupita”.
Sulaiman al-Hanafi katika kitabu chake cha Yanabi al-Muwaddah7, Ibn al-Maghazili ash-Shafii katika Manaqib na Ghayat al-Maram na katika Tarikh Baghdad cha al-Khatib al-Baghdad8, hadithi hiyo imesimuliwa kutokana na Ibn Abbas. Vile vile Qadhi Ayadh ameeleza katika kitabu chake cha Shifaa, Allama Sayyid Abu Bakr Shahabuddeen Shafii katika kitabu chake cha Rishfat-us-Saadi min Bahril Fadail Bani al-Hadi9, Qurashi katika Shamsul Akbar10, Sheikh Abdallah Shabrawi Shafii katika al-Ittihaf bi hubbil Ashraf11 na Shaykh Muhammad Sabban katika Isafur Raghibeen12.
Kurasa za rejea hizo
1 Mlango 19, uk. 234
2 uk. 17,
3 uk. 222,
4 Juzu 1, uk. 39,
5 Juzu 1, Mlango 54,
6 Juzu 2, uk. 173, 177 na 244,
7 uk. 95, chapa ya Iraq,
8 Juz 3, uk. 161
9 uk. 459
10 uk. 36
11 uk. 15
12 uk. 161
Basi hadithi hiyo wamehadithia kikundi kikubwa cha Masahaba licha ya Abu Bakr, Ibn Abbas, Ibn Masood na Anas bin Malik. Hawa wote ni masahaba wakubwa na miongoni mwao walikuwa wapinzani wake, lakini ukweli haufichiki bado walieleza ukweli kuhusu Imam Ally katika kadhia hii. Alhamdulillah
Comments
Post a Comment