IMAM ALLY (A.S) AITOA NAFSI YAKE KUMWOKOA MTUME

IMAM ALLY (A.S) AITOA NAFSI YAKE KUMWOKOA MTUME

Ameeleza Qadhi Husain Ibn Muhammad Diyar Bakari al-Maliki katika kitabu chake Tareekh-e-Khamees kuwa walipoafikiana makafiri wa Kikureshi kumuua Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na wakaizunguka nyumba yake ili kumuua, akaja Jibril (Malaika mletaji Wahyi) kwa Mtume na akampasha habari juu ya hila zao na akamtaka asilale kitandani mwake bali atoke na aende Madina.

Ibn Athir al-Jazari ameandika katika kitabu chake Tarikh al- Kamil kwamba ilipoingia giza ya usiku, makafiri wakiqureshi walikusanyika mlangoni mwa Mtume kwa kusudi la kuvizia atapolala kitandani mwake tu wamshambulie na kumuua. Mtume akaona mkutano nje na akamwamrisha Ali Ibn Abi Talib, “Lala kitandani mwangu na ujifunike toka kichwani mpaka miguuni kwa shuka langu la kijani. Kuwa na hakika hayatakufikia madhara yeyote.
Vile vile alimwamuru Ali awakabidhi wenye amana zao walizoziweka kwake (Mtume). Kumbuka Mtume alikuwa kama benki kwa wakazi ya Makah. Hapo Mtume akatoka nje ya nyumba yake huku anasoma aya za mwanzo wa Sura Yaseen (Sura 36) mpaka aya “Fa Hum La Yubsirun” na akawarushia vichwani mwa makafiri wakiqureshi ukofi mmoja wa mchanga, na akashika njia ya Madina na Maqureshi wasimwone.
Jalaluddin akaendelea na kisa hiki katika Tafsir Durr-e-Manthur kwa ushahidi madhubuti unaotokana na Ibn Abbas kwamba Ali Ibn Abi Talib alijifidia roho (maisha) yake juu ya Mtume na akalala kitandani mwake na kujifunika kwa shuka la Mtume. Wakati wote huo mpaka asubuhi Maqureshi walioizunguka nyumba wakifikiria kwamba Mtume alilala na wakifanya mipango ya kumuua Mtume.

Katika Usdul Ghabah cha Ibn Athir al-Jazari na Ihya-ul-Uloom cha Ghazali na Tareekh-e-Khamees cha Qadhi Husain Ibn Muhammad Diyar Bakari al-Maliki imeelezwa kwamba alipolala Ali kitandani mwa Mtume, Mwenyezi Mungu aliwaambia kwa (Wahyi) Jibril na Mikaeel (Malaika watukufu), “Nimefanyiza udugu kati yenu wawili na nimejalia umri wa mmoja katika nyie kuwa zaidi kuliko mwenziwe. Kwa kufanya hivyo nani mmojawapo yu tayari kufidia maisha yake kwa nduguye?”

Waliposikia hayo kwa Mwenyezi Mungu, wote wawili wakakataa kumfidia maisha juu ya mwenziwe. Ndipo Mwenyezi Mungu akawaambia, “Je, hamwezi kuwa kama Ali Ibn Abi Talib? Tazameni mimi nimefanyiza udugu kati ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Ali, na sasa Ali, amelala kitandani mwa Muhammad (s.a.w.w.) kwa kutaka kumfidia maisha yake kwa kuwa ndugu yake. Basi sasa nyinyi wote wawili teremkeni kwenye ardhi na nendeni mkamlinde Ali na maafa ya Makuraishi”.
Hapo watukufu hawa wawili wakimalaika wakateremka na kila mmoja akashika mahala pake, Jibril kwenye kichwa cha Ali na Mikail kwenye miguu ya Ali. Jibril akanena, “Salaam na pongezi kwako. Nani kama wewe Ee mtoto wa Abu Talib! Ambaye Mwenyezi Mungu anafanya fahari (kwa kitendo chako) juu ya malaika?” na alipokuwa Mtume yupo njiani kwenda Madina, Mwenyezi Mungu akamteremshia aya zifuatazo katika kumsifu Ali: “Wa Min-An-Nasi Man-Yashri Nafsahubtighaa Mardhatil-Laahi Wallahu Raoofun Bil-Ibaad”. (Na katika watu wauzao nafsi zao kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa watumwa wake) (Sura al-Baqara aya 207)

Huyu ndiye Imam Ally (a.s) ambaye Mungu alimfanya.
1. ndugu wa Mtume
2. khalifa wa kwanza wa Mtume kwa waislamu wote
3. imam wa kwanza wa Mtume kwa waislamu wote
4. kamanda wa majeshi ya kiislamu asiyeshindika
5. mwenye elimu kuliko masahaba wote
6. mcha Mungu kuliko masahaba wote.

Ni vyema tumfuate imam Ally na kumfanya kuwa kiongozi wetu baada tu ya Mtume. Kumfuata asiyekuwa imam Ally ni sawa na kujiangamiza mwenyewe.

Comments