MAISHA YA MWANZO YA BI KHADIJA (A.S).

MAISHA YA MWANZO YA BI KHADIJA (A.S).
Mama wa waumini, Khadija bint Khuwalid alizaliwa Makka. Alikuwa mtoto wa kike wa Khuwaylid bin Asad bin Abdul Uzza bin Qusayy. Qusayy alikuwa babu aliyejulikana sana kwenye ukoo wa Khadija vile vile kwenye ukoo wa Mtume Muhammad Mustafa, wa uzao wa Bani Hashim, aliyekuja kuwa Mtume wa Uislamu (S.a.w.).

Kwa hiyo Khadija alitokana na nasaba yenye asili moja na Bani Hashim. Baada ya Bani Hashim, familia yake ilikuwa tukufu na yenye kuheshimika sana Arabuni pote. Familia ya Khadija haikuwa mashuhuri kwa utajiri tu bali pia kwa ubora wa tabia yake.

Khuwaylid, baba wa Khadija pia alikuwa mfanyabiashara kama wenzake wengine wengi wa kabila la Quraysh wa Makka. Kama walivyokuwa wafanyabiashara wa kabila la Qurayshi wengi, baba yake Khadija naye alipata mafanikio ya utajiri kutokana na biashara ya nje. Wafanyabiashara wa Makka walituma misafara miwili kila mwaka mmoja wakati wa kiangazi ambao ulikwenda Syria na mwingine wakati wa kipupwe ambao ulipelekwa Yemen.

Misafara hii ya kibiashara ilibeba mazao ya jangwani na bidhaa zilizo tengenezwa Makka na sehemu za jirani yake na ziliuzwa kwenye masoko ya Syria na Yemen. Aidha waliuza farasi-chotara Syria. Aina hii ya farasi ilithaminiwa sana Syria na nchi jirani. Baada ya kuuza bidhaa zao na farasi-chotara wao, wafanyabiashara hao walileta nafaka, mafuta ya zeituni, matunda, kahawa, nguo, bidhaa za anasa na vitu vingine vilivyotengenezwa kwa ajili ya kuviuza Makka. Hivyo walipata faida Syria, Yemen na Makka. (Biashara hii ya Makka imetajwa kwenye Qur'ani takatifu, Sura ya 106). Biashara ya nje ilikuwa ndio msingi mkubwa wa uchumi wa Makka.

Makka ilikuwa haina ardhi ya kilimo wala maji ya kilimo cha umwagiliaji. Watu wa Makka, katika hali hiyo, hawakuweza kulima mazao ya chakula. Walitegemea biashara baina yao na Syria na Yemen ili wajilishe. Kutokana na faida waliyopata walinunua nafaka na vitu vingine muhimu katika maisha.

Kila msafara ulikuwa na kiongozi. Kiongozi huyu alitakiwa kuwa mtu mwenye sifa zisizo za kawaida. Usalama na kufaulu kwa msafara katika biashara ya mauzo na manunuzi, ilitegemea sana maamuzi ya kiongozi. Kiongozi alikuwa na kazi ya kulinda msafara usishambuliwe na wanyang'anyi na mabedui wa jangwani. Kiongozi aliweza kufanya kazi hii kwa kuandikisha wapiganaji kutoka makabila mbalimbali na kuunda vikosi kufuatana na ukubwa wa msafara. Vikosi vilisindikiza misafara mpaka mwisho wa safari. Misafara yote iliyokwenda masafa marefu, ilikuwa chini ya ulinzi wa kijeshi.

Kiongozi wa msafara pia alitakiwa kuwa na kipaji cha pekee kwa kumuongoza kwenye jangwa lisilo na njia wakati wa mchana, na alitakiwa kuwa na uwezo wa kutambua njia ya msafara wakati wa usiku. Kiongozi alitakiwa kuwa na ujuzi wa kuzitumia nyota katika safari wakati wa usiku. Alikuwa anatakiwa kuhakikisha kuwepo kwa maji wakati wa safari ndefu ya kwenda Syria au kwenda Yemen. Alitakiwa kuchukuwa tahadhari dhidi ya majanga yasiyotegemewa kama vile kimbunga cha mchanga na msongamano wa miale ya taa za misafara.

Kiongozi pia, alikuwa anatakiwa kuwa na uwezo wa kutoa huduma ya kwanza ya tiba endapo msafiri aliugua au aliumia. Kwa ujumla, kiongozi alitakiwa kuwa na uwezo wa kushughulikia dharura yoyote ile. Wafanyabishara wa Makka, walimteua kiongozi wa misafara yao baada ya kuchunguza historia yake kwa uangalifu sana. Jopo la wasafiri wazoefu lilipitia majina ya watu waliopendekezwa kwa kazi hiyo.

Jopo la wachunguzi halikuridhishwa na sifa yoyote iliyo chini ya kiwango cha uwezo wa kiongozi wa msafara kuongoza kwa ustadi kwenye njia zisizo na michoro kwenye "bahari" ya mchanga, na kufaulu kwake kurudisha misafara ya "meli za jangwa" yaani ngamia pamoja na mizigo yao nyumbani salama. Ili akubalike kwa jopo, mtahiniwa alitakiwa kuonyesha kwamba alikuwa na uzoefu wa kutosha sana kuhusu utaratibu wa usafirishaji wa misafara ya biashara na "vitambulisho" vyake vilitakiwa awe hana kosa.

Baba wa bi Khadija yaani mzee Khuwalid aliweza kushika nafasi hii muhimu ya uongozi wa misafala ya biashara.

Mama yake Khadija alikufa mnamo mwaka wa 575 A.D., na Khuwayled baba yake, alikufa mnamo mwaka wa 585 A.D. Baada ya kifo cha Khuwayled, watoto wake walirithi utajiri wake na waligawana mali hiyo. Utajiri una hatari zake. Utajiri unaweza kumfanya mtu akaishi maisha ya kubweteka na anasa.

Khadija alitambua tabia ya utajiri kwa undani, na aliamua kutoruhusu utajiri kumfanya yeye asifanye kazi. Khadija alikuwa na akili ya kiwango kisicho cha kawaida na uwezo wa tabia ya kuishinda changamoto ya utajiri, na aliamua kujenga himaya ya urithi kutoka kwa baba yake. Alikuwa na ndugu wengi lakini miongoni mwa wote hao, ni yeye peke yake ndiye aliyerithi uwezo wa baba yao kuwa tajiri. Lakini alionyesha katika kipindi kifupi sana kwamba hata kama hangekuwa amerithi utajiri wa baba yake, bado angeweza kupata utajiri kwa bidii yake mwenyewe.


Wale waliokuwa wakiuliza asili ya utajili wa mama huyu mtukufu ninaamini kuwa wamepata majibu. Mali zake zilitokana na urithi toka kwa wazazi wake na baba yake alikuwa tajiri wa kuaminika. 

Comments