ULAZIMA WA KUMSWALIA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) NA AALI ZAKE

ULAZIMA WA KUMSWALIA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) NA AALI ZAKE.
Sisi Mashia tunaamini kuwa kila anapotajwa Mtume ni lazima tuitikie swalallahu alayhi wa aalihi wa salam (s.a.w.w).
Hii inatokana na agizo la Allah pale ambapo yeye mwenyewe anatangaza wazi kuwa humtakia rehema Mtume, pale aliposema;
Hakika Allah na Malaika wake wanamtakia Rehema Mtume. Enyi ambao mmeamini mtakieni rehema juu yake na Msalimuni kwa (uzuri) wa Salamu.” (33:56).

Katika Aya nyingine ya Qur’ani Tukufu, Allah anasema. “Amani na iwe juu ya watu wa Ya Sin (Ahl Ya Sin),” yenye maana ya kizazi cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).
Aya hii inatuagiza kuwa tunapomtakia rehema Mtume ni lazima tuwatakie rehema kizazi chake pia kwa sababu yeye Allah ametuonyesha mfano ili nasi tuige kufanya hivyo.

Watu Wa Ya Sin Inawahusu Watu (Ahlulbayt) Wa Muhammad (s.a.w.w).
Wafasiri wote na Wanachuo wa madhehebu ya Ahlul Sunnah waljamaa wanakiri kwamba Allah amemuita Mtume kwa jina Ya Sin. Hivyo basi Ahli (watu wa) Ya Sin maana yake ni watu wa Muhammad. Miongoni mwa wengine, Ibn Hajar Makki, Mwanachuo wa Kisunni pamoja na kuwa na chuki sana dhidi ya Shia, lakini anasema katika “Sawa’iq Muhriqa” chini ya aya zilizonukuliwa katika kuwasifu Ahlul Bait, kwamba kikundi cha Wafasiri wamemnukuu Ibn Abbas (Mfasiri mkubwa wa Waumini) akisema kwamba Ahl Yasin maana yake ni Ahl Muhammad.
Kwa hiyo, Salaam, maamkuzi ya amani kwa Ahli Ya Sin yana maana Salaam kwa Ahli Muhammad.

Imam Fakhru’d-Bin Razi anaandika: “Ahli Bait wa Mtume wako sawa naye katika mambo matano:
1) Salaam: Salaam kwa Mtume na Salaam kwa Ahli Ya Sin (Ahli Muhammad) ni kitu kimoja.
2) Salawat (kutakia rehma) katika Swala kwa Mtume na Ahlul Bait wake, ambako ni lazima.
3) Tohara: Allah Anasema katika sura ya “Ta Ha” (20:1): “(Ewe Mtume) Msafi na tohara:” Ile aya ya tohara iliteremshwa katika kuwatukuza Ahlul-Bait (33:33).
4) Uharamu wa Sadaka: Sadaka haiwezi kupokelewa imma na Mtume au Ahlul-Bait wake.
5) Mapenzi: Mapenzi kwa Mtume maana yake ni mapenzi kwa Ahlul Bait wake.


Ndugu waislamu tujitahidi sana kumtakia rehema Mtume na Ahlulbayt wake ili tuweze kufaidika na malengo matukufu ya Allah kutokana na maagizo yake haya. Kinyume na hivyo ni balaa kwetu. Hapa ninakusudia wale wanaochukia kusikia neno ahlulbayt na humtakia rehema Mtume basi bila kuwataja Ahlulbayt wake kwa madai kuwa Uislamu hauna uhusiano na ukoo wa Mtu. Watu hawa wamepata hasara kubwa maana wamepoteza faida kubwa ya kuombewa msamaha na Ahlulbayt na swala zao hazikubaliwi.

Comments