KABLA YA UISLAMU, WAARABU WALIKUWA WAUAJI WA WANAWAKE

KABLA YA UISLAMU, WAARABU WALIKUWA WAUAJI WA WANAWAKE

Mwenyezi Mungu anasema, "Na mmoja katika wao anapopewa khabari ya mtoto wa kike, husawijika uso wake akajaa sikitiko!. (Akawa) anajificha na watu kwa sababu ya hatari mbaya aliyoambiwa! (anafanyashauri) Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni (karibuni na hali ya kuwa mzima ili afe)? Sikilizeni! Ni mbaya mno hukumu yao hiyo. (Qur'ani 16:58-59).

Mara nyingi Mwarabu alimuua mwanae wa kike kwa kuogopa kwamba angekuwa mateka wa kivita wakati wa vita vya kikabila, na kwa hiyo, kuwa mtumwa wa adui, na daraja lake kama mtumwa kungeleta aibu kwa familia yake na kabila lake. Angeweza pia kumuua kwa kuhofia kwake umasikini. Aliamini kwamba binti yake angekuwa tatizo la kiuchumi kwake. Uislamu ulifanya mauaji ya watoto kuwa ni dhambi kubwa kabisa.

"Wala msiwaue wana wenu kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni hatia kubwa." (Qur'an 17:31).

Vilevile walikuwepo Waarabu ambao hawakuwaua watoto wao, lakini waliwanyang'anya haki zao zote. Walifikiri kwamba kwa vile binti zao watakapoolewa watakwenda kuingia nyumba nyingine za waume wao, hapakuwepo na haja ya kutumia gharama yoyote juu yao. Ilikuwa katika mazingira ya namna hii ambayo Khadija alizaliwa, akakua na kuishi mazingira ya "kumkataa mwanamke." Kutokea nyumbani kwake Makka, Khadija aliendesha biashara iliyokuwa inaendelea kukua na kuenea kwenye nchi za jirani. Kile ambacho alikwisha faulu kukipata kingekuwa cha kusifika katika nchi yoyote, katika kipindi chochote na kwa mtu yoyote mwanamume au mwanamke. Lakini mafanikio yake yamesifika mara mbili pale ambapo mtu atafikiria ule "mfumo-dume" wa kumpinga mwanamke, ulioendekezwa na Waarabu.

Huu ni uthibitisho wa uwezo wake wa kumudu hatima yake kwa kutumia akili yake, nguvu ya dhamira na tabia. Wafanyabiashara wenzake walikubali mafanikio yake walipomwita Malkia wa Makuraishi na Malkia wa Makka.

Comments